Mwalimu Samsoni Chande (54) pamoja na mkeweYunis Luseta (44), ambao walifunga uzazi baada ya kuzaa watoto 12, kwa sasa ni vinara wa kuelimisha jamii juu ya mpango huo eneo la kanda ya ziwa.
Kuna njia mbalimbali za uzazi wa mpango na kila ya uzuiaji mimba ina faida zake na hasara. Hata hivyo kuna chaguo mbalimbali ambazo zinafanya kazi kwa kila mwanamke au mwanaume.
Daktari au muuguzi aliyefunzwa uzazi wa mpango anaweza kumsaidia kila anayehitaji huduma kuamua ni njia ipi sahihi kwake kwa muda mrefu.
Afya ya uzazi ni ya msingi kwa afya ya ujumla na ustawi wa mtu mmoja mmoja, wana ndoa, familia na kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limekuwa likisisitiza njia za uzazi wa mpango zinazozingatia afya ya uzazi kwa maana kwamba hali ya kuwa mkamilifu kimaumbile, kiakili na ustawi wa kijamii kwa mambo yote yanayohusiana na mfumo mzima wa uzazi.
Kwa hiyo, afya ya uzazi inamaanisha kwamba watu wanaweza kuwa na maisha ya kujamiina yanayojitosheleza na salama na kwamba wanaweza kuzaliana na kuwa uhuru katika kuamua mambo yanayowahusu.
Ndiyo maana njia mbalimbali za uzazi wa mpango zimefanyiwa tafiti za muda mrefu ili kuthibitisha usalama wake kwa mtumiaji.
Zipo aina nyingi za uzazi wa mpango miongoni ni zile zinazomhusu mwanamke kama vile kutumia kalenda, kumeza vidonge, kuchoma sindano au vipandikizi.
Pia zipo njia ambazo zinaweza kuwahusisha pande zote, mwanaume na mwanamke, kama vile kondomu na kufunga uzazi.
Kufunga uzazi kunaweza kutekelezwa na wanandoa kwa maana kwamba hawatarajii tena kuendelea kuzaa.
Kama mpango huu ukitekelezwa kwa mwanamke ina maana kwamba mirija inayopeleka yai kwenye kizazi, huzibwa kabisa.
Vivyo hivyo kwa wanaume, mirija inayotoka kiwandani kupeleka mbegu tayari kutoka na kurutubisha yai, hukatwa na kufungwa.
Kwa miaka mingi, mpango wa kupanga uzazi umekuwa ukitekelezwa kwa kuegemea upande wa mwanamke.
Matumizi ya njia za mpango wa uzazi kwa wanandoa ni moja wapo ya mikakati ya kufikia malengo ya milenia yaliyoanza kutumika tangu miaka 25 iliyopita.
Katika kipindi hicho, wanaume wengi wamekuwa wakipinga vikali kufunga uzazi kwa wasiwasi kwamba kitendo hicho kinaweza kikawaathiri katika nguvu za kiume.
Pengine inawezekana hawakuelimishwa vya kutosha na inawezekana hakuna hamasa zilizofanywa ili kuwachochea kutekeleza hilo.
Kwa mfano nchini India ili wanaume waweze kujitokeza kufunga uzazi walipewa zawadi. Aliyefanikiwa kufunga alipewa redio kaseti kubwa, watu wengi walijitokeza kwa ajili ya kupata zawadi kutokana na umaskini wao.
Mikoa ya Kanda ya Ziwa inatajwa kuongoza kwa uzazi usiozingatia mipango ambapo wastani wa watoto saba huzaliwa na kiwango cha ushiriki njia hizo ni mdogo ikiwa ni tofauti na mkoa wa Kilimanjaro ambapo una wastani wa familia moja huzaa watoto 4 na asilimia 59 wanatumia njia za uzazi wa mpango.
