Baada ya kuuzima moto huo, kazi iliyobakia ni kuitoa miili ya marehemu katika gari hilo.
Juma Mtanda, Morogoro.
Ajali hiyo iliyotokea jana majira ya saa 11:30 alfajiri na waliofariki katika ajali hiyo ni dereva wa lori hilo Ahmed Diliya (55), utingo wa lori hilo David Omela maarufu kama Jaruo na mtu mwingine aliyefahamika kwa jina la Mohamed Ally (35) wote wakazi wa Jijini Dar es Salaam.
Baada ya lori hilo kuanguka lilianza kutoa moshi na baadaye kuwaka moto hali iliyosababisha barabara kuu ya Morogoro-Dar es Salaam kushindwa kupitika kwa zaidia ya masaa mawili.
Akizungumza eneo la tukio Mkaguzi msaidizi wa jeshi la Zimamoto mkoa wa Morogoro, Hamad Dadi alieleza kuwa askari wa kikosi cha zimamoto kiliwasili mapema eneo hilo na kufanya jitihada za kuuzima moto huo lakini baadaye waligundua kuwepo kwa watu ambao walikandamizwa na roli hilo.
Dadi aliongeza kuwa baada ya kazi ya kuzima moto na kunyanyua tenki ilifuata kazi ya kunyanyua kichwa cha gari kisha miili ya watu hao kuonekana huku wakiwa wamekandamizwa na kuungua moto.
Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo akiwemo Afisa Mtendaji wa kijiji hicho cha Maseyu Juma Kipile alisema kuwa alisikia kishindo kikubwa na kufuatilia na moshi mkubwa hata hivyo wananchi walishindwa kutoa msaada kutokana na kutanda kwa moshi na moto mkali.
“Baada ya ajali hiyo nilitoa taarifa kwa jeshi la polisi ambao walifika eneo la tukio na kuomba msaada kituo cha zimamoto Morogoro ili kuzima moto huo.”alisema Kipile.
Kamanda wa Polisi mkaoni Morogoro Leonard Paulo alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa lori hilo lenye namba za usajili T593 CDC lililokuwa na tela namba T259 CQM aina ya Scania lilikuwa limebena mafuta yenye ujazo wa lita 37,000 mali ya Petro Africa Company na kwamba gari hilo linamilikiwa na Waseme Express Logistics mkazi wa jijini Dar.
Kamanda paulo alisema kuwa jeshi la Polisi liliwahi kufika eneo la tukio na kufanikisha kuimarisha ulinzi kwa kuwazuia watu kufika jirani na eneo la tukio ili kuepuka madhara ambayo yangeweza kutokea kutokana na jali hiyo.
0 comments:
Post a Comment