Simba mwenda pole... Ndiye mla nyama. Au kwa lugha nyingine unaweza kusema Simba dhaifu ndiyo huwa inaifunga Yanga. Usemi huu umekuwa ukijidhihirisha mara nyingi Yanga na Simba zinapokutana hasa katika miaka ya hivi karibuni. Yanga mara kwa mara ikiwa katika kiwango bora uwanjani huwa inapata wakati mgumu inapokutana na Simba mbovu, jambo hili limekuwa likiwaumiza wachezaji wa klabu hiyo, viongozi na hata mashabiki kuwa ni kwa nini hali hiyo hutokea na mpaka leo wameshindwa kupata jibu.
Yanga na Simba zitakutana Machi 8 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam ukiwa ni mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara. mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka suluhu.
Wakati timu hizo zikitarajia kukutana, Yanga imeonekana iko katika kiwango bora msimu huu kwani inaongoza ligi kwa kuwa na pointi 31 ikiizidi Simba pointi 11, huku wekundu hao wa Msimbazi wakienda mwendo wa kusuasua kwenye ligi mithili ya homa za vipindi.
Kwa nini Yanga bora huwa inazidiwa na Simba dhaifu?
Simba hata kama itakuwa katika kiwango dhaifu huwa inafanya maandalizi makubwa kujiandaa dhidi ya Yanga kuliko inavyojiandaa na mechi yoyote ile labda jambo hilo nalo linachangia kuwapa wakati mgumu wapinzani wao pindi wanapokutana.
Hata hivyo, jambo jingine linalochangia Yanga kuwa na wakati mgumu katika mechi dhidi ya Simba ni kwamba wanakuwa katika presha kubwa ya mchezo kuliko Simba ambao huwa wanatulia.
Msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Bara, Simba ikiwa dhaifu, lakini ilitoka sare ya mabao 3-3 na Yanga, mabao ya Yanga yakifungwa na Mrisho Ngassa na Hamis Kiiza aliyefunga mawili wakati ya Simba yalifungwa na Betram Mwombeki, Joseph Owino na Gilbert Kaze.
Mzunguko wa pili timu hizo zilitoka tena sare ya bao 1- 1, bao la Simba likifungwa na Harun Chanongo wakati la Yanga lilifungwa na Simon Msuva.
Hata hivyo, Simba iliyokuwa dhaifu iliibuka mbabe mbele ya Yanga iliyokuwa katika ubora wake kwa kuinyuka mechi zote mbili za Nani Mtani Jembe kuanzia mwaka juzi walipoifunga Yanga mabao 3-1 na mwaka jana waliichapa mabao 2- 0.
Kocha mzoefu Joseph Kanakamfumu anasema kwa miaka miwili Yanga bora inasumbuliwa na Simba iliyo dhaifu na jambo hilo linatokana na wachezaji wengi wa Yanga kuathirika kisaikolojia kabla ya mchezo huo.
Anasema, “Wachezaji wa Yanga pamoja na kuwa na ubora wakifika katika mechi hiyo kisaikolojia wanakuwa hawako vizuri maana wanakuwa wameshaweka akilini kuwa Simba wamewapania hivyo wanakuwa hawajiamini tena.”
“Kosa jingine wanalofanya Yanga kwa miaka miwili mfululizo ni makocha kutowapa maandalizi mazuri wachezaji kwani wanajiamini wana kikosi bora, pia Simba wanachowazidi Yanga mara kwa mara huwa wanawajazia viungo wengi uwanjani,” anasema Kanakamfumu.
Kocha na mchambuzi wa soka, Kenny Mwaisabula anasema, “Simba imekuwa na rekodi ya kuifunga Yanga mfululizo katika miaka ya hivi karibuni, hiyo imewajengea zaidi kujiamini kwani mpira ni saikolojia hivyo Simba huingia uwanjani ikijiamini wakati Yanga wakiwa na hofu.”
“Japo Yanga Yanga iko vizuri sasa na inashiriki mashindano ya kimataifa ambayo yanawaongezea uwezo, lakini hufungwa na Simba kisaikolojia,” anasema Mwaisabula.
Mchambuzi wa soka, Edo Kumwembe anasema, “Yanga inapocheza na Simba huwa inacheza na wasiwasi tofauti na Simba ambayo inatulia.
“Hata mashabiki wa Yanga huwa na wasiwasi katika kuifunga Simba kulinganisha na upande wa pili ambao huwa umetulia, Simba wanaingia uwanjani wakijiamini kutokana na rekodi ya kuifunga Yanga miaka ya hivi karibuni.
“Hata mechi inayokuja Simba pamoja na udhaifu ilionao inaweza kuwashangaza mashabiki na wachezaji wa Yanga,” anasema Edo.
Aliyewahi kuwa kocha wa Taifa Stars na mtaalamu wa soka, Mshindo Msola anasema Simba hushinda mechi dhidi ya Yanga kwa sababu hujiaminisha kuwa ina uwezo wa kuifunga Yanga. “Kimpira Yanga inakuwa vizuri, lakini mbele ya Simba haitoki kutokana na kushindwa kutulia na kutaka kucheza soka la kujionyesha, Simba inatulia na kucheza kitimu wanapokutana na Yanga,” anasema Msola.
Wachezaji hatari
Yanga itakuwa ikiwategemea Ammis Tambwe, Mrisho Ngassa na Simon Msuva kupeleka kilio Msimbazi kwani wachezaji hao wameonekana kucheza kwa maelewano makubwa katika mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu Bara.
Tangu mechi ya Mtibwa Sugar, Prisons na Mbeya City utatu huo umefanya vizuri kwani wachezaji wote hao wameifungia mabao timu yao.
Simba wao watawategemea Emmanuel Okwi, Danny Sserunkuma na Ibrahim Ajib kupeleka maafa Yanga, wachezaji hao ndiyo wanaonekana wataibeba Simba kwa kiasi kikubwa Machi 8.
Hata hivyo, Sserunkuma (Danny) bado hajaonyesha kiwango kizuri kama alivyokuwa akipewa sifa na mashabiki wa Simba hivyo kuwatia shaka mashabiki wa klabu hiyo ambao hivi sasa wanahoji uwezo wake.
Pia kutakuwa na vita katika viungo kwani Simba itaendelea kuwatumia Jonas Mkude na Said Ndemla wakati Yanga watakuwa wakijibu mapigo kupitia kwa Haruna Niyonzima na Salum Telela.
Nguvu za Makocha
Kocha wa Simba, Goran Kopunovic ndiyo itakuwa mechi yake ya kwanza kuiongoza Simba dhidi ya Yanga hivyo atakutana na presha kubwa kwanza kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo, pili kutoka kwa viongozi. Viongozi wa timu hiyo watakuwa wameshamwambia kuwa hata kama wakikosa ubingwa, lakini raha ni kuifunga Yanga hivyo kama anataka kibarua chake kiendelee kuwapo ni lazima ahakikishe ushindi unapatikana siku hiyo.
Kocha wa Yanga, Hans Pluijm licha ya kupendwa na mashabiki na viongozi kutokana na kuibadilisha Yanga uwanjani atakuwa katika presha ya kushinda mchezo huo kwani makocha wenzake waliomtangulia walitimuliwa kwa sababu ya matokeo mabaya ya mechi kama hiyo hivyo hata yeye lolote linaweza kumkuta.
Aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Ernest Brandts alitimuliwa mwaka juzi kwa sababu Yanga ilipata kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Simba kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe wakati Mbrazil Marcio Maximo naye alitimuliwa Yanga baada ya timu hiyo kupata kipigo cha mabao 2- 0 kutoka kwa Simba kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe mwaka jana.
Ubora na udhaifu Yanga
Yanga imeonekana kukamilika kila idara hasa iko vizuri kwenye upande wa ushambuliaji ndiyo maana ni timu ya pili kufunga mabao mengi kwenye Ligi Kuu Bara mpaka hivi sasa ikiwa imefunga mabao 21, ikizidiwa bao moja tu na vinara Azam, hivyo Simba inatakiwa kuandaa beki za maana kuwawakabili Ngassa, Tambwe na Msuva ambao wana kasi kama umeme.
Pia Yanga ni nzuri hata kwenye safu ya ulinzi kwani ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache kuliko timu zote zinazoshiriki ligi ikiwa imefungwa mabao manane tu ingawa wakati mwingine beki ya timu hiyo imekuwa ikifanya makosa mara kwa mara ambayo yanaweza yakawagharimu katika mchezo huo kama wasipokuwa makini.
Simba
Nayo iko vizuri kwa uapnde wa ushambuliaji ikiongozwa na Okwi ambaye ndiye kinara wao akiwa ameshaifungia timu hiyo mabao matano, hivyo safu ya ulinzi ya Yanga inatakiwa kuwa makini sana. Pia Simba imekuwa bora kwa miaka mingi katika eneno la kiungo linaloongozwa na Jonas Mkude ingawa wapinzani wao Yanga nao hivi sasa wako vizuri eneo hilo wakiwatumia Niyonzima, Telela na Twite hivyo kuifanya mechi hiyo kuwa ya aina yake katika eneo la katikati na watu wakingoja kujua nani atamfunika mwenzake.
Simba bado ina udhaifu katika safu yake ya ulinzi hasa kama timu pinzani ikiwapiga presha mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi kwao hivyo wanatakiwa kujipanga kutokana na kasi ya mawinga na washambuliaji wa Yanga ilivyo.
Wachezaji wanaizungumziaje mechi hiyo?
“Itakuwa mechi nzuri, lakini sisi tumejiandaa kushinda na safari hii hatukubali lazima tuwafunge kwani sisi ni bora zaidi yao,” anasema mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva.
Beki wa Yanga, Juma Abdul anasema,”Ni mechi ambayo inakuwa na presha kubwa, lakini tunahitajika kutulia na kucheza mpira kwani sisi tuko vizuri zaidi yao hivyo lazima tuwafunge.”
Kwa upande wa beki wa Simba, Hassan Isihaka anasema,” Timu yetu inasuasua kwenye ligi, ni jambo linaloumiza sana, lakini tutahakikisha tunaifunga Yanga angalau tupate furaha.”
Mshambuliaji wa Simba, Elius Maguri anasema, “Sisi tunajiandaa na mechi zote siyo Yanga tu, hivyo kama kawaida kipigo kwao kiko pale pale.”MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment