TOTO AFRICA FC, MAJIMAJI ZAPATA POINTI ZA CHEE LIGI DARAJA LA KWANZA TANZANIA BARA, VURUGU ZAWANUFAISHA.
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imethibitisha ushindi wa pointi na mabao matatu kwa timu za Majimaji na Toto Africans baada ya mechi zao za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuvurugika kutokana na sababu mbalimbali.
Toto Africans imepewa ushindi huo kwa mujibu wa Kanuni ya 41(3) ya FDL baada ya vurugu za washabiki wa Geita Gold kusababisha mechi hiyo iliyochezwa Februari 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita kuvunjika dakika ya 12.
Pia Kamati hiyo iliyokutana Dar es Salaam jana (Februari 12 mwaka huu) imezuia mechi za FDL kuchezwa kwenye uwanja huo ambao hauna uzio wa kutenganisha wachezaji na washabiki kwa sababu za kiusalama.
Naye mchezaji Venance Joseph wa Geita Gold ambaye alimpiga kichwa refa akipinga adhabu ya penalti iliyotolewa dhidi ya timu yake kwenye mechi hiyo amesimamishwa wakati akisubiri kosa lake kusikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Malalamiko ya Friends Rangers kwenye mechi dhidi ya Majimaji yametupwa na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kusababisha mchezo huo uliochezwa Januari 29 mwaka huu Uwanja wa Majimaji mjini Songea kuvunjika dakika ya 39. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 28(4) ya FDL.
Friends Rangers imepoteza mechi hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 28(1) ya FDL, Majimaji kama ilivyo Toto Africans imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu.
Naye Kocha wa Friends Rangers, Herry Chibakasa (Mzozo) suala lake limepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF ili aweze kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni ya 39(8) ya FDL kwa kuhamamisha vurugu kwenye mechi dhidi ya Majimaji.
Mwamuzi John Mafuru wa Mbeya aliyechezesha mechi ya Majimaji na Friends Rangers amefungiwa miezi 12 (kumi na mbili) kwa kutozingatia sheria kiasi cha kuvuruga mchezo. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 37(1) ya FDL.
Pia Kamishna wa mechi hiyo Kim Rajab wa Dodoma amefungiwa miezi 12 (kumi na mbili) kwa mujibu wa Kanuni ya 38(1) ya FDL kwa kutoa taarifa zisizo sahihi.
Lipuli ya Iringa imepewa ushindi wa mabao matatu na pointi tatu baada ya timu ya KMC (Tessema) kumchezesha mchezaji Morris Paulo Katumbo aliyekuwa na kadi tatu za njano kinyume na Kanuni ya 41(12) ya FDL. Katumbo ambaye alipata kadi hizo kwenye mechi namba 85, 100 na 112 alicheza mchezo huo uliomalizika kwa timu ya KMC kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
0 comments:
Post a Comment