CCM YAANDAA HUKU NDANI YA MASAA 72 TU KUWAHUKUMU VIGOGO WAKE AKIWEMO LOWASSA, CHENGE, PROF TIBAIJUKA NA NGELEJA.
Dar es Salaam. Kamati Kuu ya CCM, itakuwa na vikao vizito kuanzia Jumatatu kujadili masuala mbalimbali yanayokikabili chama hicho.
Mambo makubwa yanayotarajiwa kuchukua nafasi katika vikao hivyo vitakavyoanza saa 72 zijazo ni kuwajadili wanachama wake ambao baadhi ni mawaziri waliokumbwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow na tathmini ya wanachama wake sita walio katika adhabu ya mwaka mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kudaiwa kufanya kampeni za urais kabla ya muda.
Pia kamati hiyo, inatarajia kutumia vikao hivyo kuangalia namna ya kupata wagombea watakaokubalika na wananchi kuelekea kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
Akiwa katika ziara ya kuwashukuru wananchi kwa kuipa CCM ushindi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mkoani Tanga hivi karibuni, Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana alisema chama hicho kitaanza rasmi vikao vyake vya ngazi ya Taifa kupitia masuala mbalimbali yanayokihusu.
Alipoulizwa kuhusu agenda hizo katika vikao hivyo jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikuja juu na kusema hakuna kitu kama hicho... “Hata mkiiandika vibaya CCM, itashinda tu,” na kisha kukata simu.
Hata hivyo, habari zilizopatikana jana jioni kutoka ndani ya CCM, zinasema kuwa sekretarieti ya chama hicho, inakutana leo mjini Dodoma kuandaa ajenda za kikao hicho kitakachoanza Jumatatu ijayo.
Mawaziri waliokumbwa na kashfa ya escrow ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye ni pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Profesa Tibaijuka tayari ameondolewa kwenye nafasi yake ya uwaziri baada ya kukiri kupewa Sh1.6 bilioni na Mkurugenzi wa VIP Engineering, James Rugemalila.
Wengine waliotajwa kupewa mgawo na Rugemalila ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba, William Ngeleja.
Pia Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo yupo katika uchunguzi kuhusiana na kashfa hiyo.
Mbali na wahusika wa Akaunti ya Escrow, kikao hicho cha Kamati Kuu ya CCM kitachunguza maadili ya viongozi wakiwamo waliokumbwa na zuio la kujihusisha na kampeni kwa miezi 12, huku mienendo yao ya kisiasa ikifuatiliwa.
Watakaojadiliwa ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi, Teknolojia, January Makamba, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Kinana akiwa Tanga alikaririwa akisema: “Wiki ijayo tunaanza kukaa vikao vya kupimana sisi viongozi juu ya uadilifu wetu ndani ya Serikali, tunataka kuwa na viongozi wenye kujua Watanzania wanataka nini na uadilifu wao usiwe hata na chembe ya shaka.”
Alisema salamu za CCM kwa Watanzania kwa mwaka 2015 ni ahadi ya kuweka mkazo katika maadili kwa viongozi wake na kwamba itafanya tathmini kwa lengo la kujipanga kwa uchaguzi mkuu ujao.
“Watanzania wanataka viongozi wasiokuwa na urasimu umangimeza, wenye mlolongo wa itifaki na wanaoweza kushuka chini,” alisema Kinana.
Msingi wa hukumu
Kikao cha tathmini cha wiki ijayo ni mfululizo wa baada ya kikao cha mwisho cha Agosti mwaka jana kilichokutana chini ya Mwenyekiti wake, Philip Mangula kupitia taarifa za utekelezaji wa adhabu kwa makada sita wa chama hicho wanaodaiwa kuanza kampeni kuwania urais kabla ya wakati.
Kufanyika kwa kikao hicho kulitokana na agizo la Mangula ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, alilolitoa Februari 8, mwaka jana akizitaka ofisi zote za ngazi ya mikoa na wilaya kufungua mafaili kupitia mienendo ya wagombea walioanza kampeni za uchaguzi wa kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati.
Makada hao waliozuiwa kujihusisha na kampeni kwa miezi 12 na adhabu zao zinamalizika Februari 18.
Hatua ya kufanyia tathmini hiyo ni kutokana na kuelezwa kuwa pamoja na adhabu hiyo, baadhi yao walikuwa wakikiuka na kuendelea na mikakati ya kampeni kwa kukusanya watu wa kupanga nini cha kufanya tayari kwa uchaguzi wa mwaka huu.
Katika kikao hicho cha Kamati Ndogo ya Maadili na Nidhamu, ilielezwa kuwa katika kipindi cha miezi kadhaa, timu za maofisa usalama wa chama zilisambazwa mikoa yote na kukusanya taarifa za makada hao.
Kikao kama hicho cha Kamati Kuu kilikutana Julai 16, mwaka jana na kupokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonyesha nia ya kuomba ridhaa ya chama kuwania urais.
Kutokana na hali hiyo, Kamati Kuu iliitaka Kamati ya Maadili kufanya marejeo na kuangalia utekelezaji wa adhabu kwa makada hao sita.
Siku moja baadaye, Julai 17, mwaka jana, Nape alisema endapo Kamati ya Usalama na Maadili itabaini kama makada hao walikiuka mwenendo wa utekelezaji wa adhabu waliyopewa, watapoteza sifa...
“Baada ya kutafakari kwa kina, Kamati Kuu inapenda kuwakumbusha kuwa ili wasipoteze nia ya kugombea ni muhimu wakazingatia katiba, kanuni na taratibu za chama zinazosimamia masuala hayo.”MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment