NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI APENYA KATIKA TUNDU LA SINDANO SAKATA YA AKAUNTI YA ESCROW.
Masele avuka kiunzi cha kuvuliwa uongozi
Dodoma. Bunge limefuta pendekezo la Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) lililotaka Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele kuwajibika kuhusiana na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Bunge lilifikia uamuzi huo mjini Dodoma juzi baada ya mvutano mkali kati ya wabunge na Serikali kuhusu utekelezaji wa mapendekezo ya PAC.
Katika kupitia mapendekezo ya PAC, Serikali ilileta hoja ya kubadilisha mapendekezo ya kamati hiyo ambayo yalijadiliwa ndani ya Bunge. Bunge liliazimia vyombo vinavyohusika na uchunguzi kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow kuendelea na uchunguzi na vile ambavyo havijaanza vifanye hivyo ili kubaini ukweli na kuchukua hatua kwa watu wote waliohusika.
Pia, Bunge liliazimia kuzitaka mamlaka zinazohusika ikiwamo Benki Kuu kuchukua hatua dhidi ya benki zote zilizohusika na miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Azimio jingine ni kuitaka Serikali ifanye mapitio yote ya mikataba ya umeme na kutoa taarifa bungeni kabla ya kikao kinachofuata cha Bunge kuhusu utekelezaji wake mapema kabla ya Bunge la Bajeti la mwaka 2015/2016.
Kuhusu kuiwajibisha bodi ya Shirika la Umeme nchini, (Tanesco), Bunge liliishauri Serikali ifanye uchunguzi na kuwachukulia hatua wote waliohusika na kashfa hiyo.
Kuhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi kuwajibika kutokana na sakata hilo, Bunge limeazimia kulifikisha suala hilo kwa mamlaka ya uteuzi kwa hatua zaidi.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment