Mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa (kulia) akiwania mpira na beki wa
Mtibwa Sugar, Kessy Kidingile katika mchezo wa Ligi Kuu, kwenye Uwanja
wa Jamhuri, Morogoro. Picha na Juma Mtanda
‘Kweli Jaja mwisho Msamvu’! Mtibwa Sugar wamethibitisha kuwa makali ya mshambuliaji wa Yanga, Genlison Santos ‘Jaja’ mwisho Msamvu baada ya jana kuibuka na ushindi mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Ndanda FC iliyopanda daraja msimu huu inashikilia usukani wa ligi baada ya kuichapa Stand United 4-1, huku mabingwa watetezi Azam wakiibamiza Polisi Morogoro mabao 3-1.
Wakati Yanga wakichezea kichapo Morogoro watani zao Simba leo watakuwa Uwanja wa Taifa kuikabili Coastal Union.
Morogoro. Mshambuliaji Jaja aliyejijengea jina kubwa baada ya kuifunga Azam mabao mawili katika mchezo wa Ngao ya Jamii, jana mambo yalikuwa magumu kwake pamoja na kukosa penalti.
Washambuliaji wa Mtibwa Sugar, Mussa Mgosi na Ame Ally waking’ara kwa kufunga mabao mawili yaliyotosha kuzima kelele za mashabiki wa Yanga waliofurika kwa wingi kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Kocha Mecky Mexime amethibitisha ubora wake mbele ya baba yake Marcio Maximo aliyeshindwa kuvunja mwiko wa miaka mitano wa Yanga kushindwa kupata ushindi kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Mgosi alitumia vizuri makosa ya mabeki wa Yanga, walioshindwa kuokoa mpira uliomgonga vibaya Kelvin Yondani na kumdokolea kidogo kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ aliyekuwa ametoka golini kuwahi mpira huo.
Wakati watu wakidhani matokeo yangebaki hivyo dakika ya 82, Ally alipokea mpira mrefu na kumpiga chenga Nadir Haroub kabla ya kupiga shuti la juu nje kidogo ya 18, na kumwacha kipa Dida aliyeruka juu kupangua mpira huo, akijikuta akiusukumizia wavuni.
Kocha wa Yanga, Maximo alisema wamefanya makosa machache na wapinzani wao wameyatumia wakapata ushindi, hivyo anajipanga kwa mchezo ujao.
Naye kocha wa Mtibwa Sugar, Mexime alisema wanamshukuru Mungu amewasaidia kupata ushindi kwani Yanga ni timu nzuri na imecheza kwa ushindani.
Katika mchezo huo ulioanza kwa kasi, Mtibwa Sugar nusura wapate bao dakika ya nane baada ya Mgosi kupiga mpira wa kichwa uliotoka nje kidogo ya lango baada ya kupokea mpira wa kona wa David Luhende.
Kuingia kwa Simon Msuva kulibadili mchezo kwani Yanga waliamka na kucheza kwa kasi na kufanikiwa kupata penalti dakika ya 46, lakini hata hivyo Jaja alikosa penalti hiyo baada ya kupanguliwa na kipa wa Mtibwa, Mohamed ambaye aling’ara katika mchezo huo kwa kuokoa hatari nyingi zilizoelekezwa golini kwake.
Yanga waliendelea kulishambulia lango la Mtibwa na kufanikiwa kupata bao kupitia kwa Msuva dakika ya 49, lakini mwamuzi Dominic Kavemba alilikataa bao hilo kwa madai wachezaji wa Yanga waliotea.
Azam, Ndanda zafanya mauaji
Chamanzi. Mabingwa watetezi Azam waliutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani Azam Complex baada ya kuwachapa Polisi Morogoro mabao 3- 1.
Mshambuliaji Didier Kavumbagu alifunga mabao mawili na beki Aggery Morris alifunga bao moja huku Nahoda Bakari akifunga bao la kufutia machozi kwa Polisi.
Kavumbagu alifunga bao la kwanza dakika ya 14 kwa shuti akiunganisha krosi iliyopigwa na Kipre Tchetche aliyetumia uzembe wa kipa wa Polisi Moro, Tonny Kavishe aliyetoka golini.
Azam walipata bao la pili dakika ya 22 lililofungwa kwa kichwa na beki Morris akiunganisha mpira wa faulo uliopigwa na Tchetche.
Polisi Moro waliamka na kuanza kuwashambulia Azam na kufanikiwa kupata bao dakika ya 61, lililofungwa na Bakari kabla ya Kavumbagu kuifungia Azam bao la tatu dakika ya 90.
Shinyanga. Ndanda ‘kuchele’ baada ya kuwasambaratisha wenyeji Stand United kwa mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Kambarage.
Karamu ya Ndanda ilifunguliwa dakika ya 15 kwa bao la Paul Ngarema na kufuatiwa na mabao ya Nassoro Kapama (33), Ernest Mwalupani (42) na Elius Ndekezi (90) yaliyotosha kuipa ushindi timu hiyo ya Mtwara, huku wenyeji Stand United wakipata bao la kufutia machozi kupitia Kamana Salum.
Michezo mingine kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani, Prisons imeibamiza Ruvu Shooting mabao 2- 0 katika mchezo mkali na wa kusisimua wa maafande hao. Mabao ya Prisons yalipachikwa wavuni na Jacob Mwaitalako na Laurian Mpalile.
Nayo Mgambo JKT ilitumia vizuri uwanja wake wa Mkwakwani Tanga, kwa kuichapa Kagera Sugar bao 1- 0 lililofungwa na Ramadhan Pera. Kagera Sugar walishindwa kusawazisha bao hilo baada ya penalti iliyopigwa na beki Abubakary Mtiro kutoka nje.Washindi wa tatu msimu uliopita Mbeya City walilazimishwa sare 0-0 na JKT Ruvu kwenye uwanja wao wa Sokoine Mbeya.MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment