BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

VIONGOZI WA KISIASA WAMESHINDWA KUMUENZI MWALIMU JULIUS NYERERE KUTOKANA NA KUJIHUSISHA NA RUSHWA, UFISADI NA KUPOROMOKA KWA MAADILI YA UONGOZI.


Nukuu Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mstari wa mbele kukemea vitendo viovu. Lakini pia alijitahidi kujenga jamii isiyokuwa na ubaguzi wa rangi wala dini. Miaka 15 baada ya kifo chake, vitendo viovu vimezidi kushamiri.


Zanzibar.
Baadhi ya wanasiasa na wananchi mjini Zanzibar, wamesema viongozi wengi wameshindwa kufuata kwa vitendo yale aliyofanya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa uhai wake.


Badala yake, tangu kufariki dunia kwake miaka 15 iliyopita, nchi imeshuhudia kuongezeka kwa vitendo vya rushwa, ufisadi na kuporomoka kwa maadili ya uongozi nchini.


Walisema hayo walipokuwa wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 15 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na kuitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kupambana na vitendo hivyo.


Katibu Mkuu wa Tadea, Juma Ali Khatib alisema mambo yote yaliyokuwa yakipigwa vita na Mwalimu Nyerere, sasa yamekuwa yakifanywa na baadhi ya watendaji na viongozi wa Serikali ikiwamo kujihusisha na rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka bila ya kuchukuliwa hatua kutokana na kuanguka kwa maadili ya uongozi.


“Hata viongozi wanaotajwa kuwa na nia ya kuwania urais mwakani, hakuna hata mmoja anayefanana na Mwalimu Nyerere kwa uadilifu na uwajibikaji, tunahitaji kiongozi kama huyo,” alisema Khatib.


Upande wake, Katibu wa Vijana Mkoa wa Mjini Magharibi (Bavicha), Francis Gebwa Warema alisema Mwalimu Nyerere amekuwa akienziwa kwa maneno na siyo vitendo, ndiyo maana vita dhidi ya rushwa na ufisadi imekuwa ngumu.


Alisema Serikali ya CCM imeshindwa kusimamia misingi ya utawala bora ikiwamo sheria zinazopiga vita rushwa na uhujumu uchumi baada ya viongozi kuamua kuliua Azimio la Arusha wakati ndiyo ulikuwa msingi wa utawala bora.


Naye aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Simai Mohamed Said alisema Serikali zote mbili zinamuenzi Mwalimu Nyerere, lakini zinahitaji kuongeza nguvu katika kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi ili kuharakisha maendeleo ya wananchi na Taifa.


Naye Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani Abdallah alisema: “Inasikitisha mambo aliyokuwa akiyapinga Mwalimu Nyerere kama ubaguzi na ukabila, sasa yanafanyika ndani ya vyombo vya kutunga sheria.”


“Misingi ya utawala bora imeshindwa kusimama kutokana na kuanguka kwa maadili ya uongozi... viongozi wetu wameshindwa kufuata nyayo zake tangu kufa kwa Azimio la Arusha,” alisema Bimani.


Mjini Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo amewataka Watanzania kumuenzi kwa vitendo hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere ili kurithisha kwa vijana uadilifu wake.


Akizungumza katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere yaliyokwenda sambamba na kutolewa zawadi kwa wanafunzi wa shule za msingi, Magesa alisema ni muhimu Watanzania kumuenzi Nyerere kutokana na mchango mkubwa alioutoa.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: