MECHI YA WATANI, OKWI AIMALIZA YANGA SC LIGI KUU TANZANIA BARA KWA BAO 1-0.
Mshambuliaji wa Simba SC, Emmanuel Okwi aimaliza yanga sc ligi kuu Tanzania bara baada ya kuitungua bao na kuiwezesha timu yake kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
TIMU ya Simba leo imeendeleza ubabe kwa mahasimu wao Yanga, baada ya kuifunga bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya Simba kuendeleza ubabe kwa Yanga baada ya Desemba 12, mwaka jana kuibuka mshindi katika mchezo wa Nani Mtani Jembe uliochezwa katika uwanja huo.
Katika mchezo huo Simba ambayo ilitumia mfumo wa 4-4-2, ilionekana kupania kupata bao la mapema ambapo dakika ya pili, Ibrahim Ajibu aliachia shuti kali akiwa nje ya 18 lilitoka nje ya lango.
Yanga ilijibu shambulio hilo dakika ya 16 ambapo, Simon Msuva akiwa ndani ya 18 naye aliachia shuti kali lililodakwa na kipa, Ivo Mapunda.
Dakika ya 17 Msuva alipata nafasi nyingine ya kufunga baada ya kuipangua ngome ya Simba, lakini kabla ya kupiga aliwahiwa na mpira kuokolewa.
Amis Tambwe ambaye jana alionekana kuipania mechi hiyo alikosa bao la wazi dakika ya 19 baada ya kupiga mpira wa kichwa kilichopaa juu ya lango.
Beki wa Yanga, Said Juma alipewa kadi ya njano baada ya kumchezea madhambi Ajibu ambaye alikuwa katika harakati ya kwenda kufunga.
Mwamuzi wa mchezo huo alilazimika kutoa kadi za njano kwa wachezaji Danny Mrwanda na Shaban Kessy wa Simba kwa utovu wa nidhamu.
Dakika ya 35, Mrisho Ngassa alikosa bao akiwa ndani ya 18 baada ya kupokea pasi safi ya Haruna Niyonzima ambaye alipiga shuti likaokolewa na kipa Mapunda ambapo mpira ukamkuta tena Ngassa lakini akashindwa kupachika mpira kimiani.
Tambwe alikosa bao lingine dakika ya 41 baada ya kuingia na mpira hadi ndani ya 18, lakini shuti lake likadakwa na kipa Ivo.
Dakika ya 43 nusura, Emmanuel Okwi angeipatia bao Simba baada ya kupiga faulo iliyotoka nje kidogo ya lango la Yanga.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuwa na kiu ya kupata bao ambapo dakika ya 52 Okwi aliipatia timu hiyo bao pekee baada ya kumchambua kipa wa Yanga, Ally Mustafa 'Bathez' akiwa nje ya 18 ambaye alikosa jinsi na kushtukia mpira ukitikisa nyavu.
Simba ilicharuka tena dakika ya 61 ambapo Ajibu nusura angeipatia Simba bao baada ya kupiga shuti lililopaa nje ya lango.
Dakika ya 66 Simba ililiandama lango la Yanga ambapo, Ramadhan Singano 'Messi' alipiga shuti lililopaa nje ya lango.
Hussein Javu aliyeingia badala ya Mrwanda alikosa bao dakika ya 78 akiwa yeye na kipa Ivo.
Okwi nusura angeipatia bao lingine Simba, dakika ya 81 baada ya kuachia mkwaju mkali uliotoka nje ya lango.
Hadi mwamuzi wa mchezo huo anapuliza kipenga cha kumaliza mpira Simba waliibuka kifua mbele kwa bao 1-0.
Kwa ushindi huo Simba wamechumpa hadi nafasi ya tatu baada kufikisha pointi 26 na kuishusha Kagera Sugar iliyobaki na pointi zake 25.
Kwa matokeo hayo Yanga bado inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 31 ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 30.


0 comments:
Post a Comment