BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CCM WATANUFAIKA NA KATIBA MPYA


Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mohamed Aboud Mohamed amesema Katiba inayopendekezwa, itaibeba CCM katika uchaguzi mkuu ujao visiwani humo.


Akizungumza katika mahojiano maalumu bungeni jana, Aboud alisema katiba hiyo itawasaidia katika kujibu kero mbalimbali zilizokuwa zikitolewa kwani imejibu asilimia 90 ya kero hizo.


“Kwa asilimia zaidi ya 90 kero za muda mrefu za wananchi wa Zanzibar zimejibiwa. Kwa hiyo wananchi watajua kuwa tumeshughulika na kero zao kwa kuzipatia ufumbuzi,”alisema.


Aboud alisema watakwenda kwa wananchi wa Zanzibar wakiwa kifua mbele kufafanulia kero ambazo zimetafutiwa ufumbuzi na wajumbe wa Bunge la Katiba, wengi wao wakitokana na CCM.


“Mimi ninaamini kuwa wananchi wakipelekewa Rasimu ya Katiba hii inayopendekezwa na wakaiona kuwa imekidhi matakwa yao wataiunga mkono,”alisema Aboud katika mahojiano hayo.


Aeleza kuhusu urais 2015
Waziri huyo ambaye aliwahi kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar mara mbili (mwaka 2000 baada ya Dk Salmin Amour kumaliza muda wake na mwaka 2010 wakati Amani Abeid Karume alipokuwa akiondoka madarakani), alisema hatagombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015.


“Sina nia wala dhamira ya kugombea tena urais. Mimi dhamira yangu kubwa ilikuwa ni kuiunganisha Zanzibar kazi ambayo Rais aliopo (Dk Ali Mohamed Shein) ameifanya vizuri,”alisema.


Aboud alisema sifa ya Rais ni uadilifu na kuwaunganisha Wazanzibari na Watanzania kwa jumla, sifa ambazo zote amekuwa nazo Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk Shein. Hata hivyo, alisema kazi yoyote inayofanywa na mwanadamu inakuwa na upungufu, haiwezi kuwa kamili.


“Mimi nina uhakika matarajio ya Wazanzibari yamepata majibu katika Rasimu hii ya Katiba. Na ninaamini kuwa wataipokea vizuri. Lazima tufahamu kuwa Katiba ni mchakato,” alisema.


Aboud alisema kama kuna jambo ambalo hawakulipata katika mchakato wa sasa wa Katiba unaomalizika Oktoba 4 au hawakufikia mwafaka , kesho wanaweza kupata nafasi ya kulizungumza.


Alipoulizwa kero zilizopatiwa ufumbuzi katika Katiba hiyo, Aboud aliitaja kero ya mafuta na gesi ambapo sasa Zanzibar itakuwa na uwezo wa kushughulikia.


“Zanzibar sasa itaweza kutunga sheria na sera zake za kushughulikia mafuta na gesi, lingine lilikuwa ni ushiriki wa Zanzibar katika taasisi za kimataifa,” alisema Aboud.


Alisema Rasimu imetoa haki ya Zanzibar katika mikopo na imetoa fursa ya kupunguzwa kwa mambo ya muungano ambayo ilikuwa ni sehemu ya kero ya Wazanzibari.


Ukawa kuondoka bungeni


Aboud alisema Ukawa na wajumbe wanaotokana na CUF, kususia Bunge hilo, hiyo haitaathiri uendeshaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa vile bado wana umoja.


“Hawa walijitoa si kwa sababu hawaoni umuhimu wa Bunge la Katiba. Walijitoa kwa sababu waliamini suala la serikali tatu ni suala la msingi. Sisi tumeona mfumo wa Serikali mbili ndiyo utakaodumisha muungano,” alisema na kuongeza:


“Sisi tumejali sana masilahi ya wananchi, sasa wao pengine wamejali sana masilahi yao. Sisi tumeona kuwa mfumo wa serikali mbili ndiyo utaweka msingi wa muungano.”


Alisema pengine CUF wamejali sana faida watakazopata kutokana na mfumo wa serikali tatu.


“Wanajua wao kwa nini wanataka mfumo wa Serikali tatu. Lakini kwa mimi na imani kabisa serikali mbili ndiyo njia sahihi,” alisema Aboud.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: