BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SABABU YA ASKOFU WA KANISA LA UFUFUO NA UZIMA JOSEPHAT GWAJIMA KULAZWA CHUMBA CHA WAGONJWA MAHUTUTI HOSPITALI YA TMJ DAR ES SALAAM.

 
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na uzima ,Josephat Gwajima akihudumiwa na muuguzi wa hospitali ya TMJ, Dar es Salaam jana.Askofu Gwajima amelazwa katika hospitali hiyo baada ya kuzimia wakati akihojiwa na polisi juzi.Picha na Salim Shao.


Dar es Salaam.
Hali ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima inaendelea vizuri, ingawa haijabainika anasumbuliwa na tatizo gani kiafya hadi hapo vipimo vitakapopatikana.



Gwajima aliyelazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu kwenye Hospitali ya TMJ, Mikocheni, Dar es Salaam alifikishwa hospitali hapo juzi usiku baada ya hali yake kubadilika ghafla alipokuwa akihojiwa Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.


Askofu huyo alijisalimisha kituoni hapo juzi mchana akiitikia wito wa polisi uliomtaka kufanya hivyo kutokana na tuhuma za kutoa lugha chafu dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.


Akizungumza na gazeti hili hospitalini hapo jana, Dk Fortunatus Mazigo anayemtibu kiongozi huyo wa kiroho alisema kuwa hali yake haijabadilika tangu afikishwe hospitalini hapo jana (juzi) usiku.


Alisema hadi sasa bado hawajafahamu ana tatizo gani kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya vipimo, ingawa kuna matumaini kutokana na kuwa na hali nzuri katika mfumo mzima wa damu, mapigo ya moyo na viungo vyote vinafanya kazi.


“Sina cha kusema kuhusu ugonjwa wake kwa sababu hiyo ni siri ya anayeumwa na daktari, ninachoweza kusema hali yake aliyokuja nayo jana usiku haijabadilika, ingawa kuna matumaini kwa sababu vitu muhimu vipo sawa,” alisema Dk Mazigo.


Hali ilivyo hospitalini hapo
Waumini kutoka katika Kanisa na Ufufuo na Uzima walikuwa wakipishana hospitalini hapo jana ili kumwangalia kiongozi wao ambaye amelala kitandani, akiwa hawezi kuzungumza.


Mchungaji Yekonia Biyagaze ndiye anafanya kazi ya ziada kuhakikisha waumini wanaoshindwa kupata nafasi ya kuingia wodini kumwona kiongozi wao wanapata maelezo ya kina kutoka kwake kuhusiana na kinachoendelea kwa mgonjwa huyo.


Baadhi ya waumini waliozungumza na gazeti hili hospitalini hapo, walieleza kushtushwa kwao.


Muumini aliyejitambulisha kwa jina la Masinde alisema kuwa anachofahamu kiongozi wake alikuwa Arusha na alirudi ili kutii amri ya polisi ya kutakiwa kufika kituoni hapo kwa ajili ya mahojiano.


“Nimeshtuka, natamani ufanyike uchunguzi wa kina tubaini nini kinaendelea ni kiongozi mkubwa na ni muhimu kwetu kama waumini wake, sitarajii kama litatokea jambo baya, kwani inaweza kuwa hatari,” alisema muumini huyo.


Masinde alisema walikuja wengi, lakini baada ya kupewa maelezo na Mchungaji Biyagaze wakaamua kuondoka ili kupisha na wengine wapate nafasi ya kumjulia hali kwa sababu kila mmoja anataka kusikia au kuona kwa macho badala ya kuambiwa akiwa mbali.


Awali, kabla ya kufika katika wodi hiyo kulikuwa na askari kadhaa waliovaa kiraia waliozunguka eneo hilo kwa kupanda juu ghorofani alipo Askofu Gwajima na kushuka, ambapo baada ya muda walipungua na kubaki wachache.


Kabla ya kuingia chumba cha mgonjwa
Tofauti na ilivyozoeleka kuwa unapotaka kuingia chumba cha mgonjwa mnapewa maelekezo na daktari, katika kile kinachoonekana kuhakikisha usalama unakuwapo.


Aliyekuwa na jukumu la kutoa maelekezo kwa watu wote wanaokwenda kumwona mgonjwa, wakiwamo wanahabari ni Mchungaji Biyakaze, ambaye aliwataka wakiingia ndani wasishike kitanda, wala shuka kwa usalama wao.


Hata baada ya kuingia, kundi la watu Askofu Gwajima hakufumbua macho wala kupepesa, hali inayoonyesha kuwa bado yupo katika hali isiyoridhisha.


Akiwa amelala chali, huku amefungwa mashine ya kupimia mapigo ya moyo mkononi, chumbani humo kulikuwa na muuguzi aliyekuwa anaratibu kila kinachoendelea, ikiwamo kuwazuia watu wasiguse kitu chochote.


Kabla ya kuingia ndani na kumwona mgonjwa, Mchungaji Biyakaze alizungumzia hali ya mgonjwa alisema anaendelea vizuri, ingawa alishindwa kumalizia na kubaki akisema...lakini na kumalizia kusema kuwa kinachonipa moyo wa kuwa atapona kwa sababu ni mtumishi wa Mungu sina jingine.


Mlangoni mwa wodi alimolazwa Askofu Gwajima kulikuwa na watu ambao hawatoki muda wote, mmojawao alipopewa pole alisema kuwa asipewe pole kwani huo ni ushindi na hakuna mapambano yasiyokuwa na vikwazo.


“Usinipe pole, nipongeze huu ni ushindi na ndiyo mapambano yalivyo lazima kuwe na vigingi, ambavyo ukivivuka unakuwa umeshinda na sisi tumeshinda,” alisema kijana huyo.


Slaa, Baregu wafika hospitalini
Saa sita mchana, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibroad Slaa alifika hospitalini hapo akiongozana na Mjumbe wa Kamati Kuu, Profesa Mwesiga Baregu kumwona Gwajima.

Baada ya kumwona mgonjwa, Dk Slaa alizungumzia utata unaowapata watu wanaohojiwa na polisi, huku akisisitiza kuna vitu vinatakiwa kufanyiwa kazi, ikiwamo kubaini kuna nini.


Alisema sheria za kuhojiwa zipo wazi kuwa mtu asihojiwe zaidi ya saa nane, vitu kama hivyo vinatakiwa kuzingatiwa katika mahojiano.


“Nyinyi kama waandishi ndiyo kazi yenu kuangalia kwa undani kuna nini kinaendelea katika haya mahojiano hadi mtu anapoteza fahamu, siyo huyu hata kama kuna mwingine ilimtokea hali hiyo,” alisema Dk Slaa.


Akizungumza hali ya mgonjwa kwa mtizamo wake, alisema kuwa daktari anayemtibu hawajawafahamisha nini kimempata, lakini kwa bahati mbaya hata mgonjwa mwenyewe hawezi kuzungumza na wao hawakuweza kumuuliza chochote, hivyo hana la kusema.


“Angekuwa anazungumza, labda angeniambia ilikuwaje, lakini hawezi hivyo sijapata lolote kutoka kwake wala daktari,” alisema Dk Slaa.
MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: