
RAIS JAKAYA KIKWETE.
RAIS Jakaya Kikwete anakusudia kumaliza ujenzi wa barabara zote zinazounganisha mikoa na nchi jirani, kabla hajamaliza muda wake wa uongozi, ili kukamilisha ahadi yake ya kuiunganisha nchi kwa mtandao bora ya barabara.
Alisema hayo jana katika Kijiji cha Kisesa, Kata ya Kisesa wilayani Magu mkoani Mwanza, wakati alipoweka jiwe la msingi katika barabara ya Kisesa–Usagara, yenye urefu wa kilometa 16 inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Rais Kikwete alisema wakati alipoingia madarakani, jambo kubwa lililompa usumbufu, ilikuwa namna ya kuunganisha mikoa mingine ya hapa nchini na Mkoa wa Kigoma. Katika kukabiliana na hali hiyo, Rais Kikwete alisema Serikali ilifanya uamuzi mgumu wa kutenga fedha kwenda katika maeneo mengine muhimu na kuzielekeza fedha hizo kwenye ujenzi wa Barabara Kuu zilizoko nchini.
“Tungefanya hivi tangu Uhuru, huenda sasa hivi tusingekuwa na ujenzi wa barabara, hii ni kazi kubwa ambayo tumeifanya katika uongozi wangu kwa kushirikiana na wenzangu serikalini,” alisema Rais Kikwete na kuwashukuru wakazi wa Kisesa na uongozi wa Wilaya ya Magu kwa kumpokea kwa mapokezi ya hali ya juu.
Alisema Serikali iliamua kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya barabara hizo, kwa kuwa barabara hizo ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Barabara hizi ni kama mishipa iliyo kwenye damu na ndio maana tuliona tuwekeze kwenye miundombinu hiyo ya ujenzi wa barabara, maeneo na mikoa iliyobakia kujengwa barabara ni madogo sana.
“Hivi sasa tunajenga barabara kuunganisha mkoa wa Katavi na Tabora, kwa kujenga barabara kutoka Sikonge kwenda Tabora, Mpanda hadi Uvinza na Kigoma-Tabora-Manyoni na kazi hii ya ujenzi inaendelea,” alisema.
Jana Rais Kikwete jana aliweka jiwe la msingi katika barabara ya Usagara-Kisesa inayojengwa kwa kiwango cha lami, huku akiwataka viongozi wa maeneo hayo kuanza kupima miji hiyo iwe katika mpango.
Sambamba na kuweka jiwe la msingi katika barabara hiyo pia alifungua daraja la watembea kwa miguu la Mabitini, jijini hapa lililojengwa kwa ajili ya kupunguza msongamano pamoja na ajali nyingi zilizokuwa zikitokea katika eneo hilo Alisema viongozi wapopima miji hiyo ya Kisesa na Usagara mapema, watakuwa viongozi mbumbumbu na huo ni ushauri wake kwao wa kuipa hadhi miji hiyo.
“Jiandaeni kupokea mazingira mapya ya kiuchumi, kwa kupima na kuupanga mji vizuri, isipofanyika sasa mtashindwa baadae kwani Kisessa inakua kuliko Magu,” alisema Rais Kikwete.
Alisema maeneo ya Kisesa na Usagara mara baada ya kukamilika kwa barabara hiyo yatakuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na huduma za msingi kama za kusafirisha mizigo zitafanyika hapo kwani malori makubwa hayataruhusiwa kuingia mjini.HABARILEO

0 comments:
Post a Comment