BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KAPTENI JOHN KOMBA AWAACHA CCM NJIAPANDA

John Komba


KIFO cha Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba kimetajwa kuwa pigo kubwa kisiasa kwa viongozi wengi ambao baadhi wameshuhudia namna walivyosaidiwa katika kampeni kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Pigo hilo linatokana na hali halisi ya kipindi cha sasa kuelekea uchaguzi mkuu, ikielezwa kwamba pamoja na masuala mengine, Komba alikuwa katika maandalizi makubwa ya kuleta mabadiliko katika sanaa ya muziki nchini kwa kushirikisha wanamuziki wa zamani na wa kizazi kipya.

Rais Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma wakiifariji familia ya Mbunge wa Mbinga Magharibi na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Kapteni John Komba nyumbani kwake Mbezi kwa Komba, Dar es Salaam jana. (Picha na Ikulu).
Katika msiba ambao jana Rais Jakaya Kikwete aliongoza viongozi na watu mbalimbali kuomboleza nyumbani kwa Komba, Dar es Salaam, miongoni mwa waliokiri kunufaika na Komba katika harakati za kupata ubunge, ni Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba.

“Kuondoka kwake ni pigo sana, binafsi alinisaidia sana katika kampeni zangu za kuwania ubunge uchaguzi uliopita…lakini kikubwa alikuwa ni mtu mkweli, asiyependa kupindisha mambo, mara zote alikuwa haongei unafiki, tumeondokewa na nembo yetu tena katika kipindi tulichokuwa tunamhitaji zaidi,” alisema Mwigulu.

Alisema ni pigo kwa CCM, wabunge na Watanzania kwa ujumla, kwa kuwa Komba alikuwa nembo ya chama hicho kutokana na kwamba, sehemu yoyote ambayo wimbo wake ukipigwa, lazima jina CCM litajwe.

Kwa upande wake, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ingawa alisema chama kitajipanga kikiwa na imani ya kufanya vizuri kwenye kampeni, alisisitiza kifo hicho kimetokea katika kipindi ambacho alikuwa katika maandalizi makubwa ya kuleta mabadiliko katika sanaa ya muziki nchini.

“Juzi saa sita mchana (siku aliyofariki dunia) nilizungumza naye, tuliongea mengi ikiwemo ombi lake la fedha kwa ajili ya mradi huo mpya wa kushirikisha wanamuziki wa zamani na wa sasa, kwa kweli hili ni pigo lakini kama chama tutajipanga na nina imani tutafanya vizuri katika kampeni zetu za uchaguzi,” alisema.

Waziri wa Mambo ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema mbunge huyo ameondoka ghafla na ni pigo kwa CCM kwa sababu alikuwa na nguvu ya kufikisha chama kwenye ushindi.

“Msiba huu umegusa ukanda mzima wa Afrika Mashariki, kwetu sisi wana CCM Komba ni ishara ya upendo na mshikamano, ameondoka ghafla kama mshumaa uliuzima, hili ni pigo kwetu kwa sababu bado alikuwa na nguvu ya kuifikisha CCM kwenye ushindi,” alisema Membe.

Aidha alisema mbunge huyo alikuwa mstari wa mbele katika kutoa ushahidi wake kwenye mazungumzo ya mgogoro wa Ziwa Nyasa uliopo baina ya Malawi na Tanzania, ambapo aliwasilisha ushahidi wa makaburi ya babu zake yaliyoko ndani ya ziwa hilo ambayo ni ishara kuwa mpaka wa ziwa hilo upo katikati.

Kikwete msibani
Rais Kikwete alifika msibani hapo jana saa mbili asubuhi. Viongozi wengine waliohudhuria msiba huo, ni Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Spika wa Bunge Anne Makinda na Mbunge wa Sengerema William Ngeleja.

Pamoja na hao, viongozi wengine waliohudhuria msiba huo ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Asha- Rose Migiro, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Stephen Kebwe, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama na Mbunge wa Songea Mjini, Emmanuel Nchimbi.

Pia viongozi kutoka vyama vya upinzani waliohudhuria msiba huo ni Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.

Lowassa
Kwa upande wake, Lowassa alisema CCM imepoteza kamanda aliyekuwa mstari wa mbele kuhamasisha shughuli za chama.

“Ukweli ni kwamba pengo lake kama msanii halitozibika.Mungu anaweza kumuita yeyote yule na wakati wowote, hilo hatuna uwezo wa kulizuia, jambo la muhimu ni sisi kuwafariji familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu,” alisema.

Ngeleja
Kwa upande wake Ngeleja, alisema msiba huo ni pigo kwa Watanzania hasa wanachama wa CCM kutokana na ukweli kuwa alikuwa anapenda kusimamia ukweli na mambo anayoamini, jambo lililomfanya aishi kwa uhalisia.

“Alitumia kipaji chake cha kuzaliwa si tu kuimba nyimbo za kuhamasisha chama pekee, bali alihamasisha pia uzalendo katika nyimbo zake zote, uwe wa msiba au sherehe lazima aweke chombezo la kuhamasisha uzalendo, alipenda nchi yake,” alisema.

Waziri Migiro
Pia Waziri Migiro kwa upande wake, alisema “Kifo cha Komba ni pigo kwetu sisi wabunge wenzake, kila mtu anafahamu mchango wake ndani ya CCM, nimefanya kazi naye akiwa mbunge na siku mbili kabla ya kifo chake nilionana naye alikuwa mcheshi sana na alizungumzia mambo mengi, ikiwemo kuendeleza sanaa ya muziki nchini.”

Spika Makinda
Spika Anne Makinda naye alisema taifa limepoteza kiongozi mahiri aliyependa ukweli na uwazi, lakini pia alionesha kujali wananchi wake.

Alisema tangu awe mbunge, amefanya vizuri jimboni kwake ambako kwa sasa kuna maendeleo tofauti na zamani.

Jimboni vilio
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wapiga kura na wana CCM wilayani Nyasa, walimtaja Komba kuwa alikuwa miongoni mwa wabunge waliojitahidi kutekeleza ahadi, ikiwemo kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo jimboni.

Katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT), Wilaya ya Nyasa, Grace Haule, alimtaja Komba kuwa mtu aliyekuwa na upendo mkubwa kwa wakazi wa jimboni kwake.

Alisema ni mbunge aliyetekeleza kwa vitendo ahadi alizotoa kwa wananchi wa Nyasa na aliwezesha wananchi wa Nyasa kuongeza kasi katika ushiriki wao wa shughuli mbalimbali za maendeleo. Alisema alisimamia vizuri ujenzi wa vyumba vya maabara unaoendelea nchi nzima.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa UWT, Komba alishanunua mabati kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya mabara kwa maeneo ambayo ujenzi huo ulikuwa haujakamilika.

Alitoa na kusimamia wazo la kuanzishwa kwa Wilaya ya Nyasa ambayo ni mpya, jambo ambalo imeelezwa wananchi wataendelea kumkumbuka.

Watu wenye ulemavu ni kundi ambalo linatajwa pia litamkumbuka kwa msaada na vifaa mbalimbali alivyowahi kuwapatia.

Wanaokodolea jimbo Watu wanaotaka kugombea ubunge katika Jimbo la Mbinga Magharibi wameaswa kuwa watulivu, wasubiri muda wa mchakato ufike badala ya kuanza kutumia mwanya wa kifo cha mbunge huyo kuanzisha vurugu.

Katibu huyo wa UWT amesema utulivu unahitajika katika kipindi hiki kigumu vinginevyo, zikianza vurugu zinaweza kutoa nafasi kwa wapinzani kuchukua jimbo hilo.

Komba alikuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi, wilayani Nyasa kwa vipindi viwili kuanzia mwaka 2005 hadi 2015. Alishaweka wazi nia ya kuendelea kugombea ubunge wa jimbo hilo kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Ratiba ya mazishi
Msemaji wa familia ambaye pia ni shemeji yake na Komba, Dominique Mwakangale, alisema mwili wa marehemu uliwasili jana jioni na kulala nyumbani kwake ambapo leo kuanzia saa moja hadi saa tatu, kutakuwa na misa na kutoa salamu za mwisho kwa ndugu na familia.

Saa 4 mwili utawasili katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuagwa ambapo viongozi mbalimbali wa kitaifa pamoja na wabunge wenzake watapata fursa ya kutoa salamu zao za mwisho.

Baadaye, utasafirishwa kwa ndege kwenda Songea mjini ambako CCM mkoani Ruvuma, pia wameandaa misa na kumuaga kiongozi wao na baadaye atasafirishwa hadi kijijini kwao Lituhi ambapo atapumzishwa rasmi kesho.

Komba alifariki dunia juzi majira ya saa 10 jioni akiwa njiani kwenda Hospitali ya TMJ.

Kwa mujibu wa familia yake, alipatwa na mauti hayo kutokana na kusumbuliwa na magonjwa kisukari na shinikizo la damu.
HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: