JESHI LA POLISI ARUSHA KUFUNGUA AKAUNTI BENKI ILI KUPAMBANA NA UHALIFU.
Afisa Mnadhimu namba wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Japhet Lusingu akitoa ufafanuzi wa mada mbalimbali zilizojadiliwa kati ya Jeshi hilo na wadau wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Bwalo la Afisa wa Polisi (Police Officers Mess) mwishoni mwa wiki. Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha.
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha.
Wadau wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha kutoka kada mbalimbali wakiwemo wanasheria, wafanyabiashara na wafanyakazi kutoka sekta binafsi na za kiserikali wamedhamiria kufungua Akaunti benki kwa ajili ya kuliwezesha Jeshi la Polisi katika kupambana na uhalifu.
Hayo yalielezwa na wadau hao wakati wa kikao cha kujadili usalama wa mkoa huu kilichofanyika kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi (Police Officers Mess) mwishoni mwa wiki kati yao na Viongozi wa Jeshi la Polisi mkoani hapa. Wadau hao walisema kwamba wawezeshaji wa Jeshi hilo ni wana Arusha wenyewe hakuna mtu yeyoye atakayetoka mkoa mwingine kwa ajili ya kuliwezesha Jeshi la Polisi mkoani hapa.
“Tunataka Arusha iwe mfano na mikoa mingine iige, bila kuwawezesha Polisi hatuwezi kukomesha uhalifu na tunatakiwa tuwawezeshe ili tupate nafasi ya kuwalaumu, hivyo basi nashauri iundwe Kamati ndogo itakayowajumuisha Polisi na Wananchi ambao watafanya harambee kwa watu mbalimbali”. Alisema Kiomoni Kibamba ambaye ni Mwanasheria wa Halmashauri ya jiji la Arusha.
Wadau hao walisema pamoja na Mfuko huo kutumika kuliwezesha jeshi la Polisi katika kuongeza bajeti ya mafuta na vifaa vingine lakini pia utakuwa unatumika kuwapa motisha wale wote watakaokuwa wanaliwezesha Jeshi hilo kuwapa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuonyesha kuwa wanathamini mchango wao.
Mbali na mada mbalimbali zilizokuwa zinajadiliwa siku hiyo pia wadau hao walilishauri Jeshi la Polisi Mkoani hapa kuwa makini na waendesha pikipiki yaani Boda Boda na ikibidi kila pikipiki inayotumika kusafirisha abiria iwe na makazi ya maegesho yanayojulikana ili tukio la uhalifu linapotokea askari wawe wanapata pa kuanzia katika suala zima la upelelezi.
Walisema kwa sasa pikipiki hizo zinafanya kazi mpaka usiku hivyo kama kuna uwezekano wangewekewa ukomo hasa muda wa usiku badala ya kufanya biashara hiyo mpaka asubuhi kwani baadhi yao wanatumia mwanya huo na kujiingiza katika vitendo vya kihalifu.
Awali akifungua kikao hicho Katibu wa kikao hicho Bw. Adolph Olomi ambaye pia ni Mwenyekiti wa TCCIA mkoa wa Arusha, alisema kwamba pamoja na mambo mengine lakini pia lengo la mkutano huo ni kufahamiana ili kupunguza kama si kuondoa kabisa pengo kati Jeshi hilo na wananchi hali ambayo itasaidia kuwa na ukaribu utakaosaidia kushughulikia matatizo ya kihalifu kabla hayajatokea.
Kwa upande wake Afisa Mnadhimu namba moja wa Jeshi hilo mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Japhet Lusingu aliwataka wadau hao watoe taarifa za wahalifu na uhalifu kupitia kwa viongozi wa Jeshi hilo ili kupunguza malalamiko juu ya uvujaji wa taarifa hizo.
(ACP) Lusingu aliongeza kwa kusema kwamba, hata watoa taarifa mara baada ya kutoa taarifa Polisi wanatakiwa wakae kimya bila kumshirikisha mtu yeyote kwani hali hiyo inasababisha majirani kumfahamu mtoaji wa taarifa hizo na baadae wahalifu kumfahamu kisha lawama kuliangukia jeshi la Polisi hivyo akasisitiza kwamba usiri unatakiwa kuanzia kwa mtoa taarifa mwenyewe.
Akitoa mada katika kikao hicho Mkuu wa kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi (SSP) Mary Lugola alisema kwamba, umefika wakati muafaka kwa Jeshi la Polisi na wananchi wote kufanya kazi kwa ukaribu zaidi ili kuweza kuimarisha usalama. Alisema kikao hicho ni moja ya mpango mkakati wa kuhakikisha mkoa wa Arusha unakuwa salama hasa ikizingatiwa pia ni kitovu cha shughuli za kitalii.
Naye Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha Mrakibu wa Polisi (SP) Francis Duma alisema kwamba, Falsafa ya Polisi Jamii ilikuja baada ya kuona kuna pengo kubwa kati ya Polisi na Jamii hivyo kuondoshwa kwa pengo hilo kumesaidia pande hizo mbili kuwa karibu.
Alisema Polisi pekee bila kushirikiana na wananchi haiwezi kukomesha uhalifu ikizingatiwa kwamba, kutokana na sensa ya mwaka 2012 uwiano unaonyesha kuwa, Polisi mmoja anatakiwa ahudumie kaya 1300 kwa masaa 24 bila kupumzika, hivyo ukomeshaji wa matukio ya uhalifu utafanikiwa endapo wanajamii nao watajitoa ipasavyo katika suala zima la kuimarisha usalama.
0 comments:
Post a Comment