
MIPANGO ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kuandamana katika mikoa mitatu ikiwemo ngome yake ya Arusha jana imeshindikana baada ya polisi kuwanyima vibali na kutanda maeneo muhimu kwenye mikoa hiyo kwa ajili ya kuwadhibiti.
Gazeti hili limebaini katika mikoa ya Arusha, Morogoro na Iringa kulikopangwa kufanyika maandamano hayo jana hali ilikuwa tofauti na ilivyotarajiwa kwani hakuna mfuasi wa chama hicho aliyejaribu kuingia mtaani kuandamana pamoja na kuwepo magari machache yaliyozunguka huku na kule kuhamasisha watu kuandamana.
Mikoa yote hiyo imezuiwa na polisi kuandamana kwa kunyimwa vibali licha ya kuomba kwenye jeshi hilo na Polisi makao makuu imetoa sababu za kuzuia maandamano hayo.
Imesema kuruhusu maandamano hayo ni kuingilia uhuru wa Mahakama kutokana na kwamba kesi ya kuhoji uhalali wa kuendelea kwa Bunge la Katiba inaendelea mahakamani na pia bunge hilo la Katiba lipo kihalali kisheria na linaendelea na vikao vyake mjini Dodoma kihalali.
Mkoani Arusha wafuasi wa chama hicho kuanzia jana asubuhi hadi jioni wameshindwa kujitokeza na kuandamana kwa ajili ya kupinga Bunge la Katiba linaloendelea mkoani Dodoma, kama Makao Makuu yalivyowaagiza ili kupinga kuendelea kwa mikutano ya Bunge la Katiba.
Mwandishi wa habari hizi tangu jana asubuhi hadi jioni alitembea maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha ambayo awali yalitangazwa kama njia za wafuasi wa chama hicho kupita lakini hakukuwa na maandamano yoyote wala mikusanyiko ya watu badala yake kila sehemu polisi wamekaa tayari kwa ajili ya kudhibiti maandamano hayo.
Maeneo ya kona ya Nairobi, Stendi kubwa na ndogo polisi walionekana wakiwa ndani ya magari yao pembeni wakilinda doria wakati maeneo ya Sanawari walikuwa wamekaa pembeni ya kituo cha kuuzia mafuta huku eneo la Phillips kukiwa na gari la maji ya kuwasha pamoja na gari dogo la Polisi.
Baadhi ya wananchi waliokuwa wakipita huku na kule na kuendelea na shughuli zao za kila siku, walisema kuwa maandamano hayo hayana maana kwani hayajaruhusiwa na polisi hivyo atakayejitokeza kwenye maandamano hayo yatakayomkuta asilalamikie polisi.
Mmoja kati ya wananchi hao, Lucas Emmanuel alisema kuwa ni vyema watu wakaendelea na shughuli zao za kila siku badala ya kujiingiza kwenye masuala ya siasa kwani wanaoumia ni wananchi na si viongozi wa vyama.
“Nawaomba wananchi msikubali kutumiwa na hao wanaotaka maandamano wajitokeze waone maana hakuna nchi inayokubali watu kuamka tu na kufanya maandamano yasiyokubaliwa kisheria na kwa nini hatufanyi maendeleo badala yake ni vurugu tu na kuhamasisha watu kuandamana watu wanahitaji amani na maendeleo na si fujo,”alisema Marieth Kimario, mkazi wa Sanawari.
Lema asema ‘wamebip’
Hata hivyo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema kuwa chama hicho jana hakijapanga kuandamana bali kutangaza kwao kuandamana jana ni mchakato wa maandamano ambayo yatakuwa ya kisasa zaidi.
Lema aliyasema hayo eneo la Philips ambapo alikuwa akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari waliotaka kujua ni kwa nini jana walitangaza maandamano jijini Arusha lakini hayajafanyika na je walikuwa wameogopa au la.
Alisema wafuasi wa chama hicho hawajaogopa kuandamana jana bali kutangaza kwao nia ya kuandamana ni kupima uwezo wa polisi jinsi ulivyo huku akisisitiza kuwa maandamano makubwa ya kisasa na ya aina yake yanakuja Arusha na yatafanyika.
“Si mnaona polisi ndio wametulinda sisi mi nimekaa zangu hapa pub (baa) nakula na kunywa ila leo (jana) tumewapima wamejipanga vipi lakini maandamano makubwa yanakuja na tunashukuru mbinu zetu tulizopanga hawazijui hivyo wajiandae tena muda wowote kuanzia sasa tutafanya maandamano yasiyozuilika,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu alisema kuwa chama hicho jana kimeanza mchakato wa kuanza maandamano na muda wowote maandamano hayo yatafanyika.
Alisema Chadema wamechoka kusikia habari za watu kufa au kuumia ndio maana jana wamepima uwezo wa polisi ulivyo lakini muda wowote maandamano yatafanyika kufikisha kile wanachokitaka kwa jamii na Serikali kwa ujumla.
Aliongeza kuwa kwa jinsi hiyo ya jana walivyokuwa wakizunguka maeneo mbalimbali ya jiji hilo na viunga vyake wamepata hamasa kubwa ya kuanza maandamano na watafikisha ujumbe kwa mtindo wa kipekee.
Iringa waeleza kilichowazuia
Mkoani Iringa chama hicho Jimbo la Iringa Mjini jana wameshindwa kufanya maandamano ya amani kama ilivyotangazwa kwa kile kilichoelezwa na Mwenyekiti wake, Frank Nyalusi wamezuiwa na polisi kuandamana.
Akizungumza na HabariLeo jana, Nyalusi alisema walitoa taarifa kwa jeshi hilo siku mbili zilizopita wakielezea nia yao ya kufanya maandamano hayo ikiwa ni kuitikia wito uliotangazwa na Mwenyekiti wao wa Taifa, Mbowe wa kufanya maandamano ya amani yasiyo na ukomo yenye lengo la kushinikiza kusitishwa kwa Bunge la Katiba.
Alisema pamoja na jeshi hilo kuwazuia kufanya maandamano hayo, jana hiyo hiyo waliruhusiwa kufanya mkutano wa hadhara ulifanyika mtaa wenye machinga wengi maarufu kama Magari Mabovu, Kitanzini.
Wakati Chadema wakidai kudhibitiwa kufanya maandamano hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema jeshi hilo halijapokea barua yoyote kutoka katika chama hicho inayoonesha wameomba kufanya maandamano hayo.
Akitoa ufafanuzi huo kwa njia ya simu, Mungi alisema “nchi hii kama zilivyo nchi nyingine inaendeshwa kwa sheria, taratibu na kanuni, Watanzania bila kujali wanatoka kundi gani ni lazima wafanye mambo wanayotaka kufanya kwa kuzingatia sheria vinginevyo mkono wa sheria utawafukuzia,” alisema.
Morogoro hali ilikuwaje?
Kwa upande wa Morogoro mjini, hali ilikuwa shwari na wafuasi wa Chadema walitii amri ya Polisi hawakuandamana. Pamoja na kuwepo kwa ushwari huo, bado Jeshi la Polisi mkoani hapa liliendelea kuimarisha ulinzi kwa kuwasambaza askari mitaa mbalimbali.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, aliendelea kusisitiza kuwa maandamano ya Chadema mkoani hapa yamezuiwa na ulinzi umeimarishwa.
Polisi wanasemaje?
Wakati hayo yakijiri Jeshi la Polisi limekionya chama hicho kuwa itakichukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria na kukitaka kutoendelea na maandamano hayo kwa kuwa ni batili na ni kinyume cha sheria.
Akizungumza na gazeti hili, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba alisema, maandamano hayo ni kinyume cha sheria kwa kuwa Bunge Maalumu la Katiba lipo kisheria na hata kuendelea kwake ni kwa mujibu wa sheria.
Msemaji wa Chadema Naye Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alisema kwa jana hawako tayari kuzungumzia lolote kuhusiana na kutofanyika kwa maandamano hayo kwani leo chama hicho kitatoa tamko lake.
Hata hivyo Chadema wamesisitiza kufanya maandamano hayo ambapo yanatarajiwa kuanza kesho katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Mara, Kilimanjaro pamoja na maeneo mengine nchini.
Maandamano hayo na migomo isiyo na kikomo iliitishwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe kwenye mkutano Mkuu wa Chadema uliomalizika hivi karibuni.
Kutokana na kauli hizo Mbowe aliitwa Makao Makuu ya Polisi ambapo alitii amri hiyo kwa kufika makao makuu hayo akiwa ameongozana na jopo la mawakili sita ambapo alihojiwa kwa saa nne.Hata hivyo baada ya Mbowe kutoa kauli hiyo, Jeshi la Polisi lilitoa kauli ya kupiga marufuku maandamano hayo.
Hata hivyo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara) John Mnyika alisema, katika mahojiano hayo Mbowe alionyeshwa video yenye kauli yake ya kuitisha maandamano na migomo nchi nzima bila kikomo, lakini alikana kuandika maelezo kuhusu kauli ya kuitisha maandamano nchi nzima.
Baada ya kuhojiwa Mbowe amekwenda Afrika Kusini kushiriki shughuli ya kichama.HABARILEO

0 comments:
Post a Comment