VIONGOZI WA UKAWA BADO WATETEMESHA BUNGE MAALUMU LA KATIBA.
“Mambo siyo mepesi kama mnavyodhani, lakini yote haya yanaweza kumalizika ikiwa busara itatumika... kwa viongozi wa vyama vya siasa, kwa kila chama, kuweka mbele busara na utaifa kwanza na mchakato utaendelea vizuri,” Jaji Mutungi.
Dar es Salaam. Kikao cha maridhiano kati ya CCM na Ukawa chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kimeshindwa kufikia mwafaka.
Habari zilizotufikia wakati tukioenda mitamboni kutoka kwa mjumbe wa CCM, January Makamba zilisema wameshindwa kuafikiana.
Mjumbe mwingine kutoka Ukawa Magdalena Sakaya alisema wameshindwa kuafikiana na leo watakutana na waandishi wa habari kuzungumzia kwa undani.
Awali Jaji Mutungi akizungumza na Mwanachi kuwa hatima ya Watanzania kupata Katiba Mpya itategemea busara za viongozi wa vyama vya siasa.
Kauli ya Jaji Mutungi inakuja ikiwa zimebaki siku tatu kabla ya Bunge Maalumu la Katiba kuanza vikao vyake mjini Dodoma Agosti 5, mwaka huu huku kukiwa na sintofahamu kuhusu hatima ya mchakato huo.
Jaji Mutungi alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa mapumziko ya kikao kati yake na viongozi wa Vyama vya CCM, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kilichofanyika Hoteli ya Sea Cliff chenye lengo la kutafuta mwafaka wa mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.
“Ninavyoona mimi, hapa hatima ya Watanzania ya kupata Katiba Mpya itategemeana na busara za viongozi wetu wa vyama vya siasa pekee na si kitu kingine.”
“Mambo siyo mepesi kama mnavyodhani, lakini yote haya yanaweza kumalizika ikiwa busara itatumika... kwa viongozi wa vyama vya siasa, kwa kila chama, kuweka mbele busara na utaifa kwanza na mchakato utaendelea vizuri,” alisema Jaji Mutungi.
Alisema: “Kikao hiki ni muhimu sana, kwani kila Mtanzania anataka kujua nini hatima yake, lakini ninawasihi Watanzania watulie, wasubiri na nitakapokamilisha mazungumzo haya katika mazingira yoyote yale nitawaeleza tangu tulivyoanza hadi mwisho nini kilitokea.”
Kikao hicho cha mwisho kinafanyika baada ya vikao vitatu vya mwanzo kumalizika bila mwafaka wowote hasa kila upande kuwa na msimamo wake.
Msimamo wa Ukawa ni mjadala wa Bunge Maalumu la Katiba kuheshimu maoni ya wananchi yaliyomo katika Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba na upande wa CCM ni muundo wa muungano uwe wa serikali mbili badala ya tatu zilizo katika rasimu hiyo.
Mbali na kikao hicho, Kamati ya mashauriano iliyoundwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta iliyokuwa ikutane Julai 24 mwaka huu hakikufanyika baada ya Ukawa kutokuhudhuria kwa madai ya mwandaaji ndiye waliyemsusia Aprili 16 mwaka huu walipotoka ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo kutoka CCM ni, Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira ,Katibu wa Itikadi na Uenezi , Nape Nauye, mbunge Ilala, Mussa Azan Zungu na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai.
Wengine ni Mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Pia walikuwapo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee na Mbunge wa Mkanyageni, Habibu Mnyaa.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kuwa mvutano mkali ulikuwa ukiendelea baina ya wajumbe kutoka CCM na vyama vingine vinavyounda kundi la Ukawa.
Mjumbe mmoja wa kikao hicho alilidokeza gazeti hili kuwa kikao hicho hakikuwa na maelewano na kwamba kingeweza kuvunjika muda wowote.
“Kikao hiki kinaweza kuvunjika wakati wowote, hakuna maelewano,” alisema mjumbe huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake.
Habari nyingine zinaeleza kuwa baadhi ya wajumbe walikuwa wakitoa lugha za kuudhi kwa wenzao, hali ambayo ilichangia kumfanya Jaji Mutungi kufanya kazi ya ziada kuokoa jahazi.
Hata hivyo, baadaye saa 12:00 jioni wajumbe hao walitoka nje ya ukumbi na kukaa katika makundi Ukawa na CCM kila moja kupata msimamo wake kuhusu Katiba Mpya.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia baadhi ya wajumbe hao wakiwa katika makundi ambayo yalikuwa mbali kutoka kundi jingine ili kuepuka kusikia walichojadili wenzao.
Hata hivyo, vikao hivyo vilivyodumu kwa dakika 30, vilipokamilika wajumbe walirejea ndani ya ukumbi wa mkutano huku kila kundi likionyesha kushikilia msimamo wake.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment