BUNGE LAHAHA KUSAIDIA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII KULIPWA DENI LAO LILILOKOPWA NA SERIKALI LA SH TRIONI 8.4.
KATIKA kuhakikisha mifuko ya hifadhi za jamii nchini haitetereki kiuchumi, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imelazimika kuingilia kati kusaka suluhu ya hatima ya deni la Sh trilioni 8.4 ambalo Serikali inadaiwa na mifuko hiyo.
Serikali kwa nyakati tofauti imeripotiwa kukopa fedha kutoka katika mifuko hiyo kwa lengo la kuharakisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Kabwe Zitto alisema kamati yake imeamua kukutanisha Serikali, mifuko ya hifadhi za jamii, Mamlaka ya Kudhibiti mifuko hiyo (SSRA) na Gavana wa Benki Kuu, ili kupata suluhu ya tatizo hilo.
“Tunachotaka ni kuangalia namna ambavyo Serikali italipa madeni haya ili kuiwezesha mifuko hii iendelee kwa kuwekeza zaidi katika maeneo ya maendeleo, lakini pia kulipa mafao ya wanachama wake,” alisema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Pamoja na juhudi za kamati yake, alisema kuwa si jambo la ajabu kwa nchi kuendelezwa na mifuko ya jamii, akisisitiza kuwa nchi nyingi zilizoendelea zimepata maendeleo yake kwa kutegemea mifuko hiyo kwa kiasi kikubwa, lakini pia zimekuwa zikilipa madeni kwa wakati.
“Madhara ya mifuko hii kutokulipwa madeni haya ni makubwa kwa watanzania na kiuchumi kwa ujumla, kwani pamoja na kushindwa kuwekeza kwenye maendeleo, lakini pia itashindwa kuwalipa mafao wanachama wake, jambo ambalo ni hatari kwa mifuko hiyo,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hadi sasa Serikali inadaiwa na mifuko hiyo Sh bilioni 800 zilizotumika katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Hata hivyo, alisema deni la hifadhi ya jamii kwa serikali kwa ujumla linafikia Sh trilioni 8.4, kiasi kinachotokana pia na malimbikizo ya madeni.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka alisema ingawa Serikali inaendelea kulipa deni la Sh trilioni 7.6 la Mfuko wa PSPF, lakini ucheleweshwaji wa fedha ambazo Serikali imekopeshwa, inaiumiza mifuko kiuchumi.
Alisema endapo deni hilo litaendelea kucheleweshwa kulipwa kulingana na wakati mifuko mingi ya hifadhi ya jamii inaweza kufilisika na kusababisha madhara katika uchumi, lakini pia kushindwa kuwalipa mafao wanachama wake.
“Kama mfuko wa pensheni unawajibika kuwalipa wanachama wake mafao yao, na hatuwezi kutumia deni hili la Serikali kama sababu ya kushindwa kulipa, kwa hali hii utafikia muda mashirika haya yatashindwa kulipa kabisa mafao haya,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dk Servacius Likwelile aliihakikishia mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii nchini kuwa Serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha inalipa kwa hatua za haraka deni hilo la Sh trilioni 8.4 .
“Serikali inatambua juu ya wasiwasi uliopo kuhusu madeni haya na inafanya kazi kuliko ilivyo kawaida kuhakikisha deni hilo lote linalipwa kwa mifuko hiyo,” alisema Dk Likwelile.
Awali, akiwasilisha taarifa yake, Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Athuman Selemani alisema deni hilo linajumuisha mikopo ambayo Serikali ilikopesha mifuko hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Wakati PSPF ikiongoza kwa kuidai Serikali kiasi kikubwa cha fedha, Sh trilioni 7.6, Selemani ameyachambua madeni mengine ya mifuko kuwa Sh bilioni 192 inazodaiwa na Mfuko wa Pensheni wa PPF, Sh bilioni 467 inazodaiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Sh bilioni 107 inazodaiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Mifuko mingine inayoidai Serikali ni LAPF inayodai Sh bilioni 170 na GEPF (Sh bilioni 7.6). Hata hivyo, alisema ukubwa wa deni hilo unaweza kuongezeka kwa kuwa kiasi hicho cha Sh trilioni 8.4 hakihusishi michango ya wafanyakazi wa Serikali ambayo haijawasilishwa kwa mifuko hiyo hadi sasa.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment