KILA AKILI YA MWANASIASA IPO KATIKA NDOTO YA KUWA RAIS 2015 TANZANIA BARA AMA ZANZIBAR LAKINI HUYU NDIYE ANAYELEKEZA AKILI ZAKE KUWA RAIS WA ZANZIBAR 2015.
MBUNGE wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF) ametangaza kugombea urais wa Zanzibar huku akimtuhumu na kumkosoa Katibu Mkuu wa chama chake, Seif Sharif Hamad.
Alitumia jukwaa la Bunge Maalum la Katiba kumshambulia Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, akisema ni kiongozi mwenye lengo la kuvunja muungano.
Baada ya Mwenyekiti, Samuel Sitta kumpa fursa ya kuzungumza, mbunge huyo alisema anatumia nafasi hiyo kumjibu Seif, ambaye juzi alirushwa na kituo kimoja televisheni, akitoa tuhuma mbalimbali kwake kuhusu yeye kubaki bungeni na kamati namba tano aliyokuwa anaiongoza.
Hamad alisema Seif ametoa shutuma nyingi za uongo dhidi yake, kwa sababu amepata taarifa kuwa yeye Hamad ana nia ya kugombea urais wa Zanzibar na hilo kwake limekuwa tatizo kubwa.
“Nilitaka kugombea ukatibu mkuu ukanitimua, sasa huna nafasi ya kunitimua ninapoenda kugombea urais, na kweli nagombea urais. Nilikuwa sijasema naenda kugombea wapi, leo nasema naenda kugombea Zanzibar…asiingiwe na kiwewe,” alisema Hamad Rashid huku akishangiliwa na wajumbe wenzake.
Hamad alisema atagombea urais kama mgombea binafsi, kama itakubalika kwenye Katiba, lakini kama hilo litakataliwa, atagombea urais wa Zanzibar kupitia chama ambacho yeye ni mshauri wake cha Alliance For Democracy Change (ADC).
Kuhusu madai kwamba amebaki bungeni kwa sababu ana uchu wa madaraka, Hamad alisema “Mimi sijagombea mara nne urais, wala sijawahi kutoka makamu mwenyekiti wa chama nikawa katibu mkuu na nikarudi tena kuwa makamu wa chama halafu nikarudi tena kuwa katibu mkuu wa chama sijawahi.” Hamad alisema Seif ni kiongozi ambaye anatakiwa kuwa wazi na sio kuwa na sura mbili, kwani anawayumbisha watu.
Alihoji, “Kiongozi kama huyo akiwa amri jeshi mkuu mwenye sura mbili si jeshi lote litapigwa kwa sababu atakuwa anawayumbisha watu.”
Akijibu tuhuma mbalimbali, ikiwemo ya kwamba Hamad yuko bungeni kwa sababu ya upendeleo anaofanyiwa na spika wa Bunge, Anna Makinda kwani kesi aliyoifungua mahakamani ilikwishaisha, Hamad alisema kesi hiyo haijaisha na itaendelea kusikilizwa tena Septemba 26 mwaka huu.
Hamad alisema Makinda alikuwa makini katika kushughulikia suala lake la kuvuliwa uanachama, kwani hakutaka kuingilia masuala ya mahakama, bali aliiachia mahakama itoe uamuzi wake na yeye atafanya uamuzi wa kisheria.
“Kwa hiyo kumpandikizia lawama spika, sio jambo jema, ni vyema Maalim Seif amwombe radhi ” alisema Hamad.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment