BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KAPT JOHN KOMBA AWEKA HISTORIA KATIKA MAZISHI YAKE, AZIKWA NA GARI KUBWA AINA YA TINGATINGA MKOANI RUVUMA.



Ndugu na jamaa wakisaidiwa na kijiko cha tingatinga kushusha mfuniko wa zege kwenye kaburi la Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba aliyezikwa katika Kijiji cha LItuhi, wilayani Nyasa, Ruvuma jana. Picha na Emmanuel Herman.


Nyasa.
Safari ya mwisho ya mbunge wa Mbinga Magharibi jana ilihitimishwa saa 9.25 alasiri wakati mwili wake ulipofunikwa na mfuniko mkubwa wa zege uliobebwa na gari maarufu kwa jina la “kijiko”.


Haikuwa kitu cha kawaida wakati gari hilo kubwa likishusha mfuniko huo wa zege kwenye kaburi la mwimbaji huyo maarufu wa nyimbo za uhamasishaji za CCM na kiongozi wa kundi la Tanzania One Theatre (TOT), lakini majonzi yaliwafanya waombolezaji kulichukulia tukio hilo kuwa la kawaida.


Safari ya Komba, iliyoanza miaka 61 iliyopita kwenye kijiji cha Lituhi ambako alizikwa jana, ilikamilishwa kwa salamu mbalimbali ambazo zilielezea ushupavu wa kapteni huyo mstaafu wa jeshi.


Mazishi hayo yaliyohudhuriwa na mamia ya wananchi, wakiwamo viongozi mbalimbaliwakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete na mkewe Salma, yalifanyika katika makaburi ya Misheni,katika Kijiji cha Lituhi (Bundi) wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.


Nyuso za majonzi zilitawala kwa waombolezaji waliojitokeza nyumbani kwa marehemu, takriban mita 500 kutoka katika makaburi hayo na baadaye katika misa iliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Lituhi, ikiongozwa na Askofu John Ndimbo wa Jimbo Katoliki la Mbinga.


Kaimu katibu wa Bunge, John Joel, akisoma wasifu wa marehemu, alisema Kapteni Komba aliyefariki dunia Februari 28, mwaka huu akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam, alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu na mara kadhaa Ofisi ya Bunge ilimpeleka India kwa matibabu. Pia alikuwa na tatizo la kisukari ambalo ndilo lililochukua maisha yake.


Mazishi hayo yalishuhudiwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Edward Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Utaratibu na Bunge), Jenister Mhagama na mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi.


Wengine ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Ali Abdallah Ali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Spika wa Bunge, Anne Makinda.


Uwanja wa ndege
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Songea, viongozi mbalimbali waliwasili kwa ndege za kukodi na Lowassa ndiye aliyefungua mlango kwa ndege iliyotua saa 2:33 asubuhi akiambatana na mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani.


Haikupita muda mrefu, ndege nyingine ilitua saa 2:50 ikiwa na Spika Makinda na msafara wake uliomjumuisha mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe.


Saa 3:22 ilitua ndege iliyobeba ujumbe wa CCM ukiongozwa na Kinana. Wengine waliokuwamo ni naibu katibu mkuu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, katibu wa itikadi na uenezi, Nape Nnauye na mwimbaji wa kikundi cha TOT, Khadija Kopa. Pia baadaye Rais Kikwete alitua na ndege ya Serikali.


Mwili wa marehemu uliwasili ukiwa katika moja ya ndege mbili zilizobeba familia yake, ndugu na watu mbalimbali wa karibu.


Fulana za Lowassa
Wakati ibada ya misa ikiendelea, walionekana vijana wakiwa wamevaa fulana nyeupe na nyeusi zenye ujumbe wa “Marafiki wa Lowassa”, zilizokuwa zimeandikwa mbele “4 U Movement Lowassa” huku mgongoni zikiandikwa “Kapteni John Damiano Komba 1954-2015 Friends of Lowasa”.


Baada ya vijana hao kuonekana, mmoja wa viongozi wa Bunge alimwamuru mmoja wao aliyekuwa anapiga picha kwenda kuivua, lakini aligoma na hakuna kati yao aliyekubali kuivua hadi mazishi yalipomalizika. Mmoja wa vijana hao ambaye aligoma kutaja jina lake aliiambia Mwnanchi akisema: “Kwa sasa fulana zimeisha kwa kuwa zilizokuwa zinagawiwa. Lakini kama unazitaka unaweza kuacha namba yako na utaletewa sehemu yoyote utakapokuwa.


“Tumeamua kutoa fulani hizi kama zawadi ya kumbukumbu kwa mchango alioutoa Komba wakati wa urafiki wao (na Lowassa) na ndiyo maana unaona tumezivaa.”


Salamu za rambirambi
Katika salamu zake, Gasper Tumaini, katibu wa kikundi cha Sanaa cha TOT kilichokuwa kikiongoza Kapteni Komba, alisema Komba alipenda jimbo lake na chama chake na kuwa siku moja kabla kifo walikwenda kurekodi nyimbo za uchaguzi. Kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, mbunge wa Lindi Mjini (CUF), Salum Barwany alisema: “Tunatoa pole kwa wananchi na familia kwa kuondokewa na mbunge mahiri na shupavu, tumefika kuonyesha namna Komba alivyoishi vizuri nasi.


“Kila mmoja amejifunza namna Komba alivyoishi na watu vizuri , alikuwa akinipa faraja wakati matukio ya mauaji ya albino yalipotokea na wakati wote alikuwa akinihakikishia usalama wangu, hivyo tumepata pigo kubwa kwa kuondoka kwake.”


Katibu Mkuu CCM, Abdulahman Kinana, alisema: “Tuna huzuni kubwa kutokana na msiba mkubwa uliotokea. Komba alifanya kazi nzuri ya kuwahudumia na kuwajali na kuangalia maslahi ya wananchi aliowaongoza. Alhamisi iliyopita alikuja ofisini kwangu na kuniambia anakwenda kiwandani kutafuta mabati 900 kupeleka jimboni kwake.”


Waziri Mhagama kwa niaba ya Serikali alisema: “Komba alikuwa kiungo muhimu kwa serikali. Wengi wamemzoea katika masuala ya siasa na chama, wote wanamkumbuka kwa tukio la kuimba nyimbo za maombolezi wakati wa msiba wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.”


Spika Makinda alitumia fursa hiyo kuzungumzia muswada wa mabadiliko katika sheria za Kiislamu ya mwaka 1963 kuhusu Mahakama ya Kadhi akisema inatakiwa kubadilishwa kushughulikia mirathi, talaka hivyo Wakristo wawe wavumilivu, wasikubali kuzungumzia vitu ambavyo hawana uhakika navyo.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: