WALIOKUFA KATIKA AJALI YA MOTO KWA KULIPUKIWA NA TENKI LA MAFUTA WAFIKIA SABA DAR ES SALAAM.
IDADI ya watu waliokufa kwa ajali moto iliyotokea baada ya lori la mafuta kupinduka eneo la Mbagala Charambe jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki imeongezeka na kufikia saba huku wengine hali zao zikiwa mbaya.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Uhusiano Msaidizi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Doris Ishenda, alisema kati ya majeruhi 11 waliolazwa juzi, wawili wamefariki dunia huku majeruhi saba bado hali zao ni mbaya.
Ishenda, alisema kwa sasa wamebaki majeruhi tisa hata hivyo kati ya hao saba hali zao ni mbaya na wawili hali zao za afya mpaka sasa zinaridhisha na bado wanaendelea kupatiwa matibabu.
Alisema walipokea majeruhi 15, kati ya hao wawili walifariki mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo na wengine wawili
walifariki usiku wake na kubaki 11, kati yao usiku wa kuamkia jana wamefariki wawili.
“Waliofariki ni Abasi Unganga (21), na Rodin Mazinga (24), majeruhi waliobaki Hospitalini ni Shaabani Lukoba (42), Said Idd (30), Ibrahim Ibrahim (26), Hamis Bande (25), Hamis Ally (32), Maganga Maganga (38), Mathayo Daniel (21), na Mothes Ismail (19),” alisema.
Ajali hiyo ilitokea Jumanne saa 5 usiku ambako lori aina ya Scania lenye namba T 464 CSR mali ya kampuni ya Moil Transporter lililokuwa likisafirisha mafuta kwenda Kampala Uganda kuanguka.
0 comments:
Post a Comment