VIGOGO WA SERIKALI YA DK JAKAYA KIKWETE WALIOCHOTA FEDHA ZA AKAUNTI YA TEGETA ESCROW ZAIDI YA BILIONI 300 SASA TUMBO JOTO, BUNGE KUENDELEA KUWASAKA MJINI DODOMA.
NAIBU SPIKA JOB NDUGAI.
SASA ni rasmi kuwa mjadala wa wiki ijayo kuhusu sakata la utoaji fedha zaidi ya Sh bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa katika Benki Kuu (BoT), inayohusu Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), umeongezewa muda.
Naibu Spika, Job Ndugai amethibitisha kuwa mjadala huo utakuwa wa siku mbili badala ya siku moja wiki ijayo, ambayo ni ya mwisho ya mkutano wa 16 na 17 wa Bunge ulionza Novemba 4, mwaka huu mjini hapa.
“Ni kweli mjadala utafanyika wiki ijayo kwa siku mbili,” alisema Ndugai jana katika Viwanja vya Bunge, alipokuwa akizungumza baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Uongozi ambacho pamoja na mambo mengine, kilitarajiwa kuamua kuhusu mjadala wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu fedha hizo.
Kwa mujibu wa Kamati ya Uongozi, sasa mjadala huo ambao unasubiriwa kwa hamu na Watanzania, utafanyika kwa siku mbili, kuanzia Novemba 26 badala ya siku moja ya awali ya Novemba 27, mwaka huu iliyopangwa katika ratiba ya awali.
Bunge litamaliza kazi zake Novemba 28, mwaka huu ambapo pamoja na suala la ripoti hiyo ya CAG, wiki ijayo pia kutakuwa na muswada kuhusu Marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Akaunti hiyo ilifunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) baada ya kuwapo kwa mgogoro wa kibiashara ya Tanesco na IPTL, kampuni inayofua umeme yenye mitambo yake Tegeta, Dar es Salaam.
CCM kukaa leo
Aidha, imefahamika kuwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), watakutana leo jioni katika kikao chao ambacho hakuna shaka suala la IPTL litachukua nafasi.
Mmoja wa wabunge wa chama hicho alithibitisha jana kwenye viwanja vya Bunge kwamba watakutana leo jioni.
“Ndio, tuna kikao kesho (leo) jioni,” alisema mbunge huyo na alipoulizwa wanakwenda kujadili nini, alisema; Mjadala si unajulikana, lakini kama wapo waliohusika, basi wenyewe wapime, chama kiachwe salama.”
Kwa sasa, ripoti ya CAG inapitia na kuandaliwa uchambuzi na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema).
Zitto akitoa ushauri kwa Naibu Spika wakati mjadala ulipozuka Jumatano wiki hii, alisema kimsingi ripoti hiyo inapaswa kuwasilishwa bungeni ili umma ufahamu ukweli na jambo hilo lifike mwisho.
Juzi, Bunge lilisema ratiba ya mkutano wake wa 16 na 17 itaendelea kama ilivyo na kwamba hakuna barua yoyote kutoka katika mahakama iliyozuia kujadili ripoti kuhusu sakata lafedha za Tegeta Escrow.
Jumatano wiki hii, kuliibuka mabishano makali bungeni kwa wabunge kuonesha hisia kuwa ipo barua kutoka kwa mhimili mwingine wa dola, mahakama ikizuia Bunge kujadili suala hilo lililozua gumzo nchini.
Wabunge hao walidai kuwa mahakama haina uwezo wa kuwazuia kujadili suala hilo, na kwamba wanataka ripoti ya CAG iwasilishwe bungeni kama ilivyopangwa.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu aliyekuwa akiongoza kikao cha juzi asubuhi, alisema hakuna barua yoyote iliyoandikwa na mahakama kwenda kwa Bunge.
“Hakuna barua ya Mahakama iliyoandikwa kuizuia Bunge kujadili suala la Escrow. Uhusiano wa Bunge na Mahakama ni mzuri na wa kuheshimiana. Ratiba ya Bunge itakwenda vile vile,” alisema Zungu.
Wakati akizungumza baada ya ushauri wa wabunge juzi kuhusu suala hilo, Naibu Spika, Job Ndugai alisema suala hilo litapelekwa kwa Kamati ya Uongozi, huku akiahidi kuwa Kiti cha Spika “kitatenda haki.”
Fungate ya Kafulila Naye Fadhili Abdallah anaripoti kutoka Kigoma kwamba, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), aliyeoa jana, amelazimika kuahirisha fungate ili ashiriki mjadala huyo wa IPTL.
Akizungumza katika harusi hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), alimpongeza Kafulila kwa kukamilisha ndoa yake na mwenza wake na kumuomba mke wa Kafulila, Jesca kuwa mvumilivu katika kipindi hiki kwani hawatakuwana na mume wake katika fungate, hadi watakapomaliza kushughulikia suala hilo.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment