BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CCM YAPATA PIGO KUBWA KIFO CHA KAPTENI KOMBA, NANI ATAIMBA KAMA KOMBA ?.


JOHN DAMIANO KOMBA 1954 Alizaliwa 1963-70 Shule ya Msingi Lituhi 1971-74 Shule ya Wavulana Songea 1975-76 Chuo cha Ualimu Kleruu 1988-90 Chuo cha Magdeburg path 1978-79 Chuo cha Kijeshi Monduli 1978-92 Ofisa wa JWTZ 2006-08 Chuo Kikuu cha Washington 2005-15 Mbunge Mbinga Magharibi.


Mbunge wa Mbinga Magharibi na mkurugenzi wa kundi la uhamasishaji la CCM, Tanzania One Theatre (TOT), Kapteni mstaafu John Komba (61), amefariki dunia jana.


Akithibitisha kifo hicho Dk Elisha Ishan alisema; “Nilimpokea na kuanza kumpima shinikizo la damu na vipimo vingine lakini tayari vilikuwa havifanyi kazi na hapo ndipo tukathibitisha kuwa ndugu yetu ameaga dunia.”


Dk Ishan wa Hospitali ya TMJ alisema kuwa, Kapteni Komba alifikishwa hospitalini hapo saa 10:00 jioni akiwa amebebwa katika machela.


Dk Ishan alisema hawezi kujua kilichomuua lakini akaongeza alikuwa na tatizo la shinikizo la damu na hivi karibuni alikwenda kwenye kiliniki yake.


“Kwa kifupi ni hayo na kwa sasa mwili wake umepelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo.”


Akizungumzia msiba huo, Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel alisema Komba aliyekuwa nyumbani kwake Tangi Bovu jijini Dar es Salaam alianza kujisikia vibaya kutokana sukari yake kuwa juu wakati huo huo presha yake nayo ilikuwa imepanda, hivyo walimpeleka Hospitali ya TMJ iliyopo Upanga kwa matibabu.


Alisema kwa sasa mwili wa mbunge huyo ambaye ni kada wa maarufu wa CCM umehifadhiwa Hospitali ya Lugalo na kwamba taratibu za mazishi zinaendelea nyumbani kwake.


Nape amzungumzia


Awali Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye alisema kuwa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho imepokea kwa mshituko taarifa ya kifo hicho iliyotokea ghafla.


“Pengo lake ni vigumu kuzibika nikinukuu maneno ya Mwenyekiti wa chama chetu Taifa, Jakaya Kikwete; “ Chama kimepata pigo kubwa ukizingatia kwamba alikuwa kada na mhamasishaji mkubwa wa chama na kwamba atabaki kuwa historia iliyotukuka.”


Mtoto wake asimulia


Mtoto wa marehemu, Claudia alisimulia kifo cha baba yake kuwa: “Baba alianza kujihisi vibaya wiki iliyopita na walimpeleka Hospitali ya Sanital, Mikocheni na alionekana shinikizo la damu na sukari vipo juu.”


Alisema hali ilibadilika baadaye (leo) jana na walipokuwa wanamuwahisha hospitali, alikuwa akipiga kwikwi na alipofika hospitali alipopimwa alikuwa ameshafariki dunia.


Claudia alisema kuwa Februari 26 alifanya sherehe ya kuzaliwa na baba yao aliwaita pamoja na kuwaambia wapendane. “Siku hiyo baba alituambia wanangu mpendane… akanipa zawadi ya laptop,” alisema.


Nyumbani


Nyumbani kwa marehemu, waombolezaji walianza kumiminika jioni na wengi baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu ya CCM jana.


Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana alikuwa mmoja wa waombolezaji waliofika nyumbani kwa marehemu kuhani msiba huo.


CCM Zanzibar wamlilia


Viongozi wa Serikali na wanasiasa Zanzibar wamesema CCM kimepata pigo kwa kupoteza nguzo yake ya kisiasa kufuatia kifo cha Komba aliyefariki wakati chama hicho kikiwa katika matayarisho ya kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu.


Waziri wa Fedha Zanzibar, Omary Yussuf Mzee alisema Komba alikuwa mtu wa watu kiongozi anayejiamini akijua kazi yake na ameacha pengo kubwa kwa CCM wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.


Wasanii wamlilia


Kiongozi wa TOT na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Khadija Kopa akimuelezea marehemu, alisema: “Alikuwa kiongozi, alionyesha njia lakini sasa ametoweka.


“Alitushikia mshumaa, aliwasha taa mbele ya safari, lakini sasa taa imezimika,” alisema.


Naye Abdul Misambano, mwimbaji wa taarabu mahiri wa TOT, alisema: “Kwa kweli mimi naona haya ni kama majanga...tulikuwa tunajipanga kwa kampeni, lakini sasa sioni mbele.


Baadhi ya wasanii mbalimbali waliowahi kufanya naye kazi za sanaa kwa miaka ya nyuma wameelezea kuguswa na msiba huo huku wakielezea jinsi walivyomfahamu wakati wa uhai wake.


Msanii mkongwe wa nyimbo za dansi, Hamza Kalala alisema ameshtushwa sana na msiba huo huku akibainisha kumfahamu tangu mwaka 1985, alipokuwa akitumikia bendi ya JWTZ.


Alisema, marehemu Komba kwa mara ya kwanza walifahamiana naye kwenye sherehe za mbio za Mwenge, uwanja wa Kaitaba Mjini Bukoba mkoani Kagera.


“Tuliongea sana kuhusu muziki, mpaka anaondoka kwenda CCM hakuwa amebadilika uwezo wake wa kisanaa, kuwa na kipaji kikubwa cha ubunifu wa kutunga mashairi…kwa kweli tumempoteza mtu muhimu sana katika tasnia ya muziki huo wa dansi,” alisema Mzee Kalala.


Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Aset na Bendi ya Twanga Pepeta, Asha Baraka alisema:“Miaka ya ushindani wa bendi 2000/03 tulikuwa wote mpaka tukajenga mahusiano makubwa sana, alininshauri kama kaka yangu kwenye muziki na ndani ya chama, Nec, mpaka hatua ya mwisho alitaka kuivunja TOT. Kwa kweli sijui niseme nini yaani nimeishiwa nguvu kabisa, siyo rahisi kusahau msiba wake,” alisema Asha.


Naye msanii mkongwe wa bendi ya Magereza, Mafumu Bilali ‘Mbombenga’ alisema Komba alikuwa na mchango siyo CCM tu, bali kwa taifa na jamii kwa ujumla na kwamba mchango wake hautasahaulika.MWANANCHI


Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: