MWENYEKITI WA CCM AHUSISHWA NA TUHUMA ZA UJAMBAZI SIMIYU.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Abdulrahman Kinana,
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Mwamanyili Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, amepandishwa kizimbani baada ya kutuhumiwa kufanya unyang’anyi wa kutumia silaha na ubakaji katika kijiji cha Mwagulanja wilayani Busega.
Mtuhumiwa huyo, Ramadhan Msoka, akiwa na wenzake watatu, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Magu, chini ya ulinzi mkali wa polisi, Ijumaa iliyopita wakikabiliwa na mashitaka mawili ya jinai.
Akiwasomea mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Robert Masige, Mwendesha Mashitaka Mrakibu wa Polisi aliyetajwa kwa jina moja la Mkiwa, alidai kuwa washtakiwa hao walitenda makosa hayo Agosti 23, mwaka huu saa 7:00 usiku, eneo la Nassa Ginnery kijiji cha Mwagulanja wilayani Busega.
“Mheshimiwa hakimu, washtakiwa hawa kwa pamoja wanakabiliwa na makosa mawili, la kwanza la unyang’anyi wa kutumia silaha na la pili la kubaka kwa kundi,” alidai Mkiwa.
Alifafanua kuwa siku ya tukio hilo, washtakiwa wakiwa na silaha za jadi ambazo ni mapanga na fimbo, walimvamia Mwalimu Samuel Mkumbo na kumpora Sh. milioni 18 kwa kumpora na kisha kundi hilo kumbaka kwa zamu mpangaji wa mwalimu huyo (jina limehifadhiwa).
Aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Libent Rwegarulila, Ramadhani Msoga, Meshack Samson na Kubin Nkondo, wote wakazi wa eneo hilo katika kijiji cha Mwagulanja.
Aidha, aliiomba mahakama hiyo isiwape watuhumiwa hao dhamana kwa kuwa moja ya kosa linalowakabili halina dhamana pia upelelezi wa kesi hiyo namba 126 ya mwaka 2014, haujakamilika.
Hakimu Mfawidhi Masige alikubaliana na ombi la Mwendesha Mashitaka na kuieleza mahakama kwamba shitaka la unyang’anyi wa kutumia silaha, ni moja kati ya makosa ambayo mahakama zinazuiwa kutoa dhamana chini ya kifungu cha Sheria namba 148.
“Chini ya kifungu namba 148, kifungu kidogo cha 5 a (1) cha Mwenendo wa Sheria ya Mashitaka ya Jinai, Sura ya 20 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002, mahakama hii inawanyima dhamana hivyo mtakwenda rumande hadi hapo Septemba 9, mwaka huu kesi yenu itakapotajwa tena,” alisema hakimu huyo.
Washitakiwa hao ambao awali walikana makosa hayo, walirudishwa mahabusu ya mahakama hiyo kabla ya kupelekwa katika gereza dogo la wilaya hiyo.
Msoka ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, ni Mwenyekiti wa CCM wa kata ya Mwamanyili wilayani humo na Rwegarulila ni Mshauri wa Mahakama ya Mwanzo ya Nyashimo wilayani humo.
Kabla ya washtakiwa hao kufikishwa mahakamani, Jeshi la Polisi mkoani Simiyu lilisema lilikuwa likimsaka kwa udi na uvumba mshtakiwa mwingine wa tano ili aunganishwe na wenzake ambaye anadaiwa alikimbia. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment