BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NYUMBA NA MABOMA YA WAGUGAJI ZAIDI 125 ZACHOMWA MOTO ULANGA MKOANI MOROGORO.


Baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Igata kijiji cha Mbalinyi kata ya Biro tarafa ya Ngohelanga wakiwa eneo la Nakasisis huku wakiishi katika mazingira magumu baada ya nyumba na maboma yao zaidi ya kaya 125 kuteketezwa kwa kuchomwa na moto kufuatia wafugaji kudaiwa kuishi katika hifadhi ya msitu wa kijiji hicho wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, tukio hilo lilitokea mwishino mwa mwezi wa 10 mwaka huu. Na Juma Mtanda, Morogoro.

Na Juma Mtanda, Ulanga.

Zaidi ya wananchi 3,200 kutoka katika kaya 130 za jamii ya wafugaji wamelazimika kuishi mazingira magumu huku wengi wao wakiishi kwa kulala chini ya miti kufuatia nyumba na maboma yao kuchomwa moto wakati wa operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu katika hifadhi ya msitu wa Igata katika kijiji cha Mbalinyi kata ya Biro tarafa ya Ngohelanga wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro.


Wakizungumza wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Mbalinyi Novemba 5 mwaka huu, jamii hiyo ilieleza kuwa aidha hiyo walianza kuipata baada ya serikali kuanza kutekeleza amri halali ya kuondolewa katika msitu huo unaodaiwa kuvamiwa na wafugaji tangu mwaka 2006.


Zoezi la kuwaondoa wafugaji hao linadaiwa lilianza kwa kuondolewa mifugo usiku wa manane kisha kufuata uchomaji moto ikiwa sehemu ya kuwashinikisha kuondoka kufuatia kukaidi kuondoka kwa hiyari baada ya muda wa notisi iliyotolewa na ofisi ya mkuu Ulanga kumalizika muda wake.


Akizungumzia tukio hilo katika eneo hilo la mkutano mmoja wa wafugaji hao Masanja Msafiri (47) alieleza kuwa zoezi la kuwaondoa wafugaji katika msitu wa Igata kwa nguvu lilifanyika kwa siku tatu likianzia Oktoba 29 na kumalizika 31 mwaka huu kwa askari polisi ikishirikiana na mgambo wa kata za Biro, Ngohelanga na wale wa kijiji cha Mbalinyi kuondoa mifugo nyakati za usiku kisha kuwapeleka katika uwanja wa shule ya msingi kijijini hapo.


Masanja alisema kuwa kwa sasa jamii ya wafugaji hao wanaishi katika mazingira magumu ikiwemo kulala chini ya miti huku watoto wakilala katika vibanda vilivyofunikwa mifuko ili kuwakinga na jua na mvua huku wengine wakipata hifadhi kwa ndugu na jamaa.


“Zoezi la operesheni ya kuwaondoa wafugaji na mifugo yao kwa nguvu lilianza rasmi oktoba 29 hadi 31 mwaka huu kwa kuondoa mifugo kwa kila kaya ambapo wafugaji hao walilazimika kulipa faini ya kila mfugo kulipia kiasi cha sh5,000 na kuendelea wakijumisha mbuzi, kondoo na ng’ombe.”alisema Masanja.


Masanja alisema kuwa baada ya kumalizika kwa kazi ya kuondoa mifugo kwa siku tatu, oktoba 31 hadi Novemva 1 mwaka huu kazi ya kuteketeza nyumba na maboma ilianza na baadhi ya wafugaji kuanza kupata adha ya kulala nje chini ya miti.


Masanja alidai kuwa zoezi hilo liliendeshwa nyakati za usiku wa manane kati ya saa 9 na saa 10 kwa kuamusha wahusika na kuamuru kutoa mali zilizopo ndani ambapo zoezi hilo linadaiwa kusababisha upotevu wa baadhi ya mali kupotea ikiwemo fedha, kuku na nguo.


Wande Shabaan (27) yeye alieleza kwa kusema kuwa kwa sasa familia yake yenye zaidi ya watu 20 wanaishi katika mazingira magumu eneo la Nakasisi kwa kulala nje chini ya mti huku watoto wakilala katika kibanda kilizofunikwa mifuko ya nailoni.


Wakati wafugaji wakielezea kusanyanyasika katika operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu katika hifadhi ya msitu wa Igata baada ya kuvamia tangu kwama 2014, uongozi wa serikali ya kijiji cha Igata na ule wa wilaya ya Ulanga umekanusha kuwanyanyasa.



Kaimu afisa mtendaji wa kijiji cha Mbalinyi kata ya Biro wilaya ya Ukanga mkoa wa Morogoro, Petro Msaliboko alisema kuwa eneo la Igata ulitengwa na kijiji mwaka 2004 ili kuwa hifadhi yam situ kabla ya kuvamiwa na makundi ya wafugaji kuanzia mwaka 2006 na 2007.


Msaliboko alisema kuwa mwaka 2006 mmoja wa wafugaji aliuliziwa eneo jirani na hifadhi hiyo na mwanakijiji wa Mbalinyi lakini kadri siku zilivyoenda na miaka wafugaji wanadaiwa kumiminika na kugeuza makazi na malisho hali iliyopelekea msitu huo kuharibiwa kutokana na shughuli za makazi, kilimo, ufugaji na malisho.


“Hifadhi ya msitu wa Igata ina ukubwa wa heka 978 na baada ya serikali ya kijiji kuona msitu umevamiwa na wafugaji ilianza kwa kubainisha alama za mipaka mwaka 2010 na mwaka 2012 ilianza kuendesha operesheni ya kuwaondoa ndani ya hifadhi lakini zoezi hilo liligonga mwamba hadi mwaka huu 2014 lilipofanikiwa kwa asilimia 100.”alisema Msaliboko.


Msaliboko aliongeza kuwa wanashukuru amri ya Rais Jakaya Kikwete ya kuwaamrisha wakuu wa mikoa kujenga maabara ya sayansi kwa kila shule za sekondari za kata kwani imemsukuma mkuu wa wilaya yao, Francis Miti kuhamasisha wananchi kujitolea katika nguvu kazi kufanikisha zoezi hilo katika shule ya sekondari ya kata yao.


“Tunashukuru amri ya JK ya kuwataka wakuu wa mikoa kusimamia ujenzi wa majengo ya maabara ya shule za sekondari za kata kwani hali hiyo imesaidia mkuu wa wilaya yetu kutoa amri ya kumtaka kila mwananchi kuweka nguvu zake lakini wakati akitoa amri hiyo wananchi walimpachika swali kwa nini amesimamia kidede katika ujenzi wa majengo ya maabara huku msitu wa Igata ukiendelea kutekea na wafugaji ?, walihoji wananchi wakati wa mkutano wake wa hivi karibuni.”alisema Msaliboko.


Msaliboko alisema kutokana na kauli hizo za wananchi kuhoji kwa mkuu wa wilaya ilisaidia kutoa askari na kufanikisha operesheni hiyo.


Afisa misitu wilaya ya Ulanga mkoa wa Morogoro, Tumaini NnkoElisha akizungumza wakati wa kikao kilichoitishwa na katibu tawala wilaya ya Ulanga, Steven Mapunda kikishirikisha afisa mifugo wilaya Jackson Jekonia, afisa wanyamapori na mwanasheria wa halmashauri hiyo alisema kuwa operesheni ya kuwaondoa wafugaji ilikuwa ikianza majira ya 12 asubuhi na kufikia kikomo majira ya saa 12 jioni.


Akieleza katika kikao hicho, NnkoElisha alisema kuwa kabla ya kuchoma nyumba na maboma moto walizingatia haki kwa kumwamuru kila mfugaji ndani ya nyumba yake ama boma kuondoa vitu vyote na baada ya kumalizika kwa kutoa mali ndani kisha zoezi la uchomaji moto ulifanyika kwa kila mhusika kuchukua jukumu la kuteketeza nyumba ama boma.


“Kilichofanyika kwa askari, mgambo na maafisa wengine ni kuhakikisha kila kitu kinatoka ndani ya nyumba ama boma na baada ya yeye mhusika kuhakikisha kila kitu kimetoka ndani huchukua jukumu la kuteketeza kwa kuchoma moto boma au nyumba lakini ni baada ya kusaini katika kitabu chetu kuwa amekubaliana na operesheni yetu kwa ni operesheni halali baada ya wao kushindwa kuondoka kwa hiyari na kuisha kwa muda uliotolewa wa kuwataka kuondoka katika hifadhi ya msitu.”alisema NnkoElisha.CHANZO/MTANDA BLOG
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: