KARANI ASABABISHA MBUNGE WA NCCR-MAGEUZI APANDISHWE KIZIMBANI MAHAKAMA YA WILAYA KIGOMBA
Felix Mkosamali.
MBUNGE wa Muhambwe, Kibondo mkoani Kigoma, Felix Mkosamali amepandishwa kizimbani katika mahakama ya wilaya hiyo, akikabiliwa na shitaka la kumzuia karani kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajiwa kufanyika Desemba 14, mwaka huu.
Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Peter Makalla alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa wilaya hiyo, Erick Marley kuwa Mkosamali alitenda kosa hilo mwanzoni mwa wiki hii katika kitongoji cha Nduta Kijiji cha Kumhasha kata ya Murungu wilayani kibondo.
Alidai wakati karani huyo akiendelea na shughuli zake za uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa, Mkosamali alifika katika kituo hicho na kumzuia Hamidu Kabibili asiendelee kuwaandikisha wananchi, jambo ambalo ni ukiukaji wa sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa.
Makalla alidai kitendo cha mbunge huyo kuwazuia wananchi kujiandikisha ni kuwanyima haki yao ya msingi, ambapo wananchi baada ya kuwazuia waliendelea kudai kujiandikisha. Hata hivyo, mbunge huyo alizuia kutoendelea na kazi hiyo.
Awali, ilidaiwa Mbunge huyo alimnyang’anya karani huyo vitabu na madodoso yote na kuondoka navyo hadi ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kibondo, kinyume cha taratibu.
Baadae alikamatwa na Polisi kwa tuhuma za kufanya vurugu katika kituo cha kuandikisha wapiga kura. Mkosamali alikana shitaka hilo, ambapo Hakimu Marley baada ya kusikiliza pande zote mbili, aliahirisha kesi hiyo mpaka Desemba 29 mwaka huu.
Mtuhumiwa huyo yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti kwa kudhaminiwa na wadhamini wawili Sh milioni 2 kila mmoja.
0 comments:
Post a Comment