Kutokana na hali hiyo uchumi wa jamii Kilimanjaro uko juu kwa kuwa, kuzaliana kwao kunakwenda sambamba na ukuaji wa uchumi.
Watu wamekuwa wakijiuliza kama kweli kuna wanaume ambao wanaweza wakakubali kufunga uzazi?
Wataalamu tayari wamewahakikishia wanaume wengi kuwa njia hiyo ni salama na haipunguzi nguvu za kiume wala tatizo la kufikia kileleni wanapofanya tendo la ndoa.
Ushuhuda wa wanaume
Taarifa zinaonyesha kwamba katika kipindi cha miaka 25, wanaume wapatao 4000 wamefunga uzazi katika kanda ya ziwa.
Wanaume wengi wana hofu ya kuathiri uwezo wao wa kujamiiana iwapo watafunga uzazi lakini leo hii wapo wenzao waliothubutu kutumia njia zao na hapa wanatoa ushuhuda.
Mwalimu Samson Chande (54) na mke wake Yunis Luswetula (44) ni wakazi wa Kitongoji cha Mwamagelani, Kijiji cha Kasoli Wilaya ya Bariadi Mkoa wa Simiyu.
Hawa wana watoto 12 na ni miongoni mwa kundi la zaidi ya wanaume 400 Tanzania waliofunga uzazi.
Anasema uamuzi wao wa kufunga uzazi ni matokeo ya kuelemewa na mzigo wa familia kwa kuwa pamoja na mshahara wake, maisha yao hayakutofautiana na wanakijiji wengine wasiokuwa watumishi kwa kuwa, uliishia kula vizuri na hata kurudi nyuma kimaendeleo.
“Juni 21,2013 tulihudhuria mkutano Zahanati ya Mwamlapa Kijiji cha Kasoli, Kata ya Kasoli Wilaya ya Bariadi tukiwa wanaume wengi na wake zetu.
“Tulijifunza kuhusu njia mbalimbali za uzazi wa mpango. Tukalazimika kufunga uzazi maana uzito wa familia tuliyokuwa nayo tunaujua wenyewe,” anasema.
Chande ambaye ni Mwalimu wa shule ya Msingi Nyamagana anasema katika eneo hilo ni mwanamume pekee aliyefunga uzazi.
Anasema watu wengi walimshangaa kwa uamuzi huo na hasa ikizingatiwa alikuwa miongoni mwa waliokuwa na kipato kizuri kijijini hapo. Anasema kufunga kwake uzazi hakukusababishi nguvu za kiume kupungua na kukatwa kwa mirija ya kupitishia mbegu hakukuathiri hamu ya kujamiiana.
Isitoshe anasema nguvu za kiume zimeongezeka maana mwili unajijenga sawasawa na kuwa imara zaidi.
Mke wake naye anasisitiza kuwa kwa sasa anafurahia tendo la ndoa kuliko ilivyokuwa awali.
Anasema kuwa hakuwahi kupata nafasi ya kufurahia ndoa, maana kila wakati yeye aliambatana na ujauzito na watoto na wakati mwingine anaona aibu kuwapeleka kliniki.
“Kwa sasa nina mtoto wa miaka miwili, anazidiwa umri na wajukuu wangu watatu,” anasema.
Elias Samwel (58) ni mkazi wa kitongoji cha Kamilangete, Kijiji cha Nyenge kata ya Kurugongo, wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma ambaye naye alifunga uzazi.
Anasema ana watoto wanane na uamuzi wake wa kufunga uzazi ulimfanya baadhi ya marafiki zake kumueleza kuwa ni sawa na ameua kwa sababu amefungia ‘baadhi ya watoto’ wasiweze kutoka. Hivyo wakadai yeye hana tofauti na muuaji.
Anasema baadhi ya wataalamu wa afya walimpa moyo na kumuelimisha kuwa hakuna kosa lolote ni sawa tu na yule mtu anayetumia njia yoyote ya uzazi wa mpango.
Samwel ambaye ni mhudumu wa afya kijiji cha Nyenge kwa sasa ni kinara kuelezea ubora wa uzazi chini ya mradi wa RESPOND unaendeshwa na Shirika la Engerhealth kwa msaada wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID), anasema:
“Wanaume 12 katika kata yangu wamefunga uzazi na dhana waliyokuwa nayo kuwa mimi ni muuaji imeishatoweka. Wengi sasa wanafahamu na wanaelezea faida za mwanamme kufunga uzazi.”
Anadai kuwa baada ya kufunga sasa anajiona mpya na upendo ndani ya ndoa umeongezeka kwa kuwa walikuwa hawapati faraja kutokana na mke wake kuhangaika na watoto kila mwaka.
Mratibu wa Uzazi wa Mpango Mkoa wa Mwanza, Secilia Mrema anasema kuna changamoto kubwa ya ushiriki wa wanaume katika huduma za uzazi wa mpango kutokana sababu mbalimbali ikiwemo imani ya kuharibu uwezo wa nguvu za kiume.
“Imani potofu juu ya huduma hiyo ni moja ya changamoto na nchanzo chake ni kutokuwa na elimu sahihi,”anasema.
Hata hivyo anakiri kwa mkoa wa Mwanza kuna ongezeko la wanaume kutoka watatu hadi 89 kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi 2014.
Anasema njia ya kufunga uzazi kwa wanaume maarufu kama vasektomi, ni salama na haina madhara kama uvumi unavyoenezwa kuwa nguvu za kiume.
Anasema hakuna uhusiano wowote wa nguvu za kiume kupungua na ufungaji wa njia ya mbegu za kiume.
Anasema kiwango cha manii ayatoayo mwanaume hakitaathirika kutokana na ufungaji huo bali atatoa kama kawaida wakati wa tendo la ndoa na tofauti yake ni kwamba hazitakuwepo mbegu za kurutubisha yai la kike.
Vikwazo vya utekelezaji wa njia za uzazi wa mpango, anasema lengo la nne la milenia la kupunguza vifo vya watotokwa kwa theluthi mbili, kinamama kwa robo tatu na kuongeza kiwango cha uzazi wa mpango kwa asilimia 60, kama ilivyoanishwa kwenye lengo la 5, haitafikiwa hapo Desemba mwaka huu kama ilivyokusudiwa.
Naibu, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk Kebwe Stephen Kebwe anasema utumiaji mdogo wa njia za uzazi wa mpango ndio umesababisha hata kasi ya kushuka kwa idadi ya vifo vya kinamama kuwa ndogo.
“Vifo vya akina mama vimepungua kutoka 578 hadi 454 kwa kila 100,000 wanaoenda kujifungua.”
“Wanawake 124 wanaokolewa sasa na jitihada zinaendelea kushusha idadi hiyo. Vifo vya watoto vimeshuka kutoka 68 hadi 54, sawa na watoto 14 wanaokolewa kati ya 1,000 wanaozaliwa,” anabainisha.
Anasema ushiriki wa uzazi wa Mpango unatakiwa kuwa mkubwa kwa kuwa athari kiuchumi ni kubwa, kwa kuwa ongezeko la watu haliendani na ukuaji wa uchumi,hali inayopelekea familia nyingi kuzidi kuwa maskini,ongezeko la migogoro ya ardhi ,ukuaji wa miji.
Anasema asilimia 25 ya Watanzania wanahitaji kutumia njia hizo hawatumii, ama kwa kukosa elimu, wataalamu na vituo vya afya, kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa kasi ya uzazi imeendelea kuwa juu.
Wiki ijayo wataalamu mbalimbali wataelezea juu ya ushuhuda huo iwapo ufungaji wa uzazi kwa wanaume; vasektomi, unaongeza nguvu zaidi katika ufanisi wa tendo la ndoa.MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment