HUKUMU YA UCHOTAJI FEDHA MABILIONI YA AKAUNTI YA ESCROR, VIGOGO TUMBO JOTO LEO BUNGENI
Dodoma/Dar. Pamoja na maneno mengi yaliyosemwa, shutuma lukuki zilizotolewa na mbinu za kila aina kutaka kuzuia mjadala wa ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya IPTL, leo ndiyo siku yake ya hukumu.
Katika hukumu hiyo, ukweli utadhihirika kuhusu nani mkweli na nani mwongo wakati Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), itakapowasilisha bungeni maoni yake kuhusu ripoti ya kuchotwa kwa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Uchunguzi huo ulifanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa maelekezo ya Serikali baada ya kuombwa na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila alipolalamikia ufisadi huo bungeni.
Pamoja na juhudi za kampuni ya IPTL na PAP kufungua kesi kuzua mjadala huo bungeni, hukumu iliyotolewa jana na majaji watatu ilisema kila kitu kiendelee kama kilivyo na kitakachoendelea kisiathiri kesi iliyopo mahakamani.
Uamuzi huo ulipokewa kwa hisia tofauti, upande wa IPTL ukishangilia kwa kupewa ulinzi, huku baadhi ya watu wakieleza kuwa Mahakama imezuia mjadala huo unaosubiriwa kwa hamu.
Muda mfupi baada ya hukumu hiyo kutolewa na kusambaa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe ambaye pia alikuwa mdaiwa, aliandika katika ukurasa wake wa Twitter, “Mahakama imetoa zuio la kujadili taarifa ya CAG kuhusu Escrow. Hata hivyo, PAC itawasilisha taarifa yake kwa mujibu wa ratiba ya Bunge hapo kesho.”
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema: “Sisi hatuna taarifa hizo kutoka mahakamani, ratiba ya Bunge inaendelea kama kawaida.”
Habari zaidi kutoka ofisi za Bunge jana, zilisema kuwa Ofisi ya Sheria ya Bunge nayo imeshauri kuwa suala hilo linaweza kujadiliwa bila wasiwasi wowote.
Mapema jana katika kikao cha asubuhi, Spika Anne Makinda alilithibitishia Bunge kwamba ripoti ya escrow itajadiliwa na hakuna wa kuwazuia.
Kauli hiyo ilitokana na mwongozo wa Mbunge wa Bariadi (UDP), John Cheyo aliyetaka kujua kama Bunge linatambua kuwapo kesi iliyofunguliwa mahakamani kuzuia mjadala wa ripoti hiyo.
Akijibu mwongozo huo, Makinda alisema: “Nyie waheshimiwa wabunge msianze kuishi kwa wasiwasi, sisi kinga zetu zipo wazi, hakuna mtu anayeweza kutushtaki sisi tusifanye kazi yetu, hayupo atakayezuia sisi kufanya kazi za kibunge na kazi ambazo zinapatikana kutokana na maeneo mnayopita.”
Muda mfupi kabla ya kuahirishwa kwa Bunge jana usiku, Kaimu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisimama kuomba mwongozo juu ya hatua hiyo ya Mahakama lakini Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alimkatisha akisema kiti cha Bunge hakijapata taarifa zozote na kwamba msimamo uliotolewa mapema na Spika Makinda ndiyo unaofuatwa.
IPTL
Mwanasheria wa IPTL, Joseph Mwakandege alisema uamuzi uliotolea na Mahakama ni wa haki, kwa kuwa umesema kila kitu kibaki kilivyo na hivyo mjadala usifanyike.
Mwakandege alisema kwa hali ilivyo, huwezi kujadili suala la escrow wakati linahusiana moja kwa moja na kesi 14 zilizoko mahakamani.
“Ukitazama hadidu za rejea walizopewa zote ni issues zilizopo mahakamani. Huwezi kujadili suala hili bila sisi kuwapo, maana na sisi tuna haki ya kusikilizwa,” alisema Mwakandege.
Hali bungeni
Sakata la uchotaji wa fedha hizo limekuwa gumzo katika mkutano wa Bunge unaoendelea kutokana na kuhusishwa viongozi wa juu katika ngazi mbalimbali serikalini.
Wabunge wa pande zote, chama tawala na upinzani, wameungana kuhakikisha suala hilo linajadiliwa kwa uwazi, licha ya upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya vigogo wa Serikali.
Tangu ripoti ya uchunguzi wa CAG ikabidhiwe kwa PAC inayoongozwa na Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini-Chadema), taarifa mbalimbali zimekuwa zikitolewa ikielezwa kuwa fedha hizo zilizochotwa zilipaswa kwenda Tanesco.
Taarifa zinaeleza kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Sh306 bilioni wakati madai ya Tanesco kwa IPTL yalikuwa Sh321 bilioni, hivyo fedha zote za escrow zilipaswa kwenda Tanesco na bado ingekuwa inadai.
Wabunge mbalimbali wamekuwa wakijitahidi kutaka Spika aruhusu mjadala wa ripoti hiyo uanze mapema lakini kutokana na shughuli nyingine za Bunge, ilibidi ratiba ifuatwe hadi leo.
Katika wiki ya mwisho, limeibuka suala la vitisho kwa wabunge na madai kwamba baadhi ya wabunge kadhaa nao walipitiwa na mgawo wa fedha hizo.
Katika mlolongo wa vitisho hivyo, Kafulila jana alipokea ujumbe wa simu ukisema: “Nadhani umeamua kifo kwa kutafuta sifa za kijinga. Nakuhurumia sana maana hujui unapambana na nani. Huu ni ujumbe wa mwisho kwako. Kama huamini utaamini ukiwa kaburini.”
Baada ya kupokea ujumbe huo, mbunge huyo akiambana na Moses Machali (Kasulu Mjini - NCCR-Mageuzi) na Habib Mnyaa (Mkanyageni - CUF) walitoka bungeni jioni haraka kwenda polisi kutoa taarifa na hadi tunakwenda mitamboni hakukuwa na taarifa zaidi kuhusu tukio hilo.
Hali jana ilionekana shwari katika viunga vya Bunge tofauti na ilivyokuwa juzi na wiki zilizopita tangu Bunge lianze na wabunge wengi walikuwa hawataki kusikia kitu kingine zaidi ya ripoti ya escrow.
Kauli ya Zitto
Zitto alisema tayari amewasilisha barua kwa Spika kuhusu kukamilika kwa ripoti na kuwa yuko tayari kuiwasilisha baada ya kipindi cha maswali... “Tutatenda haki, aliyemo hatutamtoa na asiyekuwamo hatutamwingiza,” alisema Zitto.
Wakati Zitto akisema hayo, Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamis Kigwangalla katika akaunti yake ya Tweeter alieleza kama angekuwa mmoja wa watu waliochora mpango huo angekuwa ameshajiuzulu tangu Juni.
Yaliyojiri mahakamani
Uamuzi wa kutaka kila kitu kibaki kama kilivyo, ulitolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania na jopo la majaji watatu lililoongozwa na Jaji Radhia Sheikh. Wengine ni Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Richard Mziray.
Akisoma uamuzi huo kwa niaba ya wenzake jana, Jaji Sheikh alisema baada ya kusikiliza maombi ya dharura yaliyowasilishwa mahakamani hapo, wameona kila kitu chochote kibaki jinsi kilivyo (status quo) hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
IPTL na PAP ziliwakilishwa mahakamani hapo kupitia mawakili Gabriel Mnyele, Joseph Mwakandege na Felician Kay huku upande wa Serikali ukiwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Obadia Kamea.
Mwakandege alidai kuwa Bunge halifai kuingilia mambo ya Mahakama na haliruhusiwi kisheria kujadili mijadala ambayo ipo mahakamani.
“Sisi hatupingi kujadili escrow, bali tunataka ijadiliwe sehemu inayostahili ambayo ni mahakamani na siyo bungeni kwa sababu Bunge linatunga sheria na siyo kujadili ripoti,” alieleza Mwakandege.
Alisema wanataka mtu yeyote mwenye ushahidi auwasilishe mahakamani na si bungeni kwa kuwa mhimili wa kuamuru na kusikiliza masuala haya ni Mahakama na siyo Bunge.
Wakili Kamea alisema: “Tunaomba Mahakama itupe muda ili tuweze kupitia maombi yaliyowasilishwa kwetu kwa sababu tumepewa nusu saa tu kuyapitia.”
Walalamikiwa katika kesi hiyo ni Waziri Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, CAG, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Spika wa Bunge, Katibu wa Bunge, Bunge lenyewe na Mwenyekiti wa PAC.
Mawakili hao walifungua maombi hayo jana na kupewa namba 50 chini ya hati ya dharura, wakitaka tafsiri ya kisheria kuhusu ripoti ya CAG kama kilichofanywa katika uchunguzi wake ni sahihi ilhali kulikuwa na uamuzi wa kimahakama.
Pia walikuwa wanataka Bunge lisijadili mjadala wa escrow kwa sababu unahusu ripoti hiyo ya CAG. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 8.
Hata hivyo, jana jioni wabunge walipewa vitabu vyenye ripoti hiyo kwa ajili ya kuvisoma kabla ya kuanza rasmi mjadala mzito leo.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment