ANATUKERA ?, JAJI JOSEPH WALIOBA AWASHAURI WATANZANIA WASIKURUPUKE KUIPITISHA KATIBA MPYA.
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Bunda. Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amewataka Watanzania kutokurupuka kuipitisha Katiba Inayopendekezwa kwa kuwa imeyaacha kando maoni yao mengi na akawataka waisome kwa makini kabla ya kuikubali au kuikataa.
Akiwa katika likizo ya wiki moja nyumbani kwake Bunda, Mkoa wa Mara, Jaji Warioba alialikwa na vijana wa mji huo kupitia Jukwaa lao la Uwazi na Fikra Yakinifu, wakiomba azungumze nao kuhusu masuala mbalimbali hasa mchakato wa Katiba Mpya.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Harrieth, Jaji Warioba aliulizwa na kujibu maswali; anaionaje Katiba Inayopendekezwa na iwapo CCM imemgeuka kwa nini asihame chama?
Akijibu maswali hayo, Jaji Warioba alisema Katiba hiyo haina maoni yote ya wananchi kama Bunge Maalumu lilivyojinadi, bali yamewekwa machache ambayo hata hivyo yamo hata katika Katiba ya sasa.
Mathalan, alisema wananchi wengi walipendekeza kiwepo kipengele cha maadili ya viongozi ili kuwadhibiti dhidi ya vitendo viovu wanavyovifanya kwa sasa kama ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka, lakini wajumbe wa Bunge walikirekebishana hadi kikapoteza maana.
Kwa kufanya hivyo, alisema wajumbe hao walionyesha wanafurahishwa na hali iliyopo ya viongozi kukosa uzalendo, uadilifu na kukosa uwajibikaji hata kuwasababishia Watanzania maisha magumu ambayo kupitia maoni yao, walikuwa wameyatafutia dawa kwa kupendekeza maadili yatambulike kikatiba.
Alisema wananchi walipendekeza muundo wa muungano wa serikali tatu ili kuondoa matatizo yaliyopo, kupatiwa madaraka ya kuwawajibisha wabunge wao pamoja na rais kupunguziwa madaraka, mambo ambayo yameondolewa na Bunge hilo Maalumu.
“Kazi yetu kama Tume ya kuandaa Katiba ya Watanzania tuliimaliza. Bunge nalo limemaliza kazi yake japo ina upungufu. Sasa kazi imebaki kwenu wenye Katiba; kuisoma iliyopendekezwa kwa makini kabla ya kuipigia kura,” alisema Warioba.
Jaji Warioba alieleza kusikitishwa na taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa lililokuwa Bunge la Katiba, Samuel Sitta siku ya kukabidhi Katiba Inayopendekezwa kwa Rais, kwamba Bunge hilo limeweka ndani ya katiba hiyo asilimia 81 ya maoni ya Tume, akisema huo ni uongo mkubwa.
“Ukweli ni kwamba wamechukua asilimia 20 tu na kutupa nje asilimia iliyobaki na kubandika yaliyomo katika Katiba ya sasa ambayo hayawezi kuleta mabadiliko yoyote,” alisema Jaji Warioba.
Hivyo, Jaji Warioba aliwataka Watanzania kwa umoja wao bila kujali tofauti zao za kisiasa, dini, rangi, kabila kuhakikisha kuwa wanapata Katiba Inayopendekezwa na kutumia muda mwingi kuisoma kabla ya kuipigia kura na kuwa wakikurupuka watajuta siku za usoni.
Akizungumzia hatima ya Muungano wa serikali mbili uliopo kwa sasa, Warioba alisema hachelei kusema kwamba huenda ukakumbana na changamoto nyingi siku za usoni iwapo wananchi watauridhia kupitia kura yao kwa vile asilimia kubwa ya Wazanzibari hawaukubali.
“Hapa napo kuna tatizo, Mpaka mgogoro uliopo miongoni mwa Wazanzibari umalizwe. Wao wenyewe wanataka kuendeleza tamaduni zao ndani ya Zanzibar wanayoitambua kama nchi huru. Sidhani kama watakubaliana,” alisema Warioba.
Kuhusu kujitoa CCM, Jaji Warioba alisema hawezi kufanya hivyo, bali ataendelea kuwa mwanaCCM daima kwani anaamini katika chama hicho lakini akawaponda wanachama wenzake aliosema wanaweka masilahi binafsi mbele badala yale ya wananchi.
“Mimi ni mwanaCCM na nitadumu hivyo daima kwani ndicho chama ninachokiamini. Mimi siyo mwanachama masilahi ambaye akikosa kitu fulani au akiguswa kidogo tu anahamia chama kingine,” alisema Jaji Warioba.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment