Benjamin Mkapa
NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona, amedai mahakamani kwamba Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, alikuwa akifuatilia hatua kwa hatua na alikubali mchakato wa ukaguzi wa dhahabu ufanyike kwa haraka.
Yona alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alipokuwa akijitetea kwa kuongozwa na wakili wake, Elisa Msuya mbele ya jopo la mahakimu watatu linaloundwa na Jaji John Utamwa, Jaji Sam Rumanyika na Msajili Saul Kinemela.
Alidai kwamba mwaka 2002 kulikuwa na malalamiko kuhusu mapato ya madini ya dhahabu yaliyokuwa yakichimbwa na kampuni tano za kigeni na nyingine ndogondogo.
“Wizara ya Nishati iliamua kukaa na kuhakiki gharama za madini hayo, kwa kuwa BoT ndiyo iliyokuwa ikisimamia akaunti za kampuni hizo, iliziruhusu kufungua akaunti nje ya nchi, tulikubaliana kutafuta mkaguzi wa dhahabu.
“Gavana wa BoT na Wizara ya Nishati na Madini walianza mchakato huo na BoT ndiyo iliyokuwa ikisimamia mchakato huo wa kuhakikisha anapatikana mzabuni ambaye ni mkaguzi wa dhahabu kwa kufuata utaratibu,” alidai.
Alidai mchakato wa kumpata mkaguzi wa madini ya dhahabu ulifuata utaratibu na ulisimamiwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mshtakiwa huyo alidai baada ya majadiliano aliamua kumuandikia rais aliyekuwapo wakati huo, Benjamin Mkapa dokezo kuhusu ukaguzi wa dhahabu Mei 11, 2003.
Alidai alimfahamisha rais kwamba majadiliano waliyofanya kati ya Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha, BoT na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) yanaendelea vizuri.
Yona alidai kuwa Machi 3 mwaka 2003 alimwandikia rais dokezo kwa mara ya kwanza kumfahamisha kwa maandishi, akiomba aruhusu kutekeleza ukaguzi wa dhahabu kwa kufuata taratibu na sheria.
Alidai kuwa Machi 20, 2003 rais aliandika majibu kwamba anakubali waendelee na mchakato haraka.
“Tulimwahidi rais kwamba mchakato utazingatia mapato ya nchi na ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kweli katika hilo tulizingatia ushauri wa AG,” alidai.
Hata hivyo, Yona hakuweza kuendelea na utetezi baada ya Wakili wa Serikali, Oswald Tibabyekomya kupinga kupokewa kwa kielelezo kutoka ofisi ya AG.
Jopo la mahakimu kwa pamoja lilikubaliana kuahirisha kesi hiyo hadi leo kwa ajili ya kumpa nafasi Wakili Tibabyekomya kujiridhisha na kielelezo hicho.
Mbali na Yona, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Washtakiwa hao wanakabiliwa mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.
Inadaiwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda makosa hayo Agosti 2002, kwa kuisamehe kodi Kampuni ya Ukaguzi wa Madini ya Alex Stewart ya nchini Uingereza kinyume na sheria.
Kwa mara ya kwanza Mkapa alitajwa mahakamani na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mramba, wakati akitoa utetezi wake katika kesi hiyo mwaka 2012 akisema rais huyo mstaafu alibariki Kampuni ya Alex Stewart kuingia nchini kufanya ukaguzi wa mahesabu kwenye migodi iliyokuwa ikilalamikiwa.
0 comments:
Post a Comment