WAZIRI MKUU AWAKERA ASKARI POLISI JIJIJINI MWANZA, AHANI MSIBA NA KUSHINDWA KUMJULIA HALI ASKARI ALIYEJERUHIWA WAKATI AKIPIMA AJALI ILIYOSABABISHA KIFO CHA MTOTO WA WAZIRI.
HATUA ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwenda kuhani msiba wa mtoto wa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga ‘Mawe Matatu’, bila kufika hospitalini Bugando kumjulia hali askari aliyejeruhiwa vibaya wakati akipima ajali iliyosababisha kifo hicho, imewakera askari polisi wakidai hawathaminiwi.
Pinda ambaye alikuwa mkoani hapa kwa ajili ya kuendesha harambee ya Taasisi ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alifika nyumbani kwa Kitwanga eneo la Misungwi juzi, kuhani msiba wa mtoto huyo, Vedastus Kitwanga, aliyepata ajali mbaya Agosti 19 mwaka huu, eneo la Njia Panda ya barabara ya Tanesco na Bandari wakati akimsaidia mwenzake aliyekuwa amepata ajali awali.
Wengine waliyofika kwa Kitwanga ni Mzee Mkapa na Mama Salma Kikwete, ambapo baadhi ya askari waliliambia gazeti hili kwamba, kitendo hicho cha viongozi kuishia nyumbani kwa kiongozi mwenzao pasipo kwenda Bugando kumjulia hali askari aliyejeruhiwa akitimiza majukumu ya kitaifa ni ubaguzi na kutowathamini.
“Sawa wana utashi wa kwenda kumfariji yeyote, lakini huyu askari mwenzetu WP 4132 Koplo Hamida aliyelazwa Bugando alijeruhiwa wakati akipima ajali iliyosababisha kifo cha mtoto wa Kitwanga. Huyu naye bado alihitaji faraja ya viongozi wetu hao, ila hawakufanya hivyo…
“Pinda alikuwa hapa mjini, ameendesha vikao vya CCM usiku na kutangaza nia ya kugombea urais, halafu kesho yake akapata muda wa kwenda Wilaya nyingine ya Misungwi kwa Kitwanga kuhani msiba wa mtoto wake, lakini Bugando pamekuwa mbali… Labda kwa sababu Hamida si mtoto wa kiongozi,” walidai askari hao walioomba kuhifadhiwa majina yao.
Vedastus Kitwanga na rafiki yake Gasper Mroso, walifariki ajalini kwa kugongwa na gari wakati walipokwenda kumsaidia mwenzao aliyekuwa amepata ajali eneo hilo, ambako wakati WP Hamida akiendelea kupima ajali hiyo, ghafla lilitokea gari lingine na kuwagonga wote.
Inaelezwa kuwa, awali mwenzao huyo alimpigia simu Mroso kumwomba afike eneo
la ajali, ambaye naye alimpigia simu mtoto wa Kitwanga na wakati wakiwa eneo la ajali ndipo likatokea gari lingine likawagonga na kusababisha kifo cha Vedastus pale pale huku Mroso akisagika vibaya miguu yote na kufariki kesho yake akipata matibabu Bugando.
WP Hamida ambaye ni askari wa kituo cha Nyamagana jijini hapa, alijeruhiwa vibaya ambako amelazwa Bugando pamoja na Kombo Mohamed aliyekatika miguu yote.TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment