SIFA YA RAIS AJAYE WA TANZANIA 2015 AWE NA SIFA KUU YA KUMWOGOPA MWENYEZI MUNGU.
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal akimpongeza Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Beatus Kinyaiya baada ya kusimikwa kwenye sherehe iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba mjini Dodoma jana. (Picha na Sifa Lubasi).
MAKAMU wa Rais, Dk Mohamed Ghalib Bilal amesema kigezo kikuu cha Rais ajaye ni kuwa mwenye hofu ya Mungu na Serikali itahakikisha Uchaguzi Mkuu unafanyika kwa misingi ya haki na amani.
Pia ametaka kukemewa kwa wanasiasa wanaotaka kuingia madarakani kwa kutumia migongo ya wanyonge. Alisema hayo jana mjini hapa wakati wa kusimikwa kwa Askofu Beatus Kinyaiya kuwa Askofu wa Jimbo Kuu la Dodoma.
Dk Bilal alisema mwaka huu wa uchaguzi zimekuwa zikiibuka hisia tofauti, hivyo ni wajibu wa viongozi wote wa dini zote kuombea taifa ili wananchi wachague watu watakaoendeleza misingi ya amani, upendo na mshikamano.
“Kiongozi bora ni mwenye hofu ya Mungu,” alisema. Alisema kunatakiwa kukemewa kwa wanasiasa wanaotaka kuingia madarakani kwa kupitia migongo ya wanyonge. Aliwataka viongozi wa dini kuombea wanasiasa waliopotoka ili wasaidie kusaka amani kwa njia yoyote.
Pia alisema Serikali itahakikisha mchakato wote wa uchaguzi mkuu unafanyika kwa misingi ya haki na amani ili Tanzania ipate viongozi wazuri wanaowataka ili wasukume mbele gurudumu la maendeleo.
Makamu wa Rais pia aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano, kwani Mungu ameibariki nchi imekuwa na amani bila watu wake kuwa na ubaguzi wa rangi, kabila na hali za maisha yao.
“Amani si tu ya wanasiasa tunapozungumzia amani kila moja ajue ana wajibu huo,” alisema. Alisema huwezi kuwa na amani bila kumpenda Mungu na kuwataka Watanzania wampende Mungu na kupendana wao kwa wao na kuwataka viongozi wa dini kuomba usiku na mchana ili Watanzania wazidi kumpenda Mungu.
Alitaka waumini wa dini zote kupendana na kuvumiliana kwani wote ni wa Mwenyezi Mungu na hakuna dini bora kuliko dini nyingine ni marufuku na dhambi kubwa kukashifu dini au imani ya mtu mwingine na yeyote aliyefanya hivyo amepotoka. Aidha, alisema ni vizuri kama watu wataishi kwa kuvumiliana.
“Dini zote zinafundisha amani, upendo kusaidiana na kuvumiliana viongozi wa dini watoe mahubiri mema kwa watu wote,” alisema. Pia alipongeza Kanisa Katoliki Tanzania kwa kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha sekta za elimu, afya na maji na kuongeza ustawi wa maendeleo katika maeneo mengi.
Alisema serikali imeridhishwa na mchango wa madhehebu ya dini nchini na itaendelea kuhakikisha mazingira bora yanafikiwa. Akitoa salamu zake, Balozi wa Papa na Mwakilishi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Francisco Padilla aliwataka mapadri na watawa kumpokea Baba Askofu Mkuu Kinyaiya na kumpa ushirikiano.
Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Tarcisius Ngalelakuntwa alimtaka Askofu Mkuu Kinyaiya kuendeleza kazi njema kwa kuhudumia taifa la Mungu kwa upendo na amani.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini, mapadri, mawaziri, Spika wa Bunge, Anne Makinda na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na mkewe Mama Anna Mkapa, wakuu wa wilaya, wabunge na wageni mbalimbali.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment