BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KUMBE KATIBA MPYA IMEWANUFAISHA WAZANZIBAR.


WASOMI wamepongeza hotuba ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuhusu Katiba Inayopendekezwa kwa wananchi kwa kuichambua vizuri na kubainisha manufaa yake kwa Zanzibar.

Wamesema Katiba hiyo imeipa mamlaka makubwa Zanzibar na imejibu kilio cha muda mrefu cha Wazanzibari.

Katika mahojiano na gazeti hili jana kuhusu hotuba ya Dk Shein juzi, baadhi ya wasomi hao walisema ingawa tangu awali Zanzibar ilikuwa na mamlaka yake, lakini Katiba ‘mpya’ imewaongezea zaidi mamlaka hayo.

Profesa Kitilya Mkumbo wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam alisema kilio cha Wazanzibari wengi, ilikuwa ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kuondolewa kwenye umakamu wa Rais, jambo ambalo Katiba mpya imemrejesha kwenye wadhifa huo.

Katiba mpya inapendekeza kuwepo kwa makamu watatu wa Rais ambao ni mgombea mwenza, Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu.

Profesa Mkumbo pia alisema eneo lingine ambalo Wazanzibari walikuwa wanalidai kwa muda mrefu ni kuruhusiwa kujiunga na jumuiya za kimataifa, zikiwemo za kidini. "Hilo kwenye Katiba mpya wamepewa, kwa hiyo kwa maoni yangu nadhani Wazanzibari madai yao mengi yamezingatiwa," alisema Dk Mkumbo.

Alisema kinachokosekana kwenye katiba hiyo, ambacho ni kilio cha muda mrefu cha Wazanzibari ni serikali ;na alisema waliokosa suala hilo, ndio ambao wanataka katiba hiyo isikubaliwe. Mhadhiri mwingine mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema Zanzibar imepewa mamlaka makubwa mno, ambayo awali haikuwa nayo.

Alitoa mfano ni suala la gesi na mafuta, ambalo kwa sasa sio la Muungano pamoja na kuwa huru kujiunga na jumuiya yoyote ya kimataifa kwa faida ya uchumi wa kisiwa hicho.

"Kama hawajaridhika bado wanaendelea kudai, naamini hao sasa wanataka kuvunja muungano," alisema Dk Bana. Aliongeza kuwa mambo 16 ya muungano yaliyobakishwa, yanatosha kuwafanya Zanzibar watulie, kwani madai yao mengi yamezingatiwa.

Alisisitiza kuwa kinachogomba upande wa Zanzibar ni muundo wa serikali. Alisema hata hivyo Katiba mpya, inatoa fursa ya wananchi kuamua muundo wa muungano wautakao kwa kutumia kura ya maoni. Alisema ni vyema viongozi wa kisiasa, wakatanguliza maslahi ya Zanzibar na sio ya makundi yao ya siasa.

Alimshauri Makamu wa Kwanza wa Rais wa SMZ, Maalim Seif Sharifu Hamad kuisoma Katiba mpya, kwani kuna mambo mazuri mengi yanayoihusu Zanzibar. Pia, msomi huyo alitahadharisha kauli zinazotolewa na viongozi wa juu ya Zanzibar, kuwa zinafifisha Serikali ya kitaifa ya Zanzibar, kwa sababu kauli za viongozi hao zinazidi kuwagawa Wazanzibari.

Alishauri viongozi hao wa juu, wachague maeneo ya kuzungumzia, kwani kauli zao zinaweza kuzorotesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Demokrasia mjini Unguja juzi, Dk Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, aliwataka wananchi kujiandaa kuipigia kura ya ndio Katiba Inayopendekezwa, ambayo maslahi yake ni makubwa kiuchumi na maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema huyo anayewaambia wananchi kwamba Katiba hii haina maslahi na Wazanzibari, yeye kama nani na hana sifa na uwezo wa kuwasemea Wazanzibari wote. Dk Shein alisema Katiba Inayopendekezwa, imetoa fursa kubwa kwa Zanzibar, kufanya mambo yake kwa mapana zaidi ikiwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mujibu wa sheria.

Aidha, alisema zile kero zilizokuwa zikilalamikiwa na wananchi mbalimbali wakiwemo wapinzani, sasa zimepatiwa ufumbuzi wa kudumu. "Wananchi nawaombeni kaisomeni Katiba hii na msikubali ya kuambiwa…Katiba ni safi ambayo imetoa nafasi kubwa kwa wananchi wa Zanzibar kujiimarisha kiuchumi na kupiga hatua kubwa ya maendeleo," alisema.

Kwa mfano, alitaja suala la mafuta na gesi kwamba sasa limeondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano, na kwamba lilikuwa moja ya kilio kikubwa cha wananchi pamoja na wapinzani.

Alisema ni wao waliopitisha azimio katika Baraza la Wawakilishi la kuondoa mafuta na gesi katika orodha ya mambo ya muungano.

Dk Shein alisema suala hilo, lilianzia wakati yeye akiwa Makamu wa Rais na alipokuja kuwa Rais wa Zanzibar, alilikuta na kukubaliana nalo, kwa sababu yapo maslahi makubwa kwa wananchi wote.

Alisema amesikitishwa na msaidizi wake, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif, ambaye amekuwa akisisitiza siku zote kutungwa kwa sera za kuchimba mafuta, lakini Katiba Inayopendekezwa yeye haikubali na ameapa kuipinga kwa nguvu zote.

Alimtaka Maalim Seif kuacha kuwashawishi wananchi wa Zanzibar, kuikataa Katiba Inayopendekezwa kwa sababu yeye sio msemaji wa wananchi wa Zanzibar.

Alisema hawezi kuwasemea wanachi wa Unguja na Pemba katika suala la Katiba, kwa sababu wananchi wamejionea wenyewe maslahi yaliyomo katika Katiba mpya Inayopendekezwa.

“Msemaji wa wananchi wa Zanzibar wote ni mimi na sio yeye…nawataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ya kuipitisha Katiba mpya Inayopendekezwa,” alisema.

Aidha, alisisitiza kuwa Katiba Inayopendekezwa imezingatia na kuuenzi Muungano wa Tanganyika wa Zanzibar na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, ambayo yameasisiwa na viongozi wakuu wa nchi mbili hizo, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amaan Karume.

"Nataka kuwaambia wananchi kwamba hivi sasa hakuna tena kero za Muungano, zote zimepatiwa ufumbuzi na kama wale wanaosema koti lilikuwa linabana, basi sasa limevuliwa," alisema.

Alisema viongozi wa kambi ya upinzani, waliokuwa wakilalamika muda mrefu kwamba Tanganyika imevaa koti la Muungano, sasa watambue kuwa katika Katiba Inayopendekezwa, koti hilo limepunguzwa.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: