BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WABUNGE WAMTOLEA UVIVU KABWE BUNGENI ETI NI KIONGOZI MBOVU NA MBADILIFU.

http://freemedia.co.tz/daima/wp-content/uploads/2014/11/kabwe.jpg
BUNGE limemshughulikia Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe, likitaka ang’olewe kwa madai ni kiongozi mbovu, mbadhilifu na amekuwa akizua vurugu kila anakohamishiwa.

Pamoja na kuibua matatizo kila alikohamishiwa, imeelezwa Serikali imeendelea kumlinda kwa kumhamishia kituo kimoja baada ya kingine.

Hatua hiyo ilitangazwa jana na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, wakati akijibu mwongozo wa Spika ulioombwa na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA).

Selasini, aliomba mwongozo huo baada ya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kuliambia Bunge kuwa Kampuni ya Tanzania Building Works Limited, inachunguzwa kwa kushindwa kutekeleza ujenzi wa soko la Mwanjelwa mkoani Mbeya kwa wakati, hivyo kunyang’anywa kazi hiyo.

Mbunge huyo, alihoji iwapo kampuni hiyo itachunguzwa, kwanini Kabwe naye asichunguzwe kwa madai kuwa kila anapohamishiwa, huhama na kampuni hiyo na kuipa tena kazi.

Akijibu mwongozo huo, Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Ilala jijini Dar es Salaam, alisema ingawa ana maslahi katika hoja hiyo, anailaumu Serikali kwa kumlinda Kabwe.

Bila kumung’unya maneno, Zungu alisema serikali bado ina uzembe wa kulea viongozi wabovu kwa kuwahamisha kutoka sehemu moja hadi nyingine.

“Huyu Kabwe ni tatizo kubwa sana. Na siyo tatizo Dar es Salaam, amefanya tatizo Mwanza. Chama Cha Mapinduzi kimekosa uongozi Mwanza sababu ya huyu Mkurugenzi…

“Huko Mbeya amefanya fujo, sasa mnaleta Dar es Salaam anafanya fujo. Tumetangaza na tumetoa taarifa serikalini mipaka ya halmashauri imechukuliwa, Tamisemi wamekaa kimya, mkuu wa mkoa amekaa kimya.

“Mimi naiagiza serikali na leo hoja hii ya huyu Mkurugenzi tunakwenda nayo kwa Waziri Mkuu,” alisema Zungu.

Awali, Selasini akiomba mwongozo huo, alisema Kabwe akiwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, ndiye aliyeipa kampuni hiyo kazi hiyo.

Hata hivyo, alisema Kabwe aliondoka Mbeya baada ya kelele za madiwani na wananchi na kuliachia jiji hilo hasara kubwa.

“Kabwe huyo huyo alipelekwa Mwanza na pale Mwanza ameacha hasara kubwa sana. NSSF pamoja na viwanja, ambavyo aliuza na fedha hazikujulikana zilikokwenda. Lakini amehama na kampuni hii,” alisema Selasini.

“Kabwe huyu huyu aliondoka Mwanza baada ya kelele kubwa za wananchi pamoja na madiwani. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Wilson Kabwe yuko pale Dar es Salaam, Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam,” alisema.

Alisema akiwa Dar es Salaam, nako pia ameanzisha mtafaruku mkubwa akipora vitega uchumi vya manispaa akivifanya kuwa vya jiji.

Selasini, alisema Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeshatoa maelezo na mapendekezo mengi kwa serikali kuhusu Kabwe, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, picha inayotolewa ni kwamba, inawezekana Wilson Kabwe ana wakubwa wanaomlinda huko Tamisemi,” alisema Selasini.

Selasini, alimaliza kuomba mwongozo wake kwa kusema kuwa kama kampuni ya Tanzania Building Works inachunguzwa na Mkurugenzi huyo achunguzwe kwani amekuwa akihama nayo kila anapohamishiwa licha ya kushindwa kufanya kazi.TANZANIA DAIMA.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: