FEDHA ZA KAMPUNI ZAMTOKEA PUANI.
Dar es Salaam. Shahidi wa kwanza katika kesi ya wizi wa Sh23.4 milioni inayomkabili mfanyabishara Proches Mrosso (33), mkazi wa Mbezi Salasala, ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala jinsi mshtakiwa alivyokuwa akichukua fedha hizo kidogo kidogo hadi kujenga nyumba yake na kusababishia hasara kwa kampuni.
Shahidi huyo, Peter Shine (61), mstaafu na mshauri wa kampuni ya Woiso Original Production ya jijini Dar es Salaam, alieleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Hassan Juma.
Akiongozwa na wakili wa Serikali, Shine alidai kuwa akiwa katika ofisi ya kampuni hiyo, alielezwa kuwa kampuni imepata hasara ya Sh23 milioni.
Shine alidai baada ya hasara hiyo, walimwita Mrosso na kumhoji kuhusu tukio hilo na alikiri kuchukua fedha hizo kwa nyakati tofauti.
Shine aliendelea kudai kuwa baada ya mshtakiwa kukiri tuhuma, alidai kuwa alitumia fedha hizo kununua kiwanja maeneo ya Mbezi na kujenga nyumba yenye vyumba vitatu.
Hata hivyo, mshtakiwa alipendekeza kwa mkurugenzi wake kwamba nyumba hiyo iuzwe na fedha itakayopatikana ilipe fidia ya hasara aliyosababisha na hatua hiyo ifanywe kwa maandishi.
Pia alidai baada ya kukubaliana kwa maandishi, walipanga siku ya kwenda kuiona nyumba hiyo, lakini mshtakiwa hakutokea hadi alipokamatwa na polisi.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment