HIVI NDIVYO ILIVYOKUWA KUPATA KWA AJALI MEYA WA MANISPAA YA MORO NA WAANDISHI WA HABARI KATIKA MSAFARA WA MKUU WA MKOA.
Meya wa Manispaa ya Morogoro, Amir Nondo akisaidiwa na baadhi ya Madiwani wa Manispaa hiyo alipofikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro baada ya kupata ajali eneo la Mzambarauni Darajani. Gari lake liligongana na Basi la Happy Africa lililokuwa likitokea Njombe kuelekea Dar es Salaam katika barabara kuu ya Dar es Salaam jana. Picha na Juma Mtanda.
Na Lilian Lucas, Morogoro.
Msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rajabu Rutengwe umepata ajali jana saa 9.30 alasiri eneo la Mizambarauni Darajani barabara kuu ya Dar es Salaam-Morogoro.
Katika ajali hiyo, Meya wa Manispaa ya Morogoro, Amiri Juma Nondo amevunjika mkono wa kushoto, pamoja na waandishi na wapigapicha wawili wa Kituo cha ITV, Hussein Nua na Anitha Chali wa Televisheni ya Taifa (TBC) pamoja na dereva wa meya huyo, Ally Mwambara wamejeruhiwa vibaya.
Basi la abiria la Happy Afrika aina ya scania lililokuwa likitokea mkoani Njombe kwenda Dar es Salaam linadaiwa lilitaka kulipita gari lililokuwa limeegeshwa pembeni ya barabara ndipo lilipoligonga gari hilo la Manispaa ya Morogoro aina ya Nissan Patrol.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Meya Nondo alisema wakiwa katika gari lao, aliliona basi likija kwa kasi sana na kutaka kukatiza na kwenda upande wa kulia bila kuangalia mbele ndipo wakagongwa.
“Yule mwenye basi alikuwa anaendesha kwa kasi sana akawa anakuja kwenye gari letu kwa kutaka kukatiza upande wa pili na sisi tukapigwa ubavuni, ndicho nilichokiona,” alisema Nondo.
Msafara huo wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ulikuwa katika ziara tangu asubuhi kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na wakiwa wanakwenda kupata chakula cha mchana ndipo ajali ilipotokea.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Godfrey Mtei alithibitisha kupokea majeruhi wanne na kwamba wanapatiwa matibabu na majeruhi wawili hali zao ni mbaya.
0 comments:
Post a Comment