BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MTENI WA SIMBA SC ATANDIKWA BAO 2-0 NA YANGA UWANJA WA MKWAKWANI TANGA.


Shabiki wa Yanga akishangilia ushindi wa timu yake dhidi ya Mgambo JKT katika mchezo wa Ligi kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga jana.Yanga ilishinda mabao 2-0.


Yanga imevunja mwiko wa kutoifunga JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani baada ya kuichapa kwa mabao 2-0 jana na kukalia usukani wa ligi.


Yanga kwa misimu mitatu mfululizo haijawahi kuifunga Mgambo kwenye uwanja huo na jana walivunja mwiko kwa mabao yaliyofungwa na Simon Msuva na Amiss Tambwe na kuwafanya kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 37, nne zaidi ya mabingwa watetezi Azam inayocheza leo na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, pointi nane zaidi ya Simba itakayoivaa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa.


Mshambuliaji Msuva alipoteza nafasi nne za wazi za kufunga kabla ya kurekebisha makosa yake kwa kumalizia mpira wa kichwa uliopigwa na Kpah Sherman dakika ya 77 na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa Yanga waliokuwa kimya muda mwingi wa mchezo.


Dakika sita baadae Msuva alipiga krosi iliyompita kipa wa Mgambo JKT, Godson Mmasa na kumkuta Tambwe aliyeunganisha kwa kichwa wavuni, bao lililowainua benchi lote la ufundi la Yanga kunyanyuka na kushangilia kwa furaha.


Mvua kubwa iliyonyesha Tanga ilisabisha uwanja wa Mkwakwani kujaa matope na kuufanya mchezo huo kukosa ufundi na kuwa wa butua butua nyingi ingawa mabeki wa Mgambo walifanya kazi ya ziada baada ya kumfisha Tambwe muda mwingi wa mchezo.


Imani za Kishirikina
Kama kawaida mechi hiyo ilijaa na imani za kishirikina kwani Yanga walifanya kama walichofanya watani zao Simba wiki iliyopita baada ya kugoma kuingia vyumbani kabla ya mchezo na kuamua kukaa kwenye viti vilivyokuwa nje ya basi lao kubwa.


Hata hivyo, tofauti na Simba ni kwamba Yanga waliingia vyumbani na kutoka wakati watani zao wekundu wa Msimbazi hawakuingia kabisa, lakini wakachezea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa timu hiyo ya Mgambo.


Yanga na Mgambo zilirudia jambo hilo wakati wa mapumziko kwani zote hazikuingia katika vyumba vya wachezaji na kukaa pembezoni mwa uwanja hivyo kuzusha mshangao kwa mashabiki waliokuwa uwanjani hapo.


Mchezo mwingine ulichezwa jana kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona wenyeji Ndanda FC walishindwa kutumia uwanja wa nyumba baada ya kulazimishwa suluhu na JKT Ruvu.


Simba, Azam vitani
Mabingwa watetezi Azam wenyewe watajiuliza mbele ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, wakati Simba baada ya kunyukwa na Mgambo JKT leo watakuwa Uwanja wa Taifa kujiuliza mbele ya Ruvu Shooting.


Azam itashuka kwenye Uwanja Mkwakwani kwa lengo moja tu la kupata ushindi dhidi ya Coastal Union ili kuendelea kuipa presha Yanga inayoongoza ligi.


Endapo Azam itapoteza kwa Coastal Union na Simba ikashinda basi tofauti ya pointi baina ya timu hizo itabaki moja na kufanya mbio za kuwani nafasi ya pili kuwa ngumu zaidi kwao.


Simba imeshinda mechi sita kati ya saba ilizocheza dhidi ya Ruvu Shooting na mmoja wakitoka sare katika Ligi Kuu. Simba itaingia uwanjani wakijua ushindi katika mchezo huo utarudisha matumani yake ya kusaka ubingwa pamoja na kucheza mashindano ya kimataifa mwakani.


Mechi nyingine leo itakuwa kati ya Prisons dhidi ya Polisi Morogoro.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: