WABUNGE SASA WAWALIPUA MAWAZIRI, YUMO WAZIRI WA FEDHA NA LAZARO NYALANDU BUNGENI DODOMA.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya akimsikiliza mbunge wa viti maalumu, Ester Bulaya aliyetaka waziri huyo afukuzwe kazi kwa sababu amevunja katiba. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dodoma. Bunge limeendelea kuwa moto kwa viongozi wakati wabunge wakiwalipua mawaziri, huku wakimtaka Waziri wa Fedha, Saada Mkuya kufukuzwa kutokana na kukiuka Katiba na kumrushia bomu Lazaro Nyalandu kuwa anazunguka nje ya nchi na msichana kwa madai ya kutangaza utalii.
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, pia alikumbana na kadhia hiyo wakati alipodaiwa kuwa anahusika kwenye kila mikataba mibomu, jambo lililosababisha mwanasheria huyo mkuu wa zamani kuingilia kati akitaka “kuheshimiana”.
Wabunge walifanya hivyo jana bungeni mjini Dodoma wakati wakichangia taarifa za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ya mwaka ulioishia Juni 30 mwaka 2014.
Mkuya alijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kuonyesha kuwa Serikali ilitumia fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi mengine, kitendo kinachomaanisha kuwa alivunja Katiba.
Akichangia mjadala huo, mbunge wa viti maalumu (CCM), Ester Bulaya alisema Bunge limekuwa likitunga sheria na wao kama viongozi lazima waonyeshe mfano wa kufuata sheria.
“Fedha ambazo ziko kwenye ring fence (mfuko maalumu), hazitakiwi kutumika kwa matumizi mengine kwa mujibu wa sheria. Kwa mujibu wa Katiba, Waziri umevunja Katiba kwa mujibu wa ibara ya 135 na ibara ya 136 ni Tanzania peke yake (Waziri Mkuya) unabaki salama. Hupaswi hata kupewa heshima ya kujiuzulu, unafukuzwa kazi,” alisema Bulaya.
Bulaya, ambaye amekuwa mmoja wa wabunge wachache kutoka chama tawala wanaoihoji Serikali, alisema wizara hiyo imeshindwa kukata fedha kwa ajili ya chai, suti na sambusa na badala yake inakata fedha zilizokuwa ziende kupeleka umeme vijijini.
Alisema fedha hizo zimetengwa ili kuwezesha Watanzania ambao ni masikini kutumia vibatari.
Bulaya alikuwa akizungumzia Sh180.7 bilioni zilizokusanywa kulipia gharama za mradi kutokana na mauzo ya mafuta ili ziweze kupeleka umeme vijijini.
Ripoti inaonyesha kuwa, kati ya fedha hizo, Sh144.2 bilioni ndizo zilizopelekwa kwenye mfuko wa umeme vijijini ikiwa ni pungufu ya Sh36.5 bilioni.
Wakati wa kuhitimisha mjadala wa ripoti hizo, Naibu Waziri wa Fedha (Sera), Mwigulu Nchemba alikiri kuwa wizara iliyumba katika eneo hilo kutokana na hali ya kifedha ya Serikali.
“Mwaka huu ni hapa tu ambako tuliyumba, (katika) eneo hili la matumizi ya fedha za miradi,” alisema Mwigulu na kuongeza kuwa wizara yake inaandaa utaratibu utakaowezesha makosa hayo kutojirudia.
Hata hivyo, alisema mwaka jana wizara ilitoa Sh500 bilioni katika mwezi wa kwanza tangu kupitishwa kwa bajeti, jambo ambalo alisema lilishangaza wengi.
“Kuna baadhi ya watu wamesema miradi mingine ilipata sifuri. Ukweli ni kwamba ile ambayo ilipata sifuri ni kutokana na fedha hizo kutegemewa kutoka kwa nchi wafadhili,” alisema. “Lakini miradi mingi ilipata fedha kwa kuwa tulilipa Sh500 bilioni mwezi wa kwanza baada ya bajeti.”
Alishauri wabunge kumpongeza Waziri Mkuu kwa maeleo kuwa amefanya mengi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa kutaka fedha za miradi zisitolewe hadi wahusika watakapotoa maelezo ya matumizi ya fedha na kwamba amejiondolea hata mamlaka ya kusamehe kodi ili kuwezesha fedha zinazopatikana ziende kwenye miradi ya maendeleo.
Awali, katika mjadala huo, wabunge wengi waliilaumu Wizara ya Fedha kwa kutumia fedha za miradi kwa ajili ya shughuli nyingine na kukopa fedha kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na kutorudiusha.
Walisema vitendo hivyo vinaifanya taasisi hizo kushindwa kujiendesha wakati miradi ya maendeleo ikishindwa kuendelea kutokana na ukosefu wa fedha.
Pamoja na Waziri Nchemba kutoa maelezo ya jinsi miradi hiyo ilivyokwama, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema kuwa siyo kweli kwamba Serikali imechukua hatua na kwamba ahadi ya Waziri Mkuya kuwa ataunda kikosi kazi kwa ajili ya kushughulia matatizo hayo, haitoi matumaini kwa kuwa hiyo itakuwa ya kumi.
“Serikali haina nidhamu ya kulipa,” alisema Zitto na kutoa mfano wa fedha zilizochukuliwa kutoka Bima ya Afya kwa ajili ya kununua magari ya polisi ambazo hazijalipwa hadi leo.
“Magari ya polisi na Bima ya Afya vina uhusiano gani?” alihoji na kuongeza kuwa tabia hiyo inadhoofisha mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo inatoa fedha ambazo ni malipo ya pensheni.
“Hii inafanyika kwa mifuko yote ya NSSF, PSPF na PPF. Deni sasa ni Sh1.8 trilioni na fedha hizi ni za kuwalipa wastaafu… Kuna mfuko mmoja ambao technically (kitaalamu) ni bankrupt ( umefilisika).”
Pia, alisema wakati wa kuidhinisha fedha za mradi wa vitambulisho, Bunge liliidhinisha Sh52 bilioni. Lakini Bunge lilipomaliza vikao, Serikali ikaenda kuzikopa.
Utoro wa mawaziri
Mapema jana asubuhi wakati Bulaya akiongea hayo, kulikuwa na mawaziri wasiozidi tisa, kati yao wanne wakiwa manaibu.
Waliokuwapo bungeni ni Mhagama, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Binilith Mahenge, Waziri wa Uwezeshaji na Uwekezaji, Christopher Chiza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani.
Mawaziri wengine ni Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Dk Mary Nagu na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia.
Manaibu alikuwa ni Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi.
Hali akijua hayo, Bulaya alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama kugeuka na kuangalia idadi ya mawaziri ambao wapo bungeni.
Baadaye aliendelea kusema kuwa wabunge wamekuwa wakiongea mambo mazuri kama hayo, lakini mawaziri hawako bungeni na badala wanakuwapo wachache.
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alisema inasikitisha kwamba hata wanamitindo sasa wanaanza kufikiria kuwa marais.
Alisema hali hiyo inasababishwa na wanavyokaa katika Baraza la Mawaziri, akieleza kuwa mawazo yao mawaziri hayaonyeshi ubunifu wa kubadilisha nchi.
Lema alisema ndiyo maana Serikali imeshindwa kuwekeza katika miradi ya maji ambayo ingeweza kuleta fedha nchini.
Alisema Serikali imeshindwa pia kupata Sh20 bilioni kwa ajili ya kufufua kiwanda cha kutengeneza matairi cha General Tyre kilichopo mjini Arusha.
“Mara nyingi hii husababishwa na tabia ya mawaziri ambao mnapokutana kwenye vikao vyenu, mara nyingi mnakwenda kutafuta group picture (picha za pamoja) badala ya kushauri namna gani ya kupeleka nchi hii mbele,” alisema mbunge huyo machachari.
“Ndiyo maana mnashinda kwenye (mitandao wa kijamii ya) instagram, facebook na Jamii Forums… mnapiga picha za kung’aa kwa sababu katika vikao vyenu vya kufanya uamuzi, mnajadili mambo ambayo hayana kina cha mawazo. Ndiyo maana nchi hii inakufa.”
Alisema viongozi wengi wanakosa ubunifu wa kuiendeza nchi hii.
“Angalia Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alikwenda kutangaza utalii nje ya nchi akiwa ameongozana na (mwigizaji maarufu wa filamu wa Tanzania) Anti Ezekiel,” alisema na kuongeza kuwa waziri huyo hashindi ofisini kwa kisingizio cha kutangaza utalii.
Alisema mbuga za wanyama zipo nchini, lakini waziri huyo amekuwa akishinda Ulaya na kuongeza kuwa sekta ya utalii ingetengenezewa mikakati, ingeweza kuendesha nchi.
Chagonja atuhumiwa
Lema alisema hata juzi wakati Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe anashambuliwa na wabunge kuhusu kilichodaiwa unyanyasaji wa polisi, alimfuata, akamweleza kuwa tatizo siyo yeye bali ni nchi imekuwa kama gheto.
“Leo Jeshi la Polisi, leo (Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul) Chagonja haamini kama Rais ameshafanya Uteuzi wa IGP. Jeshi la Polisi limepasuka ma-RPC (makamanda wa polisi wa mikoa) wanalalamika. Chagonja haamini kama Rais ameshafanya uteuzi,” alisema.
“Kwa hiyo anafanya sabotage (hujuma). Hata hizi bunduki zinazoibwa inaweza kuwa ni mkakati wa Chagonja kumhujumu IGP. Chikawe anajua, watu wote wanajua lakini kila mtu anasema polepole hii nchi kama gheto (neno linalotumika kumaanisha nyumba ya mabachela) hujui Serikali ipo wapi.”
Mvutano wa Lissu na Mwanasheria Mkuu
Katika sakata jingine bungeni jana asubuhi, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema katika sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow watu walioshtakiwa hadi sasa ni wale wenye nyadhifa ndogo.
Alisema kuwa watu wamechukua mabilioni ya fedha, lakini waliochukuliwa hatua katika sakata hilo ni wale waliopatiwa Sh80 milioni.
Alisema Bunge lilipendekeza majaji waliotajwa katika sakata hilo wachukuliwe hatua, lakini hadi leo bado hawajachukuliwa hatua. Alisema Rais Jakaya Kikwete anasema hatua za kuwachukulia majaji hao zianzie mahakamani.
“Huyu Rais anashauriwa na nani? Katiba yetu inasema wazi kabisa ibara 113 na 120A2 kuwa Rais atakuwa na mamlaka ya nidhamu kwa majaji, huyu anayesema mamlaka ya nidhamu hayaanzii kwake ni nani?”alihoji.
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alimkatisha kwa kumpa taarifa kuwa suala hilo lilitolewa mwongozo na Spika kuwa hoja ikitolewa bungeni haiwezi kurejea tena bungeni hadi baada ya miezi 12.
Hata hivyo, suala hilo linaweza kurejea tena bungeni kama hoja mahususi. “Lakini pia Serikali ilete taarifa ya utekelezaji kabla ya Bunge la bajeti ambalo halijafika,” alisema.
Alisema kanuni haziruhusu kumhusisha Rais na ujengaji wa hoja kwa namna ya kejeli.
Akiendelea na hoja zake, Lissu aliendelea kusema amepata taarifa ya ‘mrithi’ wa Jaji Fredrick Werema. Hali iliyomfanya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, kuingilia kati na kumtaka Lissu kutotaja mambo ya urithi.
Hata hivyo, Lissu alisema hoja yake ya msingi Taifa linaharibiwa na ukosefu wa uwajibikaji.
Alisema wanaotakiwa kuadhibiwa na Rais hawaadhibu na kwamba hoja yake siyo kumkejeli Rais.
Alisema imeonekana katika kamati kuwa majaji wamechukua rushwa, lakini Rais amekuwa akikimbia na kushindwa kutimiza wajibu wake kikatiba.
Hali hiyo, ilimfanya Masaju kuomba tena taarifa na kusema:
“Ibara ya 112 inaunda Tume ya Utumishi wa Mahakama 113 inaeleza majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama… Moja wapo majukumu ni kumshauri Rais kuhusu nidhamu ya majaji, hivyo Rais hawezi kuchukua hatua bila kupata ushauri huo,” alisema.
Alisema Rais hawezi kuchukua hatua bila tume ya utumishi kulifanyia kazi na kisha kumpelekea Rais mapendekezo ambayo ndiyo yatafanyiwa uamuzi.
Mgawo wa Zanzibar waingizwa
Habibu Mnyaa (Mkanyageni-CUF), alilamikia tatizo la fedha za mafuta wanazokatwa pande zote kushindwa kwenda upande wa Zanzibar.
“Nahitaji majibu ya waziri ni kwanini mpaka sasa hata shilingi moja haijapelekwa huko…Tukilalamika mnasema Wazanzibari ni wakorofi. Hii ndiyo hali inayotufanya tuone uonevu wa misingi ya serikali tatu na kutoona umuhimu wa muungano,”alisema.
Kamati ya Uongozi
Kamati ya Uongozi ya Bunge imeamua kuwa kuanzia sasa halitajadili jambo lolote lililo mahakamani kama ilivyokuwa awali.
Msimamo huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu baada ya kikao cha Kamati ya Uongozi kilichokaa kujadili jambo hilo.
Zungu alitoa tamko hilo baada ya jana asubuhi mbunge wa viti maalumu, Suzan Lyimo kuomba mwongozo wa kwa nini suala la Uda linakatazwa kujadiliwa wakati lipo kwenye ripoti za kamati.
Juzi, Spika Anne Makinda pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju kuzuia kujadiliwa suala la Uda kutokana na kuwapo kwa kesi mbili mahakamani.
Jana baada ya kikao cha Kamati ya Uongozi, Zungu alisema: “Tumekubaliana kwamba suala lolote ambalo lipo mahakamani halitajadiliwa hapa bungeni kipindi hiki,” alisema Zungu na kuongeza: “Tusiingilie kabisa jambo hilo na huo ndiyo mwongozo kuhusu ombi la Suzan Lyimo.”MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment