BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAHAKAMA KUU YA TANZANIA YAIAMURU BUNGE KUTOJADILI MJADALA UCHOTAJI WA FEDHASH 306 BILIONI ZA AKAUNTI YA ESCROW ZILIZOCHOTWA NA VIGOGO WA SERIKALI YA RAIS DR JAKAYA MRISHO KIKWETE.

http://www.ippmedia.com/media/picture/large/Anne-Makinda(1).jpg
Spika wa Bunge, Anne Makinda.

WAKATI umma wa Watanzania ukisubiri kwa hamu kusikia juu ya mjadala wa sakata la akaunti ya Tegeta Escrow uliokuwa umepangwa kuunguruma kwa siku mbili kuanzia leo, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imeliamuru Bunge kusitisha kutoa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG).


Majaji watatu, Razia Begum Sheikh, Richard Mziray na Lugando Mwandambo ndio waliotoa uamuzi huo jana na kusema hatua zozote zisichukuliwe kujadili ripoti hiyo bungeni hadi hapo kesi ya msingi itakaposikilizwa.

Kesi hiyo ya madai namba 50 ya mwaka 2014 ilifunguliwa jana na kampuni mbili ikiwamo Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Kampuni ya Pan Africa Power Solution (PAP) dhidi ya Serikali.

Hata hivyo, wakati mahakama ikiweka zuio hilo, Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema hakuna chombo kingine kinachoweza kulizuia Bunge kuendelea na mjadala wa sakata la Escrow huku akisema kama mambo yatakwenda kama yalivyo, linatua bungeni leo.

Makinda alisema hayo wakati leo kwa mujibu wa ratiba, Bunge linatarajiwa kupokea uchambuzi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu sakata hilo la Tegeta Escrow.

Tangu Novemba 18, mwaka huu, Kamati ya PAC inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), ilikuwa imejifungia katika Jengo la Hazina mjini hapa, ikifanya uchambuzi wa ripoti hiyo baada ya kuwa imewasilishwa kwa Spika, Novemba 14, mwaka huu.

Kufikia jana jioni, kamati ya Zitto ilikaririwa ikisema iko tayari kuwasilisha ripoti hiyo muda wowote, kwa kuwa imekuwa ikifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha jukumu walilokabidhiwa linakamilika kwa wakati.

Lakini jana, kwa mara nyingine, wabunge waliomba miongozo kwa Spika yote ikijikita katika sakata hilo, akianza na Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP) aliyehoji kuwa kuna taarifa kwamba Bunge linazuiwa kujadili suala hilo, hivyo akataka kufahamu mwongozo wa Spika.

Akijibu hoja hiyo, Makinda alisema kazi za kibunge haziwezi kuzuiwa na mtu yeyote na kuwaambia wabunge, “msiishi kwa wasiwasi. Nawafahamu ndani kwa majina, ripoti ya CAG, hatutaweka katika pigeon hall (visanduku vya mawasilino) zenu ili zisije kuchukuliwa na mtu mwingine. Nagawa kwa sababu hii itakuwa ni kiambatanisho kuhusu ripoti ya PAC.”

Alisema kwa mujibu wa Kanuni, anasubiri Mwenyekiti wa PAC amwandikie kumuarifu kuwa wamemaliza kazi yao na kwamba ripoti iko tayari kuwasilishwa bungeni, hivyo akipata taarifa hiyo, atafuata Kanuni za Bunge zinavyoelekeza.

Alisisitiza katika kesi zilizofunguliwa mahakamani kuhusu sakata la IPTL, kampuni ya kufua umeme yenye mitambo yake Tegeta, Dar es Salaam, hakuna hata moja inayozuia jambo hilo la Tegeta Escrow kujadiliwa bungeni.

Hali hiyo ilimfanya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), kusimama na kuomba mwongozo huku akinukuu kesi inayodaiwa kufunguliwa jana katika Mahakama Kuu na IPTL, ikiweka zuio kwa Bunge kujadili suala hilo.

“Kwa sheria yetu ya Kinga na Madaraka ya Bunge hatuwezi kuzuiwa. Taratibu zetu ziko sawa, ije tu,” alisema Makinda na kuzuia miongozo zaidi kwa wabunge na kuruhusu kuwasilishwa kwa Muswada wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) jana asubuhi.

Kwa wiki kadhaa sasa, Bunge limetawaliwa ndani na nje na mjadala huo wa Tegeta Escrow ambao pia unatawala mazungumzo mengi nchini kwa sasa kutokana na madai ya uchotaji wa Dola za Marekani milioni 200 (zaidi ya Sh bilioni 300) zinazohusisha kampuni hiyo ya IPTL.

Juzi wakati akijibu hoja za wabunge katika Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2014, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, aliwaonya wabunge kuacha kuchafuana kwani hiyo inaweza kuwafanya watuhumiwa wengine kuja kulalamika kuwa wamehukumiwa kabla ya kusikilizwa (mis-trial).

Zuio la Mahakama.
Mahakama Kuu imezuia ripoti ya CAG baada ya kampuni za IPTL na PAP kuwasilisha mahakamani maombi mawili ambayo ni kutafsiri ripoti ya kisheria ya CAG ili kujua ukweli uliopo katika ripoti hiyo na kwamba Bunge lisiingilie masuala ya mahakama ambapo suala la Esrow wanatakiwa kupeleka ushahidi wote katika mamlaka husika ambayo ni mahakama.

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Waziri Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Spika wa Bunge, Mwenyekiti wa PAC, Kurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), CAG, Makarani wa Bunge na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.

Katika kesi ya msingi, Wakili wa utetezi, Joseph Makandenge alidai kwamba tayari kuna kesi 10 zinazozungumzia masuala ya hayo na kwamba kabla mahakama haijamaliza kusikiliza kesi hiyo, tayari wabunge wameanza kutoa madai mapya.

Alidai kwamba kila mtu mwenye ushahidi atatakiwa kupeleka ushahidi wake mahakamani na sio kuzungumzia katika Bunge kwani kila chombo kina mamlaka yake. Pia alidai wabunge hao wanatakiwa kuheshimu maagizo ya mahakama na kwamba kesho (leo) hawatasikia ripoti yoyote ya CAG.

Hata hivyo, upande wa mashitaka kupitia mawakili wanne wa serikali Obadia Kamea, Killy Mutas, Michael Luena na Haroun Matagane ulidai kwamba walipewa nusu saa, kati ya saa 7:30 na saa 8:00 mchana, kupitia madai yaliyowasilishwa na kampuni hizo hivyo waliomba muda kwa ajili ya kukusanya taarifa zaidi kuhusu serikali.

Pia waliomba kwamba wadaiwa wasikilizwe, kwani haki haitatendeka endapo upande huo hautasikilizwa. Hata hivyo mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi hayo na kwamba kesi iliahirishwa hadi Desemba 8 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi kwa maombi ya IPTL.

Isemavyo Katiba Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Ibara yake ya 100 kifungu kidogo cha kwanza kinachozungumzia Madaraka na Haki za Bunge, kinasema:


“Kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika Mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.”

Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu akizungumzia amri hiyo ya mahakama baada ya kuombwa mwongozo na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu juu ya jambo hilo, alisema: “Kiti hakina taarifa rasmi kuhusu uamuzi wowote uliochukuliwa na chombo chochote cha ndani au cha nje ya nchi. 


Uamuzi wa Spika wa leo (jana) asubuhi upo pale pale na ripoti ziendelee kugawiwa…” Hii ina maana kwamba, mjadala huo utaendelea kama ilivyokuwa imepangwa na bunge hilo.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: