KUMBE SERIKALI INAJUA VIJIWE VYA WAUZA MADAWA YA KULEVYA KATIKA MIKOA YAKE YOTE YA TANZANIA !!.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi.
SERIKALI imetaja vijiwe vya wauzaji wa dawa za kulevya ‘unga’ vilivyopo katika mikoa mbalimbali nchini.
Pia, imesema inafanya uchunguzi ili kubaini kama Watanzania waliokamatwa na dawa za kulevya nchini China ni Watanzania kwa kuzaliwa au ni watu waliotumia tu pasi za kusafiria (pasipoti) za Tanzania.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya dawa za kulevya hapa nchini.
Alisema ni kweli kuna Watanzania zaidi ya 80, ambao wamekamatwa nje ya nchi kwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya. Lukuvi alisema kati yao, Watanzania 19 walikamatwa nchini China kwa kosa hilo la kukutwa na dawa za kulevya.
Alisema hivi sasa Serikali kwa kushirikiana na Balozi wa Tanzania nchini China, inafanya uchunguzi ili kuona kama watuhumiwa hao kweli ni Watanzania au wametumia pasi za kitanzania.
“Ni kweli kuna watu ambao wamekamatwa nchini China na wanasema ni Watanzania, sasa tunachofanya hivi sasa ni kuhakiki kama kweli hao ni Watanzania au wanatumia pasi za Tanzania za kughushi huku wakiwa si watanzania,’’ alisema.
“Hata mimi kuna mtu kapigiwa simu kaambiwa nimepata pancha njiani hivyo nahitaji fedha na alipotuma fedha akaona jina langu limejitokeza na aka tuma wakati si kweli ni suala la kughushi hivyo wanaweza kughushi hata pasi zetu,’’ alisema.
Alisema kati ya Watanzania 80 waliokamatwa nje ya nchi, Watanzania 29 walikamatwa Hong Kong, 27 Brazil, watano Kenya na 19 China. Lukuvi alisema Watanzania hao walikamatwa kuanzia Januari hadi Desemba 2013.
Alisema baadhi ya Watanzania hao, tayari wamehukumiwa vifungo na wengine wanasubiri hukumu zao. Kwa mujibu wa Lukuvi, pia katika kipindi hicho walikamatwa watuhumiwa wanane ambao ni raia wa Nigeria, Togo, Liberia na Sierra Leone.
Lukuvi alisema kwa upande wa Tanzania, dawa hizo za kulevya hutumika zaidi kwenye vijiwe mbalimbali nchini. Alisema vijiwe maarufu ni Ngarenaro na Mianzini mkoani Arusha, Msamvu (Morogoro), Hazina, Kituo Kikuu cha mabasi (Dodoma), Meko na Mbuyuni (Kilimanjaro).
Vijiwe vingine ni Kirumba, Nyamagana na Mbita(Mwanza), Kwa Mama John, Mafiati na Mwanjelwa (Mbeya), Vigaeni, Sinani na kituo cha mabasi (Mtwara), Mwanga na Ujiji (Kigoma), Majengo, Kakora na Makaburini (Shinyanga), Mtego wa Simba (Kahama) na Sahare, Deep Sea, kituo cha basi, Barabara ya 11 na 12 katika Jiji la Tanga.
Vijiwe vingine vinapatikana kandokando ya barabara kuu zinazounganisha mikoa na vituo vya mabasi na magari makubwa ya mizigo.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment