BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SHIMIWI 20I4 KUHITIMISHWA KWA FAINALI YA NGUVU KATIKA MCHEZO WA SOKA KATI YA ELIMU SPORT CLUB DHIDI YA UCHUKUZI SPORT CLUB UWANJA WA JAMHURI MORO OKTOBA 11.

Wachezaji wa timu ya soka ya Elimu Sport Club wakiwa wamemnyanyua kocha wao mkuu, Max Marthew baada ya ushindi wa kishindo wa bao 6-0 dhidi ya Mahakama walioupata katika mchezo wa nusu fainali katika michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2014 uliofanyika uwanja wa jamhuri Morogoro.Picha/Mtanda Blog.

 
Na Mtanda Blog, Morogoro.
Michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2014 yanafikia tamati leo baada ya jana kuhitimishwa kwa michezo ya nusu fainali, huku michezo mitatu ya soka, netiboli na kamba italazimika kucheza fainali katika kilele cha kufunga michezo hiyo ili kupata mabingwa kufuatia michezo mingine kupata washindi wake wa kwanza hadi wa tatu mkoani Morogoro.


Katika mchezo wa soka, mabingwa watetezi timu ya Elimu Sport Club imetinga fainali kwa kufanya kufuzu kufuatia kuiadhibu bila huruma timu ya Mahakama Sport Club bao 6-0 katika mchezo wa nusu fainali uliofanyika uwanja wa jamhuri huku Habari Sport Club yenyewe ikiishia hatua hiyo ya nusu fainali baada ya kukubali kutandikwa bao 3-0 na Uchukuzi Sport Club uwanja wa Mazimbu.

Mabingwa hao watetezi walianza kuhesabu bao la kwanza dakika ya 25 likifungwa na Omari Juma kufuatia kazi nzuri ya Richard Mwakalinga huku bao la pili likipachikwa na Masoud Simba dakika ya 34 baada ya ushirikiano wa Josia Mwakatalima.

Mahakama Sport Club ilishindwa kuhimili kasi ya mchezo huo kutoka kwa Elimu na kujikuta waking’utwa mabao mengine yaliyokwamishwa wavuni na mshambuliaji Richard Mwakalinga aliyefunga bao mbili dakika ya 36 na 74 kwa pasi za Mussa Lusewa lakini Azizi Gunda na Mussa Lusewa walihitimisha kalamu ya mabao katika dakika za 64 na 85.

Timu ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt Fenella Mukangara, Habari Sport Club, mbio zake zilihitimishwa katika nusu fainali na Uchukuzi Sport Club iliyoshinda bao 3-0 ambapo mabao ya Abubakari Mwamachi aliyefunga dakika ya 36 na Yahaya Bernard kupachika la tatu katika dakika ya 67 huku Habari ikitoa zawadi kwa kuizawadia Uchukuzi bao la kwanza baada ya kujifunga dakika ya 23.


Katika mchezo wa fainali upande wa soka, mabingwa watetezi timu ya Elimu itatetea kwa kuchuana na Uchukuzi Sport Club wakati netiboli Utumishi ikicheza fainali na Uchukuzi katika michezo itayochezwa uwanja wa jamhuri.

Mabingwa watetezi katika mchezo wa netiboli timu ya watoto wa Rais Jakaya Kikwete (Ikulu Netiboli Sport Club) ilivuliwa ubingwa na vijana shupavu wa Waziri wa Uchukuzi, Dk HarrisonMwakyembe kwa kutolewa nishai baada ya kufungwa magoli 21-20 katika mchezo wa nusu fainali huku Afya ikifyata mkia kwa Uchukuzi kwa magoli 51-40.


Safu ya ufungaji ya Utumishi ikiwa chini ya Anna Msulwa na Hadija Msafiri ililazimika kuivimbia kichwa Ikulu na kugangamala na kusambaratisha kwa ushindi kiduchu wa magoli 21-20 huku Ikulu ikiwa na wafungaji Monica Kessy na Mwadawa Twalibu wakizidiwa ujanja na wenzao kabla ya kupulizwa kipenga cha waamuzi kumaliza mchezo na kujikuta wakivuliwa ubingwa katika hatua ya nusu fainali.


Wakati Ikulu wakiishia hatua hiyo ya nusu fainali, Uchukuzi nayo ilifanya kazi ya ziada ya kuwaondoa Afya kama si kazi mzuri ya wafungaji ya Tatu Kitula na Fatuma Msafiri waliofunga magoli 51 dhidi ya magoli machache yaliyofungwa na Juet Jabu na Rukia Yusup na kupoteza mchezo huo.


Wakati katika mchezo wa kamba wanaume Ikulu ilifanikiwa kuingia fainali ambapo itawania ubingwa huo dhidy ya Mahakama na mabingwa wanawake watetezi Ras Iringa ikitinga fainali huku ikisubiri mshindi kati ya Ikulu na Ras Lindi wataochuana katika nusu fainali ili kupata mshindi wa kutinga fainali.


Katika mchezo wa kiporo wa jadi, Makamu wa Rais wanaume walitawazwa mabingwa katika mchezo wa bao huku Kilimo ikishika nafasi ya pili na Tamisemi iliambulia nafasi ya tatu na katika upande wa wanawake NFRA ilijifariji kwa kutwaa ubingwa huo, wakati Tume ya Sheria ilishika nasi ya pili na Mambo ya Ndani ikitwaa ya tatu.


SHIMIWI 2014 YAFIKIA NUSU MORO.Oktoba 09/ 2014.

Mshambuliaji wa Waziri Mkuu Sport Club, Kalolo Ramadhan wakiwatoka wachezaji wa Habari Sport Club wakati wa mchezo wa robo fainali katika michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2014 uwanja wa jamhuri mkoani Morogoro. Habari iliishindaa bao 1-0.Picha/Mtanda Blog.


Mabingwa watetezi wa soka wa mwaka 2013 timu ya Elimu Sport Club, imeendelea kupeta na kutinga nusu fainali kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 5-3 baada ya kufanya vizuri katika mchezo wake wa robo dhidi ya Afya katika michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2014 uwanja wa jamhuri mkoani Morogoro.

Timu ya Afya Sport Club iliwabana wapinzani wao ndani ya dakika 90 na kujikuta wakiwalazimisha na kumaliza mchezo huo kwa sare ya bao 3-3 lakini bahati ilikuwa upande wao Elimu ambao walifanikiwa kupata penalti 4-3 na kufanya mchezo huo kumalizika kwa idadi ya bao 7-6.

Mahakama Sport Club nayo iliingia katika hatua hiyo ya nusu fainali baada ya kuilaza Uhamiaji bao 1-0 katika mchezo war obo fainali michezo iliyofanyika uwanja wa Mazimbu.

Katika uwanja wa jamhuri timu ya Habari Sport Club ilibahatika kutinga nusu fainali kufuatia ushindi wao wa bao 1-0 mbele ya Waziri Mkuu bao lililofungwa na mshambuliaji Ahmed Salum dakika 25 huku Uchukuzi Sport Club yenyewe iliwaondoa Kilimo Sport Club kwa mikwaju ya penalti 5-3 baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90.


Mshambuliaji wa Kilimo, Athman Tenga ndiye aliyeanza kuipatia bao timu yake ya kuongoza dakika ya 17 wakati Hassan Lubava wa Uchukuzi aliisawazishia dakika ya 57 na kumaliza mchezo huo kwa sare hiyo.


Upande wa netiboli Ikulu iliendeleza ubabe katika michuano hiyo baada ya kuilaza Bunge magoli 67-24 huku Afya ikiizamisha Maendeleo ya Jamii kwa magoli 36-20.


Tamisemi ilidondokea pua kwa kukubali kipigo cha magoli 58-20 kutoka kwa Uchukuzi wakati Utumishi ikiiadhibu Hazina magoli 73-21.

Katika mchezo huo uliingiwa na dosari baada ya wachezaji wa Hazina kugomea mchezo kwa kusimama ndani ya uwanja kwa madai ya waamuzi waliokuwa wakichezesha mchezo huo kutoa upendeleo dhidi ya wapinzani wao hali iliyowafanya kugomea.

Meneja wa timu ya netiboli ya Hazina, Rehema Kapela alieleza kuwa wachezaji wake waligomea mchezo kutokana na waamuzi kutoa upendeleo kwa kupuliza kipenga pindi wachezaji wake wakishika mpira huku makosa hay ohayo yakifumbiwa macho.


Lakini Mwenyekiti waa Kamati ya Ufundi michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2014, Joyce Benjamin alieleza kuwa timu hizo zimekuwa na upinzani wa hali ya juu na wanapokutana wamekuwa wakicheza kwa jazba jambo linalosababisha kutokea lawazi zisizo la kweli.


Benjamin alieleza kuwa Hazina na Utumishi wamekuwa na upinzani mkali na siku ya siku michezo yao humalizika kwa manung’uniko kibao.

Naye Mjumbe wa kamati ya utendaji Shimiwi Taifa, Grace Mwakifuna alisema kuwa leo (jana) watacheza mchezo mmoja wa jadi wa bao ili kupata bingwa wake ikihusisha wanaume na wanawake.

“Michezo inafikia ukingoni, leo (jana) tunacheza mchezo wa jadi (bao) na kesho (leo) michezo ya nusu fainali katika michezo ya soka, netiboli, kamba itafanyika ili kupata timu za kucheza fainali mwaka 2014 ambapo michezo yote itafanyika kwenye uwanja wa jamhuri.”alisema Mwakifuna.


ROBO FAINALI SOKA, NETIBOLI YAPIGWA KUSAKA TIMU NNE ZA KUTINGA NUSU FAINALI SHIMIWILI, Oktoba 8/ 2014.

  
Bingwa wa mchezo wa draft wanawake 2014, Ras Morogoro, Leokadia Mwang'ombe kushoto akichuana na mshindi wa pili, Sophia Mpema kutoka wizara ya Mambo ya Ndani wakati wa mchezo wa fainali uwanja wa jamhuri Morogoro, Ras Morogoro ilishinda bao 2-0.Picha/Mtanda Blog
Wakati michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2014 ikifikia hatua ya robo fainali kwa upande wa soka na kamba, kwa upande wa michezo ya jadi tayari imepata mabingwa wake mkoani Morogoro.

Akizungumza na gazeti hili Mjumbe wa kamati ya utendaji Shimiwi Taifa, Grace Mwakifuna alisema kwa upande wa michezo ya jadi tayari imepata mabingwa wakati katika michezo ya soka na kamba ikifikia hatua ya robo fainali.


Mwakifuna alisema michezo ya soka itaanza kuchezwa leo saa 8 mchana (jana) katika viwaanja viwili vya jamhuri na Mazimbu kwa timu nane kushuka dimbani kuwania kufuzu kucheza nusu fainali.

Alitaja michezo hiyo kuwa ni Kilimo itachuana na Uchukuzi saa 8 mchana wakati saa 10 jioni Habari itajipima kuona kama itavuka kikwazo na kutinga nusu fainali itakapocheza na Waziri Mkuu ambapo michezo hiyo itafanyika uwanja wa jamhuri.


Katika uwanja wa Mazimbu Elimu itacheza na Afya saa 8 huku saa 10 jioni Mahakama ikijitupa kucheza na Uhamiaji.alisema Mwakifuna.


Mwakifuna aliendelea kutoa ufafanuzi kwa kufafanua ratiba ya michezo netiboli ambapo timu nane zitacheza robo fainali ni pamoja na Uchukuzi, Mifugo,Utumishi na Hazina Maendeleo, Afya, Bunge, Ikulu ambazo zilichuana jana mchana kuanzia saa 8 ili kupata timu nne za kucheza nusu fainali katika michezo iliyochezwa uwanja wa jamhuri.


Kamba yenyewe imefikia hatua ya nusu fainali baada ya wizara nne kutinga hatua hiyi ikiwemo Ikulu, Uchukuzi, Tamisemi na Mahakama huku wanawake ni Ras Iringa, Ujenzi, Ikulu na Tamisemi.


Kwa upande wa michezo ya jadi ambayo tayari imepata mabingwa wake ni pamoja na mchezo wa karata wanaume ambapo Paul Masibula kutoka Mipango aliibuka bingwa huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Joh John wa Ras Kagera wakati nafasi ya tatu Frank Kimwaga wa Mifugo na upande wa wanawake Rehema Kazimoto aliing’arisha Bunge kwa kushika nafasi ya kwanza, nafasi ya pili ilitwaliwa na Elizaberth Kasimila wa Ikulu na tatu Dalila Yassin aliambulia nafasi hiyo.


Katika mbio za baiskeli, Prisca Kahimba aliibuka bingwa katika mbio za kilometa 32 akitokea Hazina wakati Ras Pwani, Agatha Gamba aliiongoza na kushika nafasi ya pili na Johari Moshi wa Uchukuzi akishika nafasi ya tatu.


Hassan Ligoneko kutoka Utumishi alitamba katika mbio hizo za kilometa 32 kwa kushika nafasi ya kwanza, Ezekel Muhina wa Ras Tanga akishika nafasi ya pili na John Fataki akishika nafasi ya tatu.



Katika mchezo wa draft Salum Simba yeye aliibuka bingwa kwa kushika nafasi ya kwanza huku Dk Idris Lukindo alishika nafasi ya pili na Ramadhan Stephano wa Habri aliambulia nafasi ya tatu.


Wakati upande wa wanawake wenyeji wa michezo hiyo, Leokadia Mwang’ombe aliwatoa kimasomaso Ras Morogoro kwa kutwaa ubingwa wa huo wa draft, nafasi ya pili ikienda kwa Sophia Mpema wa Mambo ya Ndani na bingwa mtetezi kutoka Ras Mwanza Badaka Kabaka akiambulia kuishia nafasi ya tatu.


Katika dats wizara ya Uchukuzi ilishika nafasi ya kwanza, Elimu ikishika nafasi ya pili na Mambo ya Ndani ikaishia nafasi ya tatu.

Grace Mwakifuna ambaye pia ni mkusanya matokeo ya michezo ya Shimiwi 2014 alielezakuwa michezo hiyo itafikia tamati Oktoba 11 mwaka huu kwa michezo ya fainali ikihusisha michezo ya soka, netiboli na Kamba.


NNE ZA SOKA ZATINGA ROBO FAINALI KWA MBINDE MICHEZO YA SHIMIWI 2014 MORO. Oktoba 7/ 2014.

Timu nne za soka kati ya nane zimetinga hatua ya robo fainali kwa mbinde baada ya kushinda michezo yao kwa njia ya mikwaju ya penalti kufuatia kumalizika kwa michezo ya hatu ya 16 bora mtoano iliyohusisha timu 32 katika michezo inayoendelea yaShirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2014 mkoani Morogoro.


Mahakama sport club ndiyo iliyoanza kufuzu kwa kuingia hatua ya robo fainali kufuatia ushindi wake wa bao 4-3 walioupata kwa njia ya penalti kwa kuiondoa Ras Arusha wakimaliza dakika 90 kwa kutoshana nguvu ya sare ya bao 1-1 huku Mambo ya Ndani ikijikuta ikiaga michezo hiyo kwa kutolewa na Kilimo kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-2 baada ya dakika 90 kutoa sare tasa 0-0.


Nyingine zilizotinga hatua ya robo fainali kwa njia ya matuta ni pamoja na Habari sport club iliyopata ushindi wa penalti 3-1 mbele ya Maji baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 wakati Uhamiaji Sport Club nayo ililazimika kuingia hatua hiyo ya robo fainali kwa ikiitambia Ras Manyara kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya bao 1-1.


Timu ambazo zilipata ushindi ndani ya dakika 90 na kutinga robo fainali ni Elimu Sport Club ilifuzu kwa kuitandika Mambo ya Nje kwa bao 2-0 wakati Waziri Mkuu ilijihakikishia kupata bao 1-0 kwa kuifunga Maliasili.


Ras Mbeya ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa timu ya Afya Sport Club na Uchukuzi iliisambaratisha NFRA kwa kuikung’uta bao 1-0.


Kwa upande wa netiboli katika hatua ya 16 bora mtoano Uchukuzi iliilaza Ras Tanga kwa magoli 54-11 wakati Tamisemi ikiibwaga Mifugo kwa magoli 41-10 huku Utumishi ilitamba mbele ya Mahakama kwa kuisambaratisha magoli 56-14 na Hazina ikamaliza kazi kwa kuifunga Ras Njombe 26-23 ambazo zimetinga hatua ya robo fainali.


Maendeleo ya Jamii ilijisogeza robo fainali kwa pinde ikipata ushindi wa magoli 23-22 dhidi ya Ardhi huku Afya ikiwaondoa Mambo ya Ndani kwa magoli 30-17 huku Bunge ilitamba kwa kuifunga Maliasili magoli 33-25 na Ikulu ikiibwaga Ulinzi kwa magoli 52-10.


Mchezo wa kamba katika hatua hiyo ya 16 bora mtoano wanaume Ikulu ilishinda 2-0 kwa kuifunga Mifugo, Habari ikapoteza mbele ya NFRA 1-0, Afya ikatamba kwa Ardhi 2-0, Uchukuzi ikaiondoa Uhamiaji 1-0, Maliasili ikiitambia Makamu wa Rais 2-0, Kilimo ikaondolewa na Hazina 2-0, Mambo ya Ndani ikapata ushindi kwa Ujenzi 1-0 na Waziri Mkuu ikiiga mashindano kwa 2-1.


Kwa upande wa wanawake Waziri mkuu ilizidiwa maarifaa na Rad Iringa kwa kufungwa 1-0, Ikilu ikipata ushindi 2-0 mbele ya Mifugo, Mambo ya Ndani 2-0 Afya, Tamisemi 1-0 Hazina, Mahakama 2-0 Mambo ya Nje, Uchukuzi 2-0 Tume ya Sheria na Ujenzi ikatamba kwa Ras Lindi kwa kupata ushindi 2-0.CHANZO:MTANDA BLOG
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: