SHEIKHE PONDA ISSA PONDA AACHIWA HURU NA MAHAKAMA KUU YA KANDA YA DAR ES SALAAM.
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Shekhe Issa Ponda (mwenye kanzu) akiingia Mahakama Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam jana kusikiliza kesi inayomkabili. (Picha na Yusuf Badi).
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemwachia huru Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Shekhe Issa Ponda kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha makosa dhidi yake.
Shekhe Ponda aliwahi kutiwa hatiani na Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Juni 2, mwaka jana, kwa kosa la kula njama kuingia kwa nguvu katika eneo lililopo Chang’ombe wilaya ya Temeke na kupewa adhabu ya kifungo cha miezi 12 jela.
Akitoa hukumu hiyo jana, Jaji Augustine Shangwa alisema ushahidi uliotumika Mahakama ya Kisutu kumtia hatiani Shekhe Ponda ulikuwa na mapungufu hivyo uliacha shaka.
Alisema upande wa mashitaka haukuthibitisha kwamba Shekhe Ponda aliwaamuru wafuasi wake kuvamia katika eneo hilo. Licha ya Ponda kuachiwa huru, bado anakabiliwa na mashitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro alikokuwa na kesi ya uchochezi.
Shekhe Ponda alishitakiwa katika Mahakama hiyo Agosti 19, mwaka jana, akikabiliwa na mashitaka matatu ya kutotii amri halali ya Mahakama.
Mwendesha mashitaka alidai kwamba Shekhe Ponda walifanya makosa hayo Agosti 10, mwaka jana katika Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege katika Manispaa ya Morogoro. Ponda alidaiwa kukiuka amri ya Mahakama kwa kutoa kauli za uchochezi na kuichochea jamii kufanya fujo.
Kulingana na mwendesha mashitaka, Shekhe Ponda alichochea waumini wa Kiislamu na kwamba Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA), walikuwa ni vibaraka wa CCM na serikali na hivyo wanapaswa kuwapiga.
Taarifa hiyo alidaiwa kupinga agizo la Mahakama ya Kisutu. Inadaiwa kwamba kwa misingi hiyo, kauli iliyotolewa na Ponda ni ya uchochezi kwa makusudi, akisema serikali iliingiza jeshi Mtwara ili kuleta machafuko ya wananchi ambao walikuwa wanapinga ujenzi wa bomba la gesi.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment