WANANCHI KIPATO CHA CHINI TANZANIA SASA KUWA NA UWEZO WA KUJENGA NYUMBA BORA BAADA YA SERIKALI KUFUTA KODI.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum
SERIKALI imewasilisha Muswada wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) bungeni ambao ukipitishwa, utatoa msamaha kwenye nyumba za upangishaji za makazi ili ku wawezesha wananchi wenye kipato cha chini kupata makazi bora kwa bei rahisi.
Aidha, muswada huo unakusudia kutoa msamaha wa VAT katika vifaa vya masomo ya sayansi kwenye maabara, msamaha kwenye vifaa mbalimbali vya umeme utokanao na jua, vifaa vya elimu kama vitabu, magazeti, vifaa vinavyotumiwa na watoto kuchorea, ramani, picha zilizopigwa angani na karatasi zinazotumika kuchapishia maswali ya mitihani.
Pia unakusudia kutoa msamaha wa VAT kwenye huduma za mazishi, kwenye bidhaa za mchele, mtama, ulezi na nyingine za nafaka, vifaa vya utabibu vya kiti maalumu cha wagonjwa (wheel chair) na fimbo maalumu ya watu wenye ulemavu wa macho.
Akiwasilisha muswada huo, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema lengo la muswada ni kuboresha mfumo wa kutoza na kukusanya kodi, kuweka utaratibu mzuri wa ulipaji wa kodi na kuziba mianya ya ukwepaji wa Kodi ya Ongezeko la Thamani.
Alisema madhumuni yake ya kwanza ni kutunga Sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kupanua wigo wa kodi hiyo na kuongeza mapato ya Serikali.
“Pili, kuweka utaratibu ambao utawawezesha walipa kodi kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani ambao haukuwekwa bayana katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148, kwa mfano utozaji wa kodi kwenye huduma zinazoingizwa kutoka nje ya nchi, utozaji wa kodi kwenye huduma zinazotumika nje ya nchi, uuzaji wa sehemu ya biashara au biashara yote na kadhalika,” alisema Salum.
Alisema tatu ni kujenga mfumo imara wa ukusanyaji kodi ya VAT na kuondoa baadhi ya misamaha ya kodi isiyokuwa na manufaa au tija kwa Taifa inayotumika sasa.
Hata hivyo, alisema ili kulinda misamaha ambayo Serikali iliridhia kutoa kwa wawekezaji katika sekta ya madini, mafuta na gesi, unafuu wa kodi ya VAT uliotolewa kwenye sheria inayotumika hivi sasa, utaendelea kutumika kwa mikataba iliyosainiwa na Serikali na kampuni za utafitina utafutaji wa madini (MDAs) na katika utafiti na utafutaji wa mafuta na gesi (PSAs) kabla ya kutungwa kwa sheria mpya ya VAT.
Katika muswada huo wa sheria, yamefanyika marekebisho ili kuongeza msamaha wa VAT kwenye vifaa vya kilimo hasa zile zinavyohusika na kilimo cha umwagiliaji, msakama kwenye mashine na vifaa vya uzalishaji na usindikaji wa maziwa kama matangi ya kuhifadhia maziwa, mashine ya kukata na kufungashia majani ya kulishia mifugo.
“Kuweka utaratibu wa kukusanya mapato kwenye huduma za bima isipokuwa bima ya maisha na afya, haki miliki na malipo yasiyofanywa kwa kutumia fedha taslimu,” alisema Salum na kuongeza: “Ili kuimarisha usafiri wa reli nchini, marekebisho yamefanywa ili kutoa msamaha kwa vifaa vinavyotumika katika usafiri wa treni kama vile mabehewa, reli na mataruma.
Aidha, imeongezwa sehemu ili kutoa msamaha wa VAT kwenye vifaa na magari ya zimamoto yatakayonunuliwa na Serikali.
” Kwa mujibu wa waziri huyo, pia muswada umebainisha kuwa msamaha wa VAT unaotolewa sasa katika huduma za utalii uendelee kutolewa kwa mwaka mmoja pindi muswada huu utakapopitishwa kuwa sheria, lengo ni kulinda miadi ambayo tayari imeingiwa baina ya watalii na wawekezaji katika sekta hii kabla ya mapendekezo ya muswada huo.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment