BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

PRESHA YA SIMBA SC YATULIA ?.


Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi (kulia) akiwania mpira na beki wa JKT Ruvu, Ramadhan Shamte wakati wa mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana. Simba Ilishinda 2-1. Picha na Said Khamis.
 

Simba imewapoza roho mashabiki wake waliokuwa na hasira baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2- 1 dhidi ya JKT Ruvu katika mchezo mkali wa Ligi Kuu Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Mganda, Danny Sserunkuma ndiye aliyeibuka shujaa wao kwenye mchezo huo baada ya kuifungia timu yake mabao mawili na kukata maneno ya mashabiki waliokuwa wakimbeza wakimwita mzigo.


Kwa matokeo hayo, Simba imepanda hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 16, nyuma ya Coastal Union yenye pointi 17 na Polisi Moro ambayo ina pointi 18 sawa na JKT Ruvu.


JKT Ruvu imeshuka kwa nafasi moja hadi ya nne ikiipisha Mtibwa Sugar ya Morogoro ambayo ina pointi 18, lakini timu hizo zinazidiana mabao.


Sserunkuma aliwainua mashabiki mapema, dakika ya kwanza ya mchezo huo baada ya kufunga bao safi la kiufundi kwa kuubetua mpira wakati akikabwa na mabeki wa JKT Ruvu baada ya kupokea pasi ya kupenyezewa ya ‘nduguye,’ Emmanuel Okwi.


Hata hivyo, bao hilo halikudumu kwani JKT Ruvu walisawazisha dakika ya 18 kupitia kwa nahodha wao, George Minja aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Jabir Aziz.


Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu hizo zilikuwa sare ya bao 1- 1 na kusababisha mashabiki wa Simba kushikwa na hasira na kuanza kuwatukana viongozi wa juu wa klabu hiyo waliokuwa wamejazana kwenye jukwaa kuu.


Hata hivyo, timu hizo ziliporudi kipindi cha pili wachezaji wa Simba walionekana kuchangamka na kupata bao la pili kupitia kwa Sserunkuma, aliyefunga kwa kichwa akipokea pasi ya Okwi aliyekuwa mwiba mkali kwa JKT Ruvu.


Simba iliingia mchezoni ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 2- 1 kutoka kwa Mbeya City, Jumatano iliyopita kilichochafua hali ya hewa ndani ya klabu hiyo na kusababisha kocha msaidizi, Seleman Matola atangaze kujiuzulu nafasi yake baada ya kupata shinikizo kutoka kwa mashabiki na baadhi ya wachezaji.


Jana, Matola alionekana kwenye benchi la ufundi, kuiongoza timu kuingia uwanjani pia akieleza jinsi timu itakavyocheza.


Mbali na sinema hiyo ya Matola kurejea kibaruani kiaina, mechi hiyo ilianza kwa kasi na Simba kuonekana wamepania kuibuka na ushindi.


Dakika ya sita, kiungo wao, Abdi Banda alimchezea rafu Nashon Naftal wa JKT Ruvu na kumwondoa mchezoni kutokana na maumivu na nafasi yake kuchukuliwa na Amos Mgisa.

Dakika ya saba, Jabir Aziz wa JKT Ruvu aliachia shuti kali lililookolewa na beki wa kati wa Simba, Hassan Isihaka na kuwa kona hata hivyo Ally Billali alipiga kona hiyo na kuokolewa na mabeki wa Simba.


JKT Ruvu, wamekosa nafasi adimu ya kukalia kiti cha uongozi wa ligi hiyo kwa pointi 21 kama wangeshinda, walilishambulia lango la Simba wakitafuta bao la kusawazisha na dakika ya nane, mshambuliaji wao hatari, Samuel Kamuntu alipiga shuti hafifu lililodakwa na kipa Ivo Mapunda.


Simba walijibu mapigo dakika ya 33 baada ya Ibrahim Ajib kuangushwa nje kidogo ya 18 na mwamuzi Hashim Abdallah kuamuru iwe faulo, hata hivyo mchezaji huyo aliipiga na kudakwa na kipa wa JKT Ruvu, Benjamin Haule.


Pia, dakika ya 42 nusura Simba ipate bao baada ya wachezaji wake kupasiana vizuri ambako Sserunkuma alimpasia Ajib ambaye naye alimpa pasi Jonas Mkude aliyeachia shuti lililookolewa na beki wa JKT Ruvu, Renatus Morris.


Kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Polisi Moro imeibamiza Mbeya City bao 1- 0. Bao hilo lilifungwa na Said Bahanunzi anayeichezea kwa mkopo akitokea Yanga.


Nako kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, wenyeji Coastal Union walitoka suluhu 0-0 na Mtibwa Sugar, timu ambayo kama JKT Ruvu ilikuwa na nafasi za kuzikaribia Azam, Yanga zilizoko juu yao kwenye msimamo.


Kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Prisons imelazimishwa sare ya bao 1- 1 dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba.


Kagera Sugar ndio walioanza kupata bao lililofungwa na Rashid Mandawa, dakika ya 20, lakini Prisons walisawazisha dakika ya 64 kupitia kwa Nurdin Chona.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: