USICHOKIJUA JUU YA ‘SERIKALI’ YA WAENDESHA PIKIPIKI TANZANIA
Waendesha bodaboda wakiwa kwenye kituo chao wakisubiri abiria, huku wengine wakiwa tayari wamepata abiria wakianza safari. Picha ya Maktaba.
Waendesha bodaboda sasa wanaweza kufananishwa na ‘serikali’ inayojitegemea au taasisi ya kipekee kutokana na kuunda umoja katika ulinzi na usalama, biashara, vizazi na hata katika vifo na magonjwa.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa hivi sasa waendesha bodaboda wana utawala wao, unaowaongoza katika maeneo mbalimbali.
Inapotokea ajali kati ya dereva wa gari na mwendesha bodaboda baada ya dakika chache, kundi la waendesha bodaboda litafika na kuanza kumwadhibu dereva wa gari. Imebainika kuwa umoja huu unatokana na waendesha bodaboda kuwa na imani kuwa wanagongwa kwa makusudi au pengine ni njama za kuwaua na kuwakomoa.
Mara kadhaa waendesha bodaboda wameonekana wakiandamana pale inapotokea mwenzao amegongwa na gari, kuibiwa pikipiki au kufanyiwa jambo lolote lile.
Hata hivyo Mwananchi lilienda ndani zaidi na kuichunguza taasisi hii isiyo rasmi ya umoja wa waendesha bodaboda na kubaini wana watu wanaoitwa ‘polisi’.
‘Polisi’ wa bodaboda
Katika vituo vingi vya bodaboda, Mwananchi liligundua kuwa licha ya kuwa na uongozi kwa mfano Mwenyekiti, na Katibu, lakini kuna polisi wa kituo.
Huyu anahusika na shughuli za ulinzi na usalama. Kwa mfano ikitokea dereva mwenzao kagongwa ‘polisi’ atakuwa wa kwanza kuchukua hatua, kuwakusanya wenzake kwa kuwapigia simu na kuanzisha mashambulizi.
“Polisi kazi yake kuangalia kuwa mwenzetu yupo salama, wakati mwingine mwenzako anakodiwa halafu hajarudi mpaka jioni lazima umpigie simu,” alisema Mwenyekiti wa waendesha bodaboda wa Kimanga, Said Kuleka.
Kuleka alisema ‘Polisi’ katika vituo vya bodaboda husaidia pia kudhibiti wizi na mauaji ya madereva hao.
Waendesha bodaboda hao wanasema wanatengeneza uongozi wao kwa kuwa Jeshi la Polisi halina usimamizi zaidi ya kuwakamata pindi wanapofanya makosa na kuchukua fedha.
Kwa mujibu wa Kondo H. Kondo mwendesha bodaboda wa kituo cha Ubungo Mataa, alisema ‘polisi’ wa kituo wana kazi ya kuhakiki usalama wa madereva wote. Kazi yake kubwa ni kuangalia kama amegonjwa kwa makusudi basi atahakikisha aliyegonga anakiona cha mtema kuni.
“Kumbuka kuna wizi wa pikipiki, mwenzako anachukuliwa hapa na mteja, kesho unaambiwa amekamatwa Mabwepande amekufa na pikipiki hana. Mimi kazi yangu kujua wapi mwenzetu amekwenda na ameenda na nani na kama amerudi,” alisema Kondo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alisema atazungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Ernest Mangu (IGP) ili walifanyie utatuzi suala hilo ikiwezakana waanze kuchunguza matukio ya uhalifu na uvamizi yanayofanywa na kundi hilo.
“Sasa hivi nitazungumza na IGP ili ajue jinsi kikosi chake kinavyoweza kulifanyia kazi hili tatizo, hii ni hatari sana kwa wakati huu. Si sahihi kwa watu kujichukulia sheria mkononi na kujiundia mamlaka yao kama wanavyofanya,”alisema.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu(SUMATRA), David Mziray alisema mamlaka hiyo ilitengeneza sheria zinazoonyesha jinsi madereva hao wanavyofanya kazi kwa mfano alieleza wanatakiwa kuwa na vituo maalumu, wawe na chama na wasimamiwe na halmashauri.
“ Hatutoi leseni kwa mwendesha bodaboda anayekuja peke yake, mpaka awe na chama kwa sababu inakuwa rahisi kumfahamu iwapo kuna chama kinachomwakilisha,” alisema.
Alisema mwongozo huo wa waendesha bodaboda unafafanua rangi ya pikipiki, namba na eneo rasmi chombo hicho kunapotakiwa kufanya kazi.
Kuhusu bodaboda kuchukua sheria mkononi Mziray alisema Jeshi la Polisi linatakiwa kufanya kazi yake kuhakikisha inaweka sawa matukio hayo.
Utawala wa bodaboda unafafanuliwa na Feisal Mushi ambaye eneo lake la kazi ni katika soko la Buguruni . Mushi alisema suala la kujenga umoja wa waendesha bodaboda limesababishwa na manyanyaso wanayoyapata kutoka kwa madereva wa magari.
“Wanatugonga makusudi, ndiyo maana ikitokea mwenzetu kagongwa lazima wote twende tukaangalie ajali ilikuwaje. Tukikuta kaonewa tunamuadhibu dereva wa gari sisi wenyewe,” alisema Mushi.
Kisa cha Geita
Kwa mfano tukio lililotokea Desemba 30 mwaka jana huko Geita ambapo waendesha bodaboda waliharibu mali na kumpiga mkazi wa eneo hilo, kwa madai kuwa anahusika na mauaji ya wenzao zaidi ya 30 na wizi wa pikipiki. Tukio hilo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Joseph Konyo.
Kisa cha Mtwara
Umoja mwingine usio rasmi wa usafiri huu unadhihirishwa na tukio la Wilayani Masasi, Mtwara ambapo waendesha bodaboda wameanza tabia ya kuwavamia madereva wa mabasi ya abiria na daladala pindi inapotokea ajali. Hali hiyo imesababisha madereva wa magari kutembea na mapanga au silaha yoyote ili kujihami.
Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani, Masasi, Nicodem Mwaipasi alisema kikosi chake kinafahamu matukio hayo na kuahidi kuyafanyia kazi.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema anafahamu shughuli mbalimbali zinazofanywa na waendesha bodaboda na kueleza kuwa tayari baadhi wameshakamatwa.
“Wanafanya matukio mengi tu kama hayo, wengine wanaua kabisa, wanashambulia na kujeruhi lakini kama unavyojua wao wanasema wanajitetea, lakini kujitetea si kuchukua sheria mkononi,”alisema Kamanda Kova.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga alisema katika kipindi cha kuanzia Januari 2012 hadi kufikia Mei 2013, idadi ya pikipiki zilizosajiliwa nchi nzima zilikuwa 10,036.
Ilielezwa kuwa mikoa inayoongoza kwa wingi wa pikipiki ni Dar es Salaam yenye pikipiki 4,432, ambapo Wilaya ya Kinondoni ni 1,735, Temeke 1,363 na Ilala 1,334. Mikoa inayofuatia kwa idadi kubwa ya pikipiki ni Morogoro 811, Arusha 644 na Kilimanjaro 479.
Madai ya kunyanyaswa
Idadi kubwa ya madereva hao walisema kuwa wananyanyaswa na madereva wa daladala na mabasi mengine ya abiria.
“Unajua wamepanga njama, sasa hivi wanatutafutia sababu, wakati mwingine utawasikia…mgonge, mgonge au nitakugonga. Sasa si makusudi hiyo,”alisema Must Mukasi, mwendesha bodaboda, kituo cha Tabata Reli.
Hata hivyo, dereva wa daladala, Hussein Mnzeru, alisema kinachosababisha waendesha bodaboda kupata ajali ni uendeshaji mbovu na kutothamini sheria za barabara.
“Ingekuwa wanafuata sheria wasingepata ajali kiasi hiki. Hakuna anayewagonga kwa makusudi zaidi ya wao kuendesha vibaya, mbona daladala hakuna ajali kila mara kama wao,”alihoji Mnzeru.
Kufa na kuzikana
Utawala huo wa bodaboda umejidhihirisha pia katika eneo la stendi ya mabasi ya Kimanga, Tabata. Hapa kuna chama cha Uwapiki, yaani Umoja wa Waendesha Pikipiki Kimanga.
Hawa wanasaidiana kwa kila hali, ikiwemo kutoa adhabu kwa madereva wanaodaiwa kuwagonga kwa makusudi. Kwa mfano ukitokea msiba wanachangishana fedha na kusafirisha mwili wa marehemu, pia wana chama cha kukopa na kuweka au Vicoba.
“Alikufa juzi mwenzetu mmoja anaitwa jina maarufu Sharobaro, hatukufanya kazi, tulipita nyumba kwa nyumba kuchangisha fedha za kusafirisha mwili kwenda Moshi,” alisema Emmanuel Mwita, mwendesha bodaboda wa eneo la Tabata Mawenzi.
Madereva hao walisema umoja wa kufa na kuzikana unawasaidia kujenga ushirikiano kijamii.
Katika tukio jingine la kushangaza, Januari 13 waendesha bodaboda, mkoani Mbeya, eneo la Uyole, Njia Panda, waliupora mwili wa dereva mwenzao, Gabriel Ngalele wakati akifanyiwa misa kanisani na kuamua kuizika wenyewe baada ya kuchoshwa na ibada ndefu ya mchungaji
Kundi la vijana 60, walipora mwili wa marehemu Gabriel Ngalele ukiwa unaombewa kwenye Kanisa la Tanzania Assemblies Of God (TAG) eneo la Uyole jijini baada ya kuchoshwa na ibada ndefu ya mchungaji.
Ibada hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Mchungaji, Edward Mtweve wa kanisa hilo ambaye alijikuta kwenye mazingira magumu baada ya vijana hao wanaodaiwa kuwa ni waendesha bodaboda kuvamia madhabahu na kubeba sanduku lililokuwa na mwili wa marehemu.
Baada ya kuuchukua mwili, vijana hao walikwenda kwenye makaburi kuuzika. Mwendesha pikipiki aliyetajwa kwa jina la Bahati Mwasote alilazimika kuendesha ibada ya mazishi.MWANANCHI....Inaendelea kesho.......
0 comments:
Post a Comment