AKAUNTI YA TEGETA ESCROW YAMFANYA WAZIRI WA NISHATI NA MADINI PROF MUHONGO AZOMEWA BUNGENI MBELE YA WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amekumbana na wakati mgumu, ikiwa ni pamoja na kuzomewa na wabunge na kukatizwa wakati akitoa maelezo kufuatia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kupendekeza yeye pamoja na viongozi wengine waandamizi wa serikali, akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wawajibishwe.
Mbali na kukumbana na wakati mgumu kabla na wakati akitoa maelezo hayo yaliyoonekana kuwa ni kujitetea, Profesa Muhongo hakujadili ripoti za uchunguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na ya Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) zilizotumiwa na PAC kama rejea ya mapendekezo yake.
Badala yake, maelezo yake, ambayo yalikuwa magumu, hasa kwa wananchi wa kawaida kuyaelewa, yalijikita zaidi katika kuishambulia taarifa ya PAC, ambayo ilizua gumzo kubwa kwa wananchi wa kada zote.
PAC ilitoa pendekezo hilo baada ya kubaini kuwa Profesa Muhongo pamoja na viongozi hao walihusika katika sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Pia imependekeza kwamba, viongozi wa umma waliopata mgawo wa fedha hizo, wafilisiwe na kuvuliwa nyadhifa zote mara moja.
Wengine, ambao PAC imependekeza wawajibishwe na kuchukuliwa hatua, ikiwamo kufikishwa mahakamani, ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema; Katibu Mkuu Wizara wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Stephen Maselle.
Profesa Muhongo alikumbana na wakati mgumu kabla na wakati akitoa maelezo hayo bungeni kuhusu taarifa ya ukaguzi maalumu kuhusiana na miamala, iliyofanyika katika akaunti hiyo pamoja na umiliki wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Limited (IPTL).
Ukaguzi huo ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).Kabla hajaanza kutoa maelezo hayo, Profesa Muhongo alianza kukumbana na hali hiyo, baada ya Mbunge wa Mgogoni (CUF), Kombo Khamis Kombo,kuomba mwongozo wa spika chini ya kanuni ya Bunge namba 68 (7).
Katika mwongozo wake, Kombo alisema matukio mengi, likiwamo lililohusu sakata la kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond na Operesheni Tokomeza, yalitokea nchini.
Lakini akasema serikali haikwenda bungeni na utetezi wa kumtetea Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa wala Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Khamis Kagasheki, kutokana na matukio hayo.
Kutokana na hilo, alisema anashangaa kuona leo serikali ikipewa nafasi bungeni ya kupeleka utetezi kutokana na sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, ambalo limewagusa baadhi ya viongozi.
”Hii mheshimiwa spika, ni kuonyesha kwamba, kuna double standard (undumilakuwili) katika uongozi, kuna baadhi ya viongozi wanatetewa na baadhi ya viongozi hawana haki ya kutetewa,” alisema Kombo.
Hivyo, aliomba Spika atoe majibu sababu ya waliobainika kuhusika na kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow wasijitetee wenyewe, badala yake watetewe na serikali.Baada ya kuhoji hilo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisimama na kuhoji sababu za Kombo kutaka kutomtendea isivyo haki akisema kwamba,alichokisema hakijui.
Spika Makinda alisema uamuzi wa kumpa nafasi Waziri Muhongo kutoa maelezo ni utaratibu wa kikanuni, baada ya PAC kuwasilisha taarifa yake jana.Kauli hiyo ya Spika Makinda iliibua zogo kubwa bungeni kutoka kwa wabunge lililoashiria kumpinga, hali ambayo ilimfanya ahamaki na kuanza kuwakemea wabunge, huku akitaja majina ya baadhi yao.
”Jamani msinanii, ee Silinde (David-Mbunge wa Mbozi Magharibi-Chadema) sipendi kuwataja majina kwa sababu mna tabia isiyokuwa sahihi,” alisema Spika Makinda, huku akionyesha kuwa amehamaki.
Alisema juzi aliruhusu taarifa yote ya PAC ikasomwa bungeni na kwa hiyo jana akaruhusu upande wa pili wa serikali nao kufanya hivyo kwa kuwa huo ndiyo utaratibu.
Hata hivyo, ufafanuzi huo wa Spika Makinda haukufua dafu, kwani wabunge walianza kuzomea kuonyesha hawakubaliani naye.Hali hiyo iliongeza hamaki kwa Spika Makinda, ambaye aliendelea kuwakemea wabunge safari hii kwa kutumia maneno makali."Unajua mimi kubishana na watu ambao wanajua kanuni lakini hawapendi sipendi kabisa, kwa sababu nakwambia hii hoja ya wabunge serikali inajibu, haimtetei mtu, inajibu.
”Tabia zenu siyo nzuri na zina tabia ya upendeleo,” alisema Spika Makinda, huku wabunge wakiendelea kupiga kelele za kupingana naye.
Baadaye, Spika Makinda alimruhusu Waziri Muhongo kutoa maelezo yake na wakati akiendelea kueleza, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisimama kwa lengo la kutoa taarifa, lakini Spika hakumruhusu kufanya hivyo.
Wakati Mnyika akiwa amesimama, wabunge wengine walikuwa wakipaza sauti kulalamika kuwa yaliyokuwa yakielezwa na Waziri Muhongo kwanza walikuwa hawajapewa nakala ya hayo maelezo wala viambatanisho.
Mara kwa mara, Waziri Muhongo alikuwa akitoa maelezo yake, huku akiahidi kwamba, atawapa wabunge vielelezo.Hata hivyo, hadi anahitimisha maelezo yake, hakuna mbunge aliyekuwa amepewa vielelezo hivyo isipokuwa nakala za vitabu vya maelezo yake.
Pia sehemu kubwa ya maelezo yake ilikuwa ikipingwa na wabunge kadri alivyokuwa akieleza na wakati mwingine alijikuta ama akipingwa au akizomewa na wabunge bungeni, kiasi cha kumfanya Spika Makinda kuingilia kati na kuwakemea wabunge.
Kwa mfano, wabunge walipaza sauti wakisema kuwa ni mwongo na kumzomea pale aliposema kuwa yeye siyo dalali wa IPTL na kwamba, yeye ni dalili wa kupeleka umeme vijijini, kuhakikishia Watanzania wanaunganishiwa umeme kwa Sh. 27,000 na kushusha bei ya umeme.
Hali hiyo ilimfanya Spika Makinda kuingilia kati na kusema: “Ukitumia maneno yako bila ruhusa huna maana.”Hali ya kupingwa, kuzomewa na maelezo yake kukatizwa na wabunge, ilijitokeza pia Waziri Muhongo alipotoa maneno ya kuhitimisha maelezo yake, aliyoyatoa kwa lugha ya Kiingereza.
Maneno hayo, ambayo hakuweza kuyatafsiri kwa Kiswahili, kwani kila alipokuwa akijaribu kufanya hivyo, alikatizwa na wabunge, ambao walipaza sauti za kumpinga, huku wakiinua juu nakala za vijitabu vyenye maelezo yake.
Wabunge walifanya hivyo wakisema kwamba, maneno hayakuwa yameandikwa kwenye maelezo, bali aliyatamka kwa kuyatoa kichwani mithili ya mwalimu anayewafundisha wanafunzi darasani.
Mbali na kutozungumzia ripoti ya CAG, Takukuru na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilizowasilishwa na PAC zikithibitisha kuwa fedha zilizochotwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow zilikuwa ni za umma, maelezo ya Waziri Muhongo hayakueleza namna fedha hizo zilivyotoka,waliolipwa wanavyohusika na uhalali wa kampuni ya Pan African Power (PAP) iliyolipwa.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment