Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Samwel Sitta.
Aidha, amesema kama moja ya makundi yaliyopo kisheria yangelijiondoa Bunge hilo lingelazimika kusitishwa.
Sitta alitoa kauli hiyo jana wakati alipokutana na ujumbe kutoka Mfuko wa Waandishi wa Habari (TMF) walioambatana na baadhi ya waandishi kutoka vyombo mbalimbali na walimu wao.
Alisema wanaosema kwamba Bunge hilo liahirishwe kwa sababu linatumia fedha za wananchi wanapaswa kufahamu kwamba kuahirishwa kwake ni kupoteza zaidi fedha hizo.
“Wanaosema Bunge lisitishwe mimi nawashangaa kwa kuwa fedha zilizokwishatumika tangu mchakato huu ulipoanza miaka mitatu iliyopita ni nyingi ukilinganisha na kipindi kilichobakia,” alisema.
Alisema ni bora Bunge hilo likaendelea katika muda mchache uliobaki ili kuokoa fedha za wananchi kuliko kuukatisha mchakato wakati fedha nyingi zimeshatumika.
Alisema vikao vya Bunge hilo kwa sasa vinaendelea kwa mujibu wa sheria na kwamba, akidi imetimia kwa kuwa wajumbe waliobaki ni 462 kati ya 629.
Sitta alisema, Bunge hilo lingeweza kusitishwa kama wajumbe wa kundi moja wangetoka wote kama vile kundi kutoka Baraza la Wawakilishi au kundi la 201 kwa kuwa makundi haya yapo kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Kundi jingine ni la wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akijibu hoja ya aina ya katiba itakayotokea alisema yeye anaaamini katiba itakayopendekezwa mara baada ya kumalizika kwa bunge hilo itakuwa bora kuliko iliyopo sasa.
Alisema wanachofanya ni kufuata sheria na wataendelea kufuata sheria mpaka Katiba hiyo itakapopatikana.
Akizungumzia uhuru wa vyombo vya habari, Sitta alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo imeridhia maoni yaliyowasilishwa na Jukwaa la Wahariri (TEF) ya kuanzishwa kwa Baraza la Habari kuwasilisha kwa kamati kwa majadiliano.
Pamoja na kusisitiza kwamba wajumbe wa kamati mbalimbali wanaona suala hilo na uhuru wa vyombo vya habari, mwenyekiti huyo alisema kwamba kutokuwepo kwa uwazi katika uendeshaji wa Serikali ni kikwazo hali inayosababisha waandishi wa habari kufanya kazi katika mazingira magumu.
Aidha alisema, kutoruhusiwa kwa waandishi kuingia kwenye kamati kumelenga kuondoa utata kwani ladha na vionjo vya waandishi katika mijadala ya wazi inaweza kuwa kikwazo kwa wananchi.
Alisema ni lengo la Bunge ni wananchi kujua kila kitu hasa majadiliano ya wazi yatakapoanza Septemba mbili mwaka huu Bunge litakapokutana.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment