
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu.
HATIMAYE ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Namtumbo hadi Tunduru yenye urefu wa kilometa 187.6, umeanza katika baadhi ya vipande vya barabara hiyo na kuleta matumaini mapya kwa wakazi wa mikoa ya Ruvuma na Mtwara.
Hayo yalibainika baada ya ziara ya hivi karibuni ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu, kutembelea wakandarasi wanaojenga barabara hiyo, ikiwa ni juhudi za Serikali kutoa msukumo kwa wakandarasi hao na kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakamilika kwa wakati.
Mwambungu alisema kuwa Serikali imelazimika kuweka wakandarasi watatu tofauti kwa ajili ya kutengeneza barabara hiyo, baada ya mkandarasi wa mwanzo kutoka Kampuni ya Progressive, kushindwa kufanya kazi hiyo na kufukuzwa.
Alisema pamoja na kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo za utendaji kwa wakandarasi hao, ujenzi wa barabara hiyo ameonesha kuridhishwa na maendeleo makubwa ya ujenzi huo na Serikali itaendelea kusimamia kuhakikisha kazi hiyo inakamilika ndani ya muda kulingana na mkataba.
Kwa mujibu wa Mwambungu, wakandarasi wanaojenga barabara hiyo wameendelea kutoa matumaini makubwa kwa wananchi kwamba pamoja na kukaribia msimu wa mvua, watahakikisha barabara hiyo inapitika wakati wote na wapo tayari kutoa msaada endapo itatokea magari kukwama.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 187.6, inajengwa na kampuni tatu ikiwemo ya China Railway Group, iliyosaini mkataka wa kujenga kilometa 60.7, Sichuan Road and Bridge Group kilometa 68.2 pamoja na China Civil Engineering Construction iliyopewa kilometa 58.7.
Awali wakitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Mhandisi wa Kampuni ya SGI Dante Tandia na Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya China Civil Engineering, Faraji Mustafa pamoja na mambo mengine, walimthibitishia Mkuu wa Mkoa huyo kwamba barbara hiyo itakwisha kulingana na maelekezo ya mkataba.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema ujenzi wa barabara hiyo kutoka Namtumbo hadi Tunduru kwa kiwango cha Lami, unaleta nuru mpya kwa wananchi na watumiaji wa barabara hiyo, ambayo kwa miaka mingi imekuwa kero kubwa na wakati mwingine kutopitika kabisa kutokana na kuharibika vibaya na mvua za masika.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment