Mlangila anadaiwa kushambuliwa kwa kipigo na askari hao muda mfupi baada ya baba yake mzazi, Bigamanywa Mlangila, kumfikisha kituoni hapo kwa tuhuma za kuvunja dirisha la nyumba yake.
Mbali na mwenyekiti wa kijiji cha Nkome kilichopo Kata ya Bugando, Angelo Daniel, kuthibitisha kutokea kwa kushambuliwa kwa kipigo hicho usiku wa Desemba 19, mwaka jana, alisema alipelekwa kituoni hapo akiwa na afya njema.
Alisema siku iliyofuata, aliamka akiwa hoi kutokana na kinachodaiwa kupewa kipigo na askari hao walioshirikiana na mgambo aliyekuwa zamu kituoni hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, amethibitisha maiti ya Mlangila kutekelezwa kwenye mbele ya kituo hicho na kuahidi kufuatilia, kisha kutoa taarifa kamili za tukio hilo.
Hata hivyo, Kamanda Konyo hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa undani zaidi, akisema alikuwa akiekelea kwenye tukio la wachimbaji kufukiwa na kifusi kwenye mgodi wa dhahabu katika kijiji cha Nyarugusu.
Baadaye Kamanda huyo akizungumza na NIPASHE, alisema Mlangila alipigana na mgambo kwenye kituo hicho cha polisi ambaye inadaiwa alikwenda kumkamata baada ya baba yake kuripoti tuhuma dhidi yake.
Alisema hata hivyo alizidiwa nguvu na mgambo huyo.
Kwa mujibu wa Konyo, mgambo huyo anashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
Akizungumzia tukio hilo, kaka wa marehemu, Galidi Lukanazya (35), alidai mdogo wake aliuawa baada ya kupigwa na askari wawili wa kituo hicho kwa virungu na mateke sehemu mbalimbali za mwili wake. (Majina ya askari hao na mgambo huyo kwa sasa tunayahifadhi).
Alidai kipigo kwa mdogo wake kilianza baada ya kuondoka kwa mkuu wa kituo hicho, Gwaga Mtawa, saa mbili za usiku kwenda kutazama taarifa ya habari kwenye moja ya ukumbi uliopo kijijini hapo.
“Sababu za baba kumpeleka kituoni hapo ilitokana na kuvunja dirisha la nyumba...ni baada ya kukuta baba akiwa ameweka mpangaji kwenye chumba alichokuwa akilala Mlangila...alipouliza sababu za kuingiza mpangaji kwenye chumba hicho baba, alisema nyumba hiyo ni mali yake...ndipo Mlangila akazunguka nyuma ya nyumba na kuanza kuvunja dirisha,” alisema.
“Baada ya kuona hali imekuwa hivyo, baba aliamua kutoa taarifa kituo cha polisi, askari walifika kisha wakamkamata na kumpeleka selo...lakini wakiwa njiani Mlangila alionekana kulalamika kuwa anaonewa na ndipo wakaanza kurushiana maneno hadharani,” alisema.
"Binafsi ninachokiamini waliamua kumtembezea kipigo baada ya kuhisi amewadharau wakati wakimpeleka kituoni...na walitambua kwa kuwa
wameshamfikisha mahali hapo wana uhuru wa kufanya wanavyojisikia...ndipo wakamjeruhi na baadaye kumpeleka kwenye zahanati ya Nkome kabla ya kumhamishia kwenye kituo cha afya cha Nzera na baadaye Hospitali ya Wilaya ya Geita.
Habari zinadai kuwa baada ya kipigo hicho, Mlangila alizirai huku akitokwa damu puani na masikio na ndipo askari hao waliposhtuka na kuamua kumkimbiza zahanati ya kijiji hicho na hali ilipoonyesha kuwa mbaya, alihamishiwa kwenye kituo cha afya cha Nzera.
Desemba 24, mwaka jana alihamishiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Geita na Desemba 31 walimpeleka tena hospitali ya Misheni ya Sengerema, mkoani Mwanza kwa matibabu zaidi.
Imedaiwa kuwa Januari 4, mwaka huu hali yake iliendelea kuwa mbaya na ndipo walipomhamisha tena na kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza kabla ya kukumbwa na mauti Januari 9, mwaka huu.
Baada ya maiti yake kuwasili jana nyumbani kwao kwa maziko, baadhi ya ndugu jamaa na marafiki walipinga kuendelea na huduma hiyo na kudai yanapaswa kufanywa na polisi na mgambo waliosababisha kifo chake.
Kutokana na hali hiyo, kundi wanakijiji hao, walibeba maiti hiyo isha kuitelekeza mbele ya kituo hicho wakiwa wameifunika sanda nyeupe huku baba wa marehemu huyo akitiwa mbaroni kwa tuhuma za kuhusika na kifo hicho.
Habari zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni jana usiku, zilieleza kuwa Ofisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Geita, John Maro, alikuwa kwenye eneo la tukio kuwasihi ndugu na jamaa wa marehemu wakubali kuchukua maiti kwa maziko huku jeshi hilo likiendelea na hatua nyingine za kusheria.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment