BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CCM YAFANYA MAANDALIZI YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA, YAWAKUSANYA VIJANA NA KUWAPA MAFUNZO MAKALI MILIMA YA ULUGURU MOROGORO.

Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini, Abdullaziz Abood wa pili kutoka kulia akitelemka katika mtelemko mkali mara baada ya kufunga mafunzo ya vijana wa ccm katika kambi iliyokuwa katika milima ya Uluguru ya Morning Site. mbele ni Katibu wake.PICHA/MTANDA BLOG

Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini Abdullaziz Abood kushoto akimsikiliza Katibu wa CCM wilaya ya Morogoro Ally Issa wakati wa kufunga kambi ya siku sita ya vijana 54 wa umoja wa vijana wa ccm katika eneo la Morning Site kata ya Milimani iliyopo milima ya Uluguru ikiwa ni matayarisho ya kuwanoa vijana hao katika usimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni hapa nchini.PICHA/MTANDA BLOG

Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini Abdullaziz Abood akizungumza jambo wakati wa kufunga kambi hiyo. PICHA/MTANDA BLOG

Kada wa umoja wa vijana CCM, Herena Leo akikabidhiwa cheti na Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini AbdullazizAbood wakati wa kufunga kambi ya siku sita ya vijana 54 wa umoja wa vijana wa ccm kutoka kata 29 katika eneo la Morning Site. PICHA/MTANDA BLOG
Picha ya pamoja wahitimu, wakufunzi na mhe Abood.
 
Moja ya cheti cha mhitimu baada ya kuhitimu mafunzo hayo.

Na Mtanda Blog, Morogoro.

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeanza kutoa mafunzo ya ujasiri, ukakamavu na wajibu wa vijana wake katika uchaguzi wa serikali za mitaa, unaotarajiwa kufanyika nchini kote baadaye mwaka huu, lengo likiwa ni kukiwezesha kupata ushindi wa kishindo.


Mambo mengine yanayofundishwa katika mafunzo hayo ni, namna ya kuhamasisha wanachama na kusimamia uchaguzi huo ambao hata hivyo, haujafahamika utafanyika lini.


Kwa kawaida huko nyuma, uchaguzi huo unaotoa taswira ya uchaguzi mkuu kwa kuzingatia ushiriki wa vyama vya siasa, ulikuwa unafanyika Septemba ya kila baada ya miaka mitano.


Katika Manispaa ya Morogoro, chama hicho kinachotawala kimetoa mafunzo ya aina hiyo kwa vijana wake 54 kutoka kata 29.


Mafunzo hayo ya wiki moja yaliyofanyika katika kambi iliyokuwa imewekwa katika eneo la Morning Site,Milima ya Uluguru na yalifungwa juzi na Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdullaziz Abood .


Akizungumza katika hafla hiyo, Abood alisema mafunzo hayo pia yamewajengea vijana hao uzalendo wa kuipenda nchi na kuwa tayari kuitumikia kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.


Alisema kuwa chama chake sasa kinaelekeza zaidi nguvu zake katika kushinda uchaguzi huo wa kuwapata wenyeviti wa serikali za mitaa na vitongoji.


Aliongeza kuwa ili kufikia azma hiyo, CCM katika Manispaa ya Morogoro, imeanzisha kambi ya vijana wake kutoka kata zote 29 ili wajifunze mbinu mbalimbali za kukiwezesha kupata ushindi.


Abood alisema chama hicho kimejipanga ili kuhakikisha kuwa kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo na uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais unaotarajiwa kufanyika mwakani.


“Mafunzo haya kwa vijana hawa 54 yatawawezesha vijana wetu kujua namna ya kuhamasisha na kusimamia vyema uchaguzi wa serikali za mitaa na hatimaye kuiwezesha CCM kuibuka na ushindi wa kishindo, hilo linawezakana kama kila kada atajitoa mhanga kwa chama chetu.”alisema Abood.


Kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, mbunge huyo alisema sehemu kubwa ya ilani hiyo imetekelezwa kikamilifu.


Alisema hali hiyo inatoa fursa kwa wanachama wa CCM kuingia katika uchaguzi huo na ule mkuu, wakiwa na nguvu.


Mbunge huyo alielezea kusikitishwa kwake juu ya kitendo cha baadhi ya kata kushindwa kutoa vijana wake kwa ajili ya kujiunga na kambi hiyo.


Hata hivyo Abood aliwataka viongozi wa CCM ngazi ya wilaya, kuendelea kutoa mafunzo ya aina hiyo kwa vijana ili kuwawezesha kujua misingi ya chama chao.


Kwa mujibu wa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Morogoro, Ally Issa Ally, CCM katika Manispaa ya Morogoro inaongoza mitaa 260 kati ya mitaa 272.


Mitaa mingine 12 inaongozwa na vyama vya upinzani.


“Mheshimiwa Abood (mbunge) tunakuhakikishia kuwa katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa, tutarejesha mitaa hiyo 12 tuliyoipoteza katika uchaguzi uliopita,”alijigamba Ally.


Ally alisema masomo mengine ambayo vijana walioshiriki wameyasoma ni kanuni za Umoja wa Vijana wa CCM, itikadi ya CCM, huduma ya kwanza na elimu ya kujitegemea


Baada ya kuhitimu mafunzo hayo vijana hao walipewa vyeti na kuahidi kuwa waaminifu na waadilifu kwa nchi yao wa wako tayari kukilinda chama.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: