BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

JE UNAMFUNDISHA MTOTO WAKO KUEPUKA UKOROFI ?.


Kwa kawaida mtoto hupitia mambo mengi katika maisha yake ya kila siku. Licha ya kucheza ama kujifunza kwa kuwa mambo yao hujumuisha watu walio katika rika lake, mara nyingi ni jambo la kawaida kukuta wakiishia kukorofishana.


Kukorofishana huku wakati mwingine husababishwa na mabishano ama migogoro midogo midogo inayotokea baina yao.


Mara nyingi sisi kama wazazi huwa tunachukulia suala la ugomvi au ukorofi kwa watoto, kuwa ni tabia ya utoto na tena tunajipa moyo tukisema, ‘’akikua ataacha ‘’


Cha kushangaza ni kwamba mara nyingi tabia kama hizi hukomaa na kuota mizizi, jambo linalosababisha kuharibika kwa taswira ya mtoto husika.


Kama mzazi unatakiwa kufahamu mbinu muhimu zinazoweza kutumika kumfanya mwanao aachane na tabia ya ukorofi na ugomvi na kuwa katika mstari mzuri wa wale wenye maadili mema.


Mfundishe kuwa na uamuzi ya busara
Kwanza kabisa unatakiwa kumfundisha mtoto jinsi ya kuzikabili hasira zake. Pia unatakiwa kumfundisha kuwa si vyema kufanya uamuzi pindi anapokuwa na hasira. Kwani mara nyingi uamuzi huo huwa si sahihi. Pia unaweza kuchangia kumwingiza kwenye matatizo. Ni lazima mtoto wako ajue mbinu bora za kufanya uamuzi. Lakini ili hayo yote yafanye kazi kwa uzuri anapaswa ajifunze kwa vitendo.


Hivyo kama mzazi unawajibika, kuwa kioo kwa mwanao. Fahamu kuwa yeye ataiga kila unachofanya wewe kiwe kizuri au kibaya. Hivyo katika hilo pia umakini mkubwa unahitajika.


Unatakiwa kumwelewesha kwa maneno rahisi tu kwamba akifanya mambo kwa hasira bila kufikiria, matokeo yanaweza kumwandama kwa muda mrefu.


Inawezekana mwenzake amemwibia kalamu. Lakini badala ya kwenda kushtaki kwa mwalimu yeye akaamua kumpiga na kumsukuma. Wakati anamsukuma kwa bahati mbaya mwenzake akaanguka na kuvunjika mkono.


Tayari hapo athari imekuwa kubwa zaidi. Hivyo hakuna haja ya kuumizana wakati kuna suluhisho rahisi la tatizo lake. Kwa kukaa na kutulia angeweza kufanya uamuzi sahihi ya kumfuata mwalim na kumueleza tatizo hilo, pengine suluhu ingepatikana.


Ucha mungu uwe sehemu ya maisha yao
Wazazi wengi huwa tunajisahau katika hili. Kumlea mtoto katika maadili ya kidini kunasaidia sana kumuweka mbali na kufanya maovu. Ikiwa mtoto atajengeka kiimani, ni wazi kuwa atakuwa na busara katika uamuzi wake.


Ikiwa unamlea mtoto katika njia hiyo, atapata kujifunza visa mbalimbali vya kidini vitakavyomjenga kiimani na hatimaye kuwa mtoto bora anayetenda mambo mema kila siku.


Kitendo hicho pia kitachangia kumuweka mbali na migogoro itakayosababisha kugombana na wenzake.


Mtie nguvu pale anapofanya vizuri
Katika makuzi yake mambo mengi yanatokea. Sisi kama wazazi tunapaswa kuwapa yale yaliyo mazuri watoto wetu. Lakini pia wakati mwingine ni vizuri pia kuwapa moyo pale wanapofanya mazuri kwa watoto wenzao hata kwa watu waliowazidi kiumri.


Inawezekana mwanao akawa chanzo cha kuungana kwa marafiki wengine wawili ambao walikuwa mahasimu kipindi cha nyuma ama muda mfupi uliopita. Ikiwa utagundua kitu kama hicho kwa mwanao ni vizuri kumsifia kwani itamjenga kuendelea kufanya jambo hilo mara kwa mara.


Usionyeshe hasira zako kwa mtoto
Wazazi wengi tuna tabia ya kuonyesha hisia zetu pale tunapokuwa tumekwazwa mbele ya watoto. Mara nyingi huwa hatufirikiri mara mbili kuwa hili nalo linaweza kuleta athari hata kwa malezi ya watoto wetu. Kumbuka kwamba mtoto ana kichwa chepesi sana katika kuiga mambo mbalimbali. Hivyo ni vyema kutojionyesha pindi unapokuwa umekasirika kwani utamfanya aone tabia hiyo kuwa ni ya kawaida kwake.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: