BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MWALIMU MKUU ATOA AMRI KWA WANAFUNZI ILI WAMZEMEE MZAZI KISHA KUMPIGA MAWE JIJINI DAR ES SALAAM.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, inadaiwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Darajani iliyoko Tabata katika Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam kuamuru wanafunzi wake kumzomea mzazi aliyefika shuleni hapo kuhoji juu ya michango wanayodaiwa wanafunzi mara kwa mara.
Mzazi huyo mbali na kutaka kujua ukweli wa michango hiyo, pia alilenga kulipia michango mingine ukiwamo wa ulinzi.

Tukio hilo limetajwa kutokea Jumanne wiki hii, baada ya mzazi huyo aliyetajwa kuwa ni Tausi Mahmoud kufika shuleni hapo mbali na kuwa na mchango wa ulinzi alitaka pia kulipia ada ya mitihani ya majaribio aliyokuwa akidaiwa mtoto wake.

Habari kutoka kwa chanzo cha kuaminika cha gazeti hili kinasema katika majadiliano baina yao, yalitokea majibizano na kutokuelewana na ndipo Mwalimu Mkuu aliyetajwa kuwa ni Kabuta ambaye aliamuru wanafunzi kumzomea na kumfukuza kwa mawe mzazi huyo.

Tukio hilo limetajwa kuripotiwa katika kituo cha Polisi Tabata Shule, ingawa Kamanda wa mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Mary Nzuki alipoulizwa juu ya tukio hilo alisema halijamfikia na kwamba atafuatilia.

Lakini habari zaidi, ikiwa ni pamoja na kutoka kwa mzazi wa mtoto husika, zinasema ni kweli kumekuwa na tukio hilo. Mzazi huyo alipotafutwa na gazeti hili, alisema;

“Inasikitisha sana, mwalimu ambaye wazazi tunaamini wanalea watoto wetu leo anawaamuru wanafunzi kunifukuza kwa mawe na kunizomea kama mwizi mimi mzazi, huu ni udhalilishaji mkubwa sana kwangu na kwa mwanangu,” alisema.

Aliongeza kuwa, siku ya tukio alifika shuleni hapo kwa kulipia michango, lakini baada ya kulipa alionana na mwalimu mkuu na kumhoji kwanini mtoto wake adaiwe fedha za malipo ya masomo ya ziada kwa mwezi ambao hakusoma kabisa na pia kwanini akataliwe asisome tena.

“Nilishambuliwa kwa maneno kama nimekosea kuhoji, mwalimu mmoja akasema akili yangu na ya mwanangu sawa sawa, maneno hayo naambiwa mbele ya mtoto wangu,” alisema mama huyo.

Anasema baada ya kuhoji alishambuliwa kwa maneno na mwalimu mkuu pamoja na walimu wengine na kutaka kufungiwa ofisini ili akaitwe Mtendaji wa Kata hiyo, Chacha Mwenge na ndipo akaamua kuondoka, hali iliyomfanya Mwalimu Mkuu kuwaita wanafunzi na kumzomea.

Inaelezwa kuwa, wanafunzi hao licha ya kumzomea walimfukuza kwa mawe hadi nyumbani kwake ambako waliendelea kuipiga nyumba kwa mawe hadi mumewe alipotoka nje na wanafunzi hao kukimbia.

Mwalimu Kabuta hakupatikana kuzungumzia suala hilo, ingawa ilielezwa baada ya mzazi huyo kushitaki kituo cha polisi huko Tabata na pia kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, naye alikwenda Polisi, hivyo wote wawili kulalamikiana.

Ofisa Mtendaji wa mtaa huo hakupatikana kulizungumzia hilo, ingawa taarifa za baadaye zinasema mzazi aliyekwenda shuleni na kutofautiana na mwalimu, baadaye alichukuliwa na polisi hadi kituo cha Tabata shule kwa mahojiano.

Aliachiwa na kutakuwa kurudi tena leo. Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala ambayo ni mwajiri wa mwalimu huyo, Tabu Shaibu alipotafutwa na gazeti hili kwanza alikilaani kitendo hicho kama kweli kimetokea, huku akisema ni ukiukwaji wa maadili kwa sababu kila kazi inaongozwa na taratibu zake.

Aidha, alisema Mwalimu huyo anatafutwa aweze kutoa maelezo ya kina juu ya kilichotokea kabla ya kumchukulia hatua za kisheria.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